ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 25, 2013

Mvua yasababisha kizaazaa Dar

Mvua kubwa iliyonyesha jana jijini Dar es Salaam, ilisababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya maeneo, hivyo nyumba kadhaa kujaa maji na baadhi ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua iliyoanza kunyesha muda wa asubuhi, pia yalisababisha hasara kubwa kutokana na vitu na mali mbalimbali kusombwa na maji.

Mwananchi lilitembelea maeneo mbalimbali na kushuhudia wananchi wakihangaika kuokoa mali zao, baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kujaa maji.
Barabara kadhaa zilikuwa hazipitiki kutokana na kujaa maji, huku baadhi ya nguzo za umeme na simu ambazo zilikuwa karibu na mifereji ziliharibiwa na kusombwa na maji.

Mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walionekana katika maeneo kadhaa ya jiji wakihangaika kuokoa baadhi ya nguzo hizo.

Athari kubwa ya mafuriko hayo ilitokea katika eneo la Kigogo Darajani ambako baadhi ya nyumba zilikuwa zimejaa maji na baadhi ya vitu vilionekana vikielea kwenye mikondo mikubwa ya maji.
Mmoja wa waathirika hao, Andrew Simon (35) alisema nyumba yake ilijaa maji kwa takriban futi nne kwenda juu na kusababisha hasara ya mali ambayo alikuwa bado hajafahamu thamani yake.“Sisi tulitoka kwenda kwenye shughuli zetu, baadaye tulipigiwa simu kwamba kuna mafuriko jambo lililonifanya nirudi haraka ndiyo nikakuta nyumba yetu ikiwa imefurika, huku vyombo vyote vikiwa vimeharibika,” alisema Simon.

Kuhusu kutii agizo la Serikali la kuwataka wananchi wa mabondeni kuyahama makazi yao, Simon alisema yeye ni mpangaji hakufahamu kuwa mafuriko yangetokea.

Mbali na Kigogo Darajani maeneo mengine ya Ubungo, Tabata, Magomeni Kagera, Jangwani, Msasani, Mikocheni, Kimara na Mbezi pia yaliathiriwa na mvua hizo hali iliyozua hofu miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.

Pia hali ilikuwa mbaya eneo la Tabata Relini nyumba na magari vilifunikwa na maji na kuwafanya watu kupanda kwenye mapaa ya nyumba zao.

Reli inayopita katika eneo hilo ilifunikwa na maji kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wasiwasi kama treni ya usafiri wa abiria itafanya kazi leo.

Eneo jingine lililoathirika ni lile la Ubungo-Maziwa, karibu na Daraja la External ambalo ujenzi wake unaendelea ambapo Meneja Masoko wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bernard Mukasa alikuwa miongoni mwa watu walioathirika na hali hiyo.

Mukasa alisema kuwa mafuriko hayo yalisababishwa na kuzibwa kwa mifereji kutokana na kazi ya ujenzi wa barabara inayoendelea katika eneo hilo.

“Tulishalalamika siku nyingi kuwa hawa wajenzi wa barabara wanaziba mifereji wakati wa kazi zao na wangetusababishia madhara mvua ikinyesha, lakini hakuna kilichofanyika”alisema Mukasa, .

Mwaka jana wakazi wa Jangwani walikumbwa na mafuriko kama hayo, walihamishiwa katika eneo la Mabwepande ambako walipewa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya kudumu. Licha ya hatua hiyo, baadhi ya wakazi hao bado wanaendelea kuishi katika eneo hilo hadi sasa.

Makamanda wanena
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englebert Kiondo alisema :“Mpaka sasa sijapokea taarifa yoyote ya matukio kuhusu mvua inayoendelea, ila wasaidizi wangu wameniambia maeneo yote yapo salama hakuna mafuriko wala maafa kama kukiwa na taarifa zaidi ya hizi nitakutaarifu”.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema mvua hiyo imesababisha adha kubwa katika mkoa wa wake kutokana na baadhi ya barabara kujaa maji na kushindwa kupitika ikiwamo ya Mwai Kibaki.

Kamanda Kenyela alisema katika barabara hiyo baadhi ya abiria walipata shida ya usafiri kwani maji yalikuwa yamejaa juu ya barabara hiyo.

Alisema Daraja la Mbezi pia lilijaa maji kusababisha watumiaji wa njia hiyo kuhangaika kuvuka. “Hakuna binadamu aliyepoteza maisha kutokana na mvua hiyo, ila baadhi ya barabara zimejaa maji na kuleta kero kwa watumiaji,” alisema Kamanda Kenyela.

Alisema baadhi ya nyumba eneo la Manzese zilijaa maji na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi, huku baadhi ya barabara zilizojaa maji zikishindwa kupitika hivyo kusababisha foleni ya magari na usumbufu kwa watumiaji wengine.

Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi hakuweza kuongea kwa kuwa alidai yupo kwenye mkutano.

Habari hii imeandikwa na Nuzulack Dausen, Bakari Kiango na Suzan Mwillo.

No comments: