ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 22, 2013

UKIJIRAHISI KWA WANAUME, WATAKUPITIA NA KUKUACHIA SHOMBO...-3

NAENDELEA kuzungumzia sababu za mwanamke kujikuta anapitiwa na wanaume kibao na kuchezewa kisha kuachiwa shombo. Wiki iliyopita nilianza kuelezea baadhi ya sababu na leo naendelea pale nilipoishia.

UKING’ANG’ANIZI
Tabia ya kung’ang’ania mambo ambayo mpenzi wako hapendi ni kati ya sababu zinazotosha kabisa kukufanya uachike. Inawezekana mpenzi hapendi aina fulani ya mavazi, tabia fulani mbaya na amekuambia kwa nini hapendi lakini wewe ukaendelea kung’ang’ania. Hili ni tatizo.
Acha uking’ang’anizi, jaribu kuwa muelewa. Mwenzi wako anapokataa kitu na kukueleza sababu za msingi, msikilize na kama unaona anachokuambia hakifai basi mjibu kwa hoja na siyo kumuwekea kiburi.

DHARAU KUPINDUKIA
Wanawake wenye dharau wapo katika nafasi kubwa sana ya kuachwa na wapenzi wao. Utakuta mwingine dharau zake zinazidi mipaka mpaka kwa ndugu wa mpenzi wake. Wakigombana kidogo, anaweza kutaja hata wazazi au ndugu wa karibu na mepenzi wake.

Ni mwanaume gani anayependa kuishi na mwanamke mwenye mdomo mchafu? Mwenye dharau? Anayeamini kila kitu anaweza mwenyewe? Sifa ya kwanza ya mwanamke ni heshima, kama mwanamke huna heshima, huwezi kuishi na mwanaume kwa muda mrefu ni wazi atakuacha.
Katika maisha ya ndoa kati ya mambo ya msingi ambayo huzingatiwa na wengi ni pamoja na kila mmoja kukubalika na ndugu wa pande zote, sasa itawezekana vipi wewe kuolewa ikiwa hata hao ndugu wenyewe unawadharau? Unawadhalilisha kwa maneno makali? Itawezekana vipi?
Mwanamke lazima uwe na heshima, uwe na haiba ya kike, siyo unaishi ilimradi siku zinakwenda. Kama huwa unaachwa kila wakati, chunguza tabia hii nayo inaweza kuwa chanzo!

KUTOTAMBUA NAFASI
Baadhi ya wanawake huwa hawataki kutambua na kutumikia nafasi zao, mwanamke hawezi kuwa sawa na mwanaume kwa kila kitu. Hata kama kwa bahati mbaya mmetofautiana, kama mwanamke ambaye anatarajiwa na mpenzi wake aje kuwa ‘kichwa cha nyumba’, lazima uonyeshe unyenyekevu.
Tulia, msikilize kwa makini, hata kama ni yeye amekosea, usitumie kauli chafu ambazo zitamuudhi. Zungumza kwa staha ukitambua nafasi ya mwenzi wako. Wakati mwingine wanawake wenyewe wanasababisha waachike. Usikubali kuwa hivyo!

KURUDIA MAKOSA
Hakuna binadamu ambaye hakosei, inaelezwa kwamba, kukosea ni sehemu ya ukamilifu wa mtu. Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema: “Ni vizuri watu wakosee ili wajifunze, huwezi kujua kitu bila kukosea, lakini unaruhusiwa kukosea mara moja tu!”
Kama ukichambua neno moja baada ya lingine ya Mwanasaikolojia huyo, utaweza kuona jinsi sentesi yake fupi ilivyo na maana kubwa. Kwa mantiki hiyo hata kama utakosea mara mia moja, hakuna tatizo, lakini yawe makosa mapya.
Kosea kila siku, lakini kitu kipya, hii inamaanisha kwamba, kwa sababu kukosea ni kujifunza, basi kama utakosea mara mia, utakuwa umejifunza pia mara mia moja.

INAWEZEKANA KUBADILIKA
Kama hayo yote hapo juu yanakuhusu, ni wazi kwamba unatakiwa kufanya mabadiliko ya haraka sana katika maisha yako, kama ni kweli unataka kuolewa na kutulia kwenye ndoa yako.
Siyo rahisi mwanaume ambaye anatafuta mke akakubali kuwa katika uhusiano na mwanamke mwenye tabia kama zako.
Badilika. Anza taratibu, rekebisha moja baada ya lingine, halafu kuwa makini katika kila jambo, mwisho wake utakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kupata mwenzi wa maisha.
Amini ninachokuambia rafiki yangu, ukiona una tabia nilizotaja hapo juu na bado mwanaume wako anaendelea kuwa na wewe, ujue hana mpango wa kukuoa. Fanya mabadiliko, inawezekana!

Global Publishers

No comments: