ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 1, 2013

Walimu wakuu waikaba koo serikali

 Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa
 Walimu wakuu wa shule za sekondari nchini wameitupia lawama serikali kwamba haiwezi kukwepa lawama za matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana kwa kuwa imechangia hali hiyo kwa kiwango kikubwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (Tahossa), Nyatagwa Manyonyi, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa kanda wa wakuu hao wa shule uliofanyika mjini hapa.
Akizungumka katika mkutano wao Kanda ya Kati alisema kuwa ongezeko la kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 limetokana na serikali kutowashirikisha walimu na wadau kwenye mabadiliko mbalimbali yanayofanyika kwenye mitalaa ya elimu. Manyonyi alisema kubadilishwa mara kwa mara kwa mitalaa kumechangia kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne.


“Hili limechangia kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu mitalaa inabadilishwa bila kuwashirikisha walimu wala wadau wa elimu…walimu wanajua kuwa mitalaa ipo, lakini ni jinsi gani wanaikabili mitalaa hiyo hawakufundishwa,” alisema.

Aidha, alisema tatizo lingine ambalo limechangia kufeli kwa wanafunzi ni serikali kutozingatia ushauri unaotolewa na walimu pamoja na wadau wa elimu.

“Serikali imekuwa na tabia ya kutojali kabisa ushauri unaotolewa na walimu na wadau wa elimu. kwa mfano, unakuta serikali bila kuuliza walimu inaondoa mitihani ya darasa la nne na ya kidato cha pili…pia inaamua kupunguza alama za kufaulu kutoka 250 hadi 70,” alisema Manyonyi na kuongeza:

“Tatizo lingine ni kutoa huduma mbovu kwa walimu na wafanyakazi wa elimu. Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu, utakuta mwalimu anapelekwa sehemu ambayo haina nyumba, usafiri wala mawasiliano na anajikuta akifanya kazi katika msongo wa mawazo kuwa ataishije kutokana na maisha kuwa magumu.”

Aliongeza kuwa walimu wamekuwa wakipata shida kwa kudai maslahi yao kwa muda mrefu na kuonekana mbele ya jamii kuwa ni watu wasiokuwa na mbele wala nyuma.

“Kitu hiki mwanzoni hakikuwapo, mwanzoni ulikuwa unaenda kwenye ualimu kwa sababu ni wito wako na unafuata misingi ya ualimu, huwezi kukuta mwalimu anafanya kitu kinyume cha maadili,” alisema Manyonyi.

Akizungumzia kuhusiana na tume ambayo serikali imeahidi kuiunda kwa ajili ya kuchunguza matokeo hayo, alisema: “Tume iundwe, lakini yale ambayo yataletwa yazingatiwe na kufanyiwa kazi.”

“Kwa sababu tume zimeundwa nyingi na hatujaona faida zake, ninachoshauri ni kwamba iundwe na ifanye kazi yake kwa uwazi na ukweli na changamoto zitakazobainika zifanyiwe kazi na hapo ndiyo tutapata mwarobaini wa kuinua elimu yetu nchini,” alisema.

Wakichangia kwenye hoja hiyo, wakuu wa shule mbalimbali za Kanda ya Kati, walisema serikali inatakiwa kuongeza bajeti katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuzingatia kile inachoshauriwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtumba ya Manispaa ya Dodoma, Esther Abius, alisema kuwa bajeti inayotengwa na serikali kwenye sekta ya elimu ni ndogo na haitoshelezi.

“Fedha ni ndogo sana kwa hiyo serikali inatakiwa iweke kipaumbele katika elimu kwa kuongeza bajeti. Pia walimu wanatakiwa kupelekwa kwenye mafunzo kwa sababu hawana mafunzo ya kutosha,” alisema.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwanakinga iliopo Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, Zuhura Chula, alisema taaluma ya elimu imeingiwa na wanasiasa na ndiyo maana imeporomoka.

“Mwalimu ili awe mwalimu ni lazima aende chuoni akasomee miaka miwili hadi mitatu, lakini sasa hivi ni siasa tu ndiyo inayotumika kwenye sekta ya ualimu, watu hawasomi, wanaingia madarasani kufundisha tu,” alisema Chula.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli.

Wanafunzi waliofeli kwa maana ya kupata sifuri ni 240,903. Waliopata daraja la nne ni 103,227, waliopata daraja la tatu nu 15,426, waliopata daraja la pili ni 6,4,53 na waliopata daraja la kwanza ni 1,641.

Baada ya kuibuka kwa kilio kikubwa nchini kote kutokana na matokeo hayo mabaya kuliko yote kuwahi kutoka nchini, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangaza kuunda tume kuchunguza kiini cha hali. Wajumbe wa tume hiyo hadi sasa hawajatangazwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: