Dar es Salaam. Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50 ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.
Habari zilizopatikana baadaye jana jioni zilidai kuwa mmiliki wa jengo, Ally Raza pamoja na mhandisi wa Kampuni iliyokuwa ikijenga jengo hilo ya Lucky Construction Limited walidakwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakijiandaa kutimka.
Viongozi wamiminika
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo la tukio saa 6:45 mchana na alipata maelezo mafupi ya tukio hilo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliyetumia dakika tisa, alimwambia Mkuu wa Mkoa na Kamanda Kova: “…mmiliki na mhandisi lazima wakamatwe mara moja.”
Kikwete baadaye alitikisa kichwa kuonyesha masikitiko na kuondoka.
Viongozi wengine waliofika ni Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal ambaye hata hivyo hakuzungumza lolote hata baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa mkoa.
Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ambaye sasa ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro alisema tukio hilo linaumiza na kusikitisha kwani limepoteza nguvu kazi ya taifa.
“Ni vigumu kupata maneno ambayo yatabeba uzito wa tukio hili lakini wajenzi wanatakiwa kuwa makini na ujenzi wao,” alisema Migiro.
Wananchi wajitokeza kuokoa
Mapema Wananchi waliojitokeza kwa kushirikiana na askari polisi na mgambo wa Jiji walioanza kuondoa kifusi cha mchanga kwa kutumia mikono kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya kuondolea kifusi hicho.
Kamanda Kova azungumza
Naye Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na majeruhi na kuahidi kuwachukulia hatua kali waliosababisha tukio hilo.
Kamanda Kova alisema wanawashikilia watu watatu kwa mahojiano ambao ni Mhandisi Mkuu, Mkaguzi Majengo na Mhandisi Majengo wote wa Halmashauri ya Ilala kwa mahojiano zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amesema kuwa biola shaka kuporomoka kwa jingo hilo kumesababishwa na uzembe.
“Huu ni uzembe kabisa…, kuna watu wamepewa kazi za kusimamia ambao inaonyesha hawakufanya kazi zao ipasavyo. “Wote waliohusika, tutawatafuta popote walipo na watatueleza…,” alisema.
Mkuu wa mkoa pia aliagiza kusitishwa kuendelea kwa ujenzi wa jengo pacha kama hilo hadi uchunguzi wa kina utakapofanyika kuona kama limetimiza vigezo.
Mtoto aliyenusurika anena
Mtoto mmoja aliyekuwa akicheza mpira na wenzake katika eneo hilo, Ally Karim alisema walikuwa tisa wakicheza mpira mara akaona jengo linadondoka na yeye akakimbia.
“Kati ya hao tisa ni mimi pekee ndiye nilikimbia lakini wengine walifukiwa chini na watatu wameokolewa lakini wengine wanne bado wako chini ya huo udongo…,” alisema Karim.
Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo, Chacha Boniface alisema jengo hilo lilikuwa na vibarua wengi juu wakiendelea na ujenzi.
“Vibarua walikuwa wengi, wengine walikuwa wakichanganya kokoto, wengine wakijenga matofali na wengine wakipiga plasta, bado mafundi wote wamefukiwa na kifusi,” alisema Boniface na kuongeza:
“Achilia mbali hao vibarua na mafundi, chini kulikuwa na magari yanapita, watoto wakicheza na mama ntilie (mama lishe) wakiuza uza chai hivyo nafikiri si chini ya watu 40 wamefukiwa”.
Naye Idd Baka alisema gari yake aina ya Noah ambayo aliiegesha katika eneo hilo na kushuka kwenda dukani kwa manunuzi, ndani ya gari hilo alikuwamo mkewe na watoto wawili, nao pia wamefunikwa na kifusi.
“Bado nawasiliana na mke wangu kwa njia ya simu, (ilikuwa saa 8 mchana) kwani mimi nilishuka kwenda dukani kurudi nikakuta kadhia hii, sijui itakuwaje” alisema Baka kwa huzuni.
Naye jirani wa jengo hilo, Ramesh Abdallah alisema alijua jengo hilo litabomoka kutokana na kujengwa chini ya viwango.
Alisema ndani ya miezi sita ilikuwa tayari ghorofa 12 zimekamilika kujengwa, hali ambayo aliitilia shaka uimara wake.
“Hata ukiangalia mchanga ni mwingi kuliko saruji, angalia hata nondo zake si za kujengea ghorofa 16, hii ndio Tanzania na wajanja ndio wanaofaidi huku watu wakipoteza maisha kizembe,” alisema Abdallah.
Wanasiasa
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi James Mbatia ambaye pia ni Mhandisi alitoa ushauri kubomoa kuta za msikiti na kibanda kilichokuwa katikati ili kurahisisha uokoaji jambo ambalo halikufanyika.
“Kama unavyoona nafasi ni ndogo, tunatakiwa kuheshimu mawazo ya kila mmoja ambaye anakuwa na nia nzuri sasa angalia matrekta (matatu) nafasi ndogo,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Ujuzi wetu katika masuala ya uokoaji bado ni mdogo, wamekuja Askari wa JKT, je, hawa askari kweli wanafundishwa kupambana na majanga?” Alihoji Mbatia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema kilichotokea ni matokeo ya rushwa na uzembe ndivyo vilivysababisha jengo hilo kuporomoka.
“Kweli unataka kusema hili jengo lilikuwa halikaguliwi? Kilichokuwa kikifanyika ni watu kula fedha bila kutekeleza wajibu wao hivyo tutaendelea kuangamia kama watu hawatakuwa makini katika sekta zao,” alisema Mtatiro.
Red Cross walia kukosa vifaa
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Dar es Salaam, Hidan Ricco alisema kuwa kazi ya uokoaji ilikuwa ngumu kwani walikosa vifaa madhubuti kwa kazi hiyo.
Alisema pia kuwa vifaa vilikuwa vya ‘kuungaunga’ kutoka taasisi mbalimbali ambavyo hata hivyo kwa kiasi fulani vilisaidia.
Alipoulizwa kuhusu ajali hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema sio kila mtu anazungumza kuhusu tukio hilo na kusisitiza kuwa atafutwe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.
Naye Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Flora Mwombeki ambaye alikuwa eneo la tukio jana alisema bodi hiyo inautambua mradi wa ujenzi wa jengo hilo lililokuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Ltd.
“Mimi sio msemaji wa CRB ila mradi huu tunautambua, kuhusu nani alikuwa mkandarasi siwezi kukujibu kwa kuwa sioni kibao kinachoonyesha kuwa ni kampuni ya Lucky, nadhani baadaye ukiwatafuta wahusika wakuu watakupa ufafanuzi,” alisema Mwombeki.
Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka, kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.
Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.
Juzi 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.
Mwaka 2006 pia liliwahi kuporomoka jengo na kuua mtu mmoja ambapo baada ya tukio hilo, tume ya kukagua majengo iliundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa na ripoti yake ilikabidhiwa serikalini lakini mpaka leo hii ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani.
Imeandikwa na Ibrahim Bakar, Ibrahim Yamola, Pamela Chilongola, Fidelis Butahe, Kelvin Matandiko, Aisha Ngoma, Aidan Mhando
Mwananchi
No comments:
Post a Comment