Dar es Salaam. Mgombea ubunge katika Jimbo la Kisii, nchini Kenya katika uchaguzi mkuu uliofanyika Machi, 2013, Donbosco Gichana (34), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kutakatisha fedha zaidi ya Sh6 bilioni.
Gichana ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu nchini Kenya, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya, akisaidiana na Wakili wa Serikali Tumaini Kweka.
Akisoma mashtaka mshtakiwa huyo, Wakili Oswald alidai kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 jijini Nairobi, Kenya; Arusha na Dar es Salaam, nchini Tanzania, akiwa na washtakiwa wengine ambao hawapo mahakamani walikula njama za kutenda kosa la kutakatisha fedha haramu.
Wakili Oswald alidai kuwa mshtakiwa huyo pamoja na wenzake walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 12 cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu, namba 12 ya mwaka 2006.
Katika shtaka la pili, anadaiwa kutenda kosa la utakatishaji fedha. Anadaiwa kuwa kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 kwa kupotosha ukweli wa chanzo cha fedha alizokuwa nazo, alizihamisha kutoka Kenya kwenda Arusha na kisha Dar es Salaam.
Katika shtaka la pili, anadaiwa kutenda kosa la utakatishaji fedha. Anadaiwa kuwa kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 kwa kupotosha ukweli wa chanzo cha fedha alizokuwa nazo, alizihamisha kutoka Kenya kwenda Arusha na kisha Dar es Salaam.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuhamisha fedha hizo kwa kutumia hundi yenye thamani ya Dola za Marekani 4,940,363.25, ambazo anadaiwa kuwa aliziweka katika akaunti namba 02J1036325000 inayomilikiwa na Kampuni ya Moyale Precious Germs Enterprises katika Benki ya CRDB Tawi la Meru, Arusha.
Wakili Oswald alidai mahakamani hapo kuwa baadaye mshtakiwa huyo alihamisha tena fedha hizo kutoka Tawi la Meru, Arusha kwenda Makao Makuu ya Benki ya CRDB Dar es Salaam, kwa nia ya kufanya utaratibu wa kuzitoa, huku akijua hundi ilikuwa ya kughushi. Hakimu Emillius Mchauru alisema kesi itatajwa Aprili1 Aprili 18 .
Mwananchi
No comments:
Post a Comment