ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 3, 2013

BARAZA KUU LAPITISHA MKATABA WA BIASHARA YA SILAHA KWA KURA

Ubao  ukionyesha kila nchi ilivyopiga kura  kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti  Biashara ya  Silaha ( ATT), Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  jana Jumanne lililazimika kuupigia kura  Mkataba huo baada ya kushindikana kuupitisha kwa kauli moja wiki iliyopita, kushindikana huko kulitokana na Ujumbe wa Syria, Iran na Korea ya  Kaskazini ( DPRK) kutoa hoja zilizosema kwamba zisingeunga mkono  Mkataba huo kwa kuwa ulikuwa umeegemea zaidi maslahi ya wakubwa. katika Upigaji kura uliofanyika siku ya Jumanne, nchi 154 zilipiga kura ya ndiyo, nchi tatu ( Syria, Iran, na  Korea ya Kaskazini ) zilipiga kura ya hapana na  nchi  23 hazikufungamana na upande wowote. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zilizopiga kura ya ndiyo.
Na Mwandishi Maalum

Hatimaye, Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti Biashara ya Silaha, (ATT) ambao  wiki  iliyopita ulishindikana kupitishwa kwa kauli  moja baada ya Ujumbe wa  Syria,  Korea ya Kaskazini  ( DPRK)na Iran kutia ngumu,  umepitishwa  na Baraza Kuu la  67 la Umoja wa Mataifa kwa kupigwa kura.
 Mkataba huo umepitishwa kwa kura 154 za ndiyo,  huku Syria,  Iran na  Korea ya Kaskazini ( DPRK) zikipiga kura ya hapana na nchi 23 zikapiga  kura ya kutofungamana na upande wowote.
Baraza hilo lilihitaji kura 97 tu kuupitisha  Mkataba tofauti na wiki iliyopita ambapo wajumbe  kutoka nchi 193 walioshiriki majadiliano ya wiki mbili  wakati wa MKutano wa  Mwisho wa Mkataba wa Silaha  walitakiwa kuupitisha  kwa kuunga mkono kwa kauli  moja badala ya kupiga kura.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya mataifa yaliyopiga kura ya ndiyo, na hasa ikizingatiwa kwamba katika miaka yote ya majadiliano ya kuandaa  Mkataba huu, Tanzania imesimama kidete kwa kutaka   silaha ndogo na nyepesi ziwe sehemu ya mkataba pamoja na  risasi kwa kile ambacho Tanzania imekuwa ikisisitiza kwamba   silaha hizo zimekuwa tatizo kubwa na tishio la amani na usalama katika eneo la nchi za Maziwa Makuu.

Baada ya kuona kwamba usiku ule wa  Marchi 28, Mkataba ulikuwa umekwama kupitshwa kwa kauli moja,  nchi moja ilitoa pendekezo la kutaka liandaliwe Azimio ambalo lingepelekea  Mkataba huo uwasilishwe   katika Baraza Kuu ili ukaamuliwe kwa  kupigiwa kura.
 Mkataba  utaanza kufanya kazi ndani ya siku 90 baada ya kuwa umeridhiwa kwa sahihi zipatazo   50.
Kupitishwa kwa  Mkataba huo  kwa kwanza na wa aina yake na Baraza Kuu,   kuna andika historia  ya aina yake katika Umoja wa Mataifa, na hasa ikizingatiwa kwamba biashara ya silaha ni biashara nyeti na yenye faida kubwa kuliko hata biashara ya madawa ya binadamu.
Lakini pamoja na faida kubwa inayopatika kutokana na biashara hiyo,   maisha ya mamilioni ya watu wasiokuwa na  hatia  yanapotea kila mwaka kutokana na  matumizi yasiyo halali ya sihala hasa zile nyepesi na ndogo ndogo.
Dhumuni kuu la  Mkatana huu pamoja na mambo mengine ni  kusimamia na kuratibu Biashara  ya silaha zikiwamo,  mizinga ya kivita, magari ya kivita,  ndege za kivita,  helkpota za mashambuli, meli za kivita, makombora , silaha ndogo na  nyepesi.
Aidha Mkataba  pamoja na masuala mengine hautaingiali uhuru wa nchi kununua silaha kwa matumizi yake ya ndani na haki ya kujilinda na kulinda mipaka yake, vile vile mkataba hauzui kufanya biashara au  kusafirisha aina yoyote ile ya silaha wala kuingilia taratibu ambazo nchi itakuwa   tayari imejiweka katika kudhibiti masuala ya silaha.
Inatarajiwa kwamba utekelezaji wa mkataba huu  utasaidia sana kudhibiti silaha zisiangukie kwa makundi mbalimbali yakiwamo ya kigaidi na hivyo kujenga na kuimarisha amani na usalama wa jumuiya ya kimataifa.


No comments: