Advertisements

Tuesday, April 9, 2013

CHUMVI: NI MUHIMU LAKINI NI HATARI


TANGU enzi na enzi, chumvi imekuwa miongoni mwa viungo muhimu vya chakula. Mbali ya kuwa na madhara itumiwapo vibaya, lakini bado ni muhimu kwa mwili wa binadamu. Utafiti wa hivi karibuni nchini Marekani na nchi zingine zinazoendelea na zilizoendelea, umebaini kuwa chumvi ndiyo chanzo cha magonjwa mengi ya shinikizo la damu na moyo.
Kwa mujibu wa utafiti wa awali wa Machi 21, mwaka huu uliowasilishwa New OrleƔns, nchini Marekani, kwenye Mkutano wa Chama cha wenye Matatizo ya moyo, imebainika kuwa matumizi ya chumvi kupita kiasi yalichangia vifo vilivyohusiana na matatizo ya moyo vya watu milioni 2.3 duniani. Asilimia 42 ya hao walikufa kutokana na magonjwa ya moyo na asilimia 41 walikufa kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Hii ni kwa mujibu wa vifo vilivyorekodiwa mwaka 2010 tu.
Idadi hii inajumuisha walaji wa chumvi zilizomo kwenye vyakula vingi vya kwenye makopo na maboksi ambavyo hutumia zaidi chumvi zenye kiwango kingi cha ‘sodium’ inayoongezwa wakati wa mchakato wa kuitengeneza kiwandani.
Aidha, katika utafiti huo, imegundulika kuwa nchi inayoongoza kwa watu wake kula chumvi nyingi sana ni nchi ya Kazakhstan iliyoko Asia ya Kati jirani na nchi ya Urusi. Inaelezwa kuwa kwa wastani Wakazakhstan wanakula kiasi cha miligram 6000 za chumvi (zaidi ya vijiko vidogo vitatu) kwa siku. Wakati nchi za Kenya na Malawi ndizo zenye kiwango kidogo sana za ulaji wa chumvi, ambapo wastani wake ni miligrams 2000 tu (sawa na kijiko kidogo kimoja).
Wastani wa kiwango cha chumvi unaokubalika kiafya ambao mtu anatakiwa kula kwa siku ni miligram 1000 tu, sawa na nusu kijiko kidogo cha chumvi kwa siku nzima, chumvi inapozidi kiwango hicho mwilini, huwa ndiyo chanzo cha matatizo mengine ya kiafya kama tutakavyoendelea kuona hapa chini.

AINA YA CHUMVI SAHIHI
Kuna matatizo makubwa mawili kwenye ulaji wa chumvi ambayo ndiyo huifanya chumvi kuwa hatari ikifikia hatua fulani. Mosi ni watu kuzidisha kiwango cha chumvi kwa kuweka chumvi nyingi kwenye vyakula vyao au kununua vyakula vilivyokwisha tengenezwa na kuwekewa chumvi nyingi.
Pili, kula chumvi isiyosahihi. Chumvi ni miongoni mwa vyakula au madini yanayopatikana kiasili na siyo kwa kutengeneza, ili kupata faida ya chumvi iliyokusudiwa ni lazima utumie chumvi ambayo haijatengenezwa na kuongezewa kemikali zingine zenye madhara mwilini.
Chumvi asilia huwa na virutubisho muhimu ambavyo ni ‘sodium’ na ‘chloride’ ambavyo huingia mwilini kwa kula dayati sahihi. Lakini kwa bahati mbaya sana chumvi inayotumiwa na watu wengi haina madini hayo ya kutosha, kutokana na kutengenezwa kiwandani upya kwa kusafishwa (refined), zaidi huongezewa madini joto tu.
Utumiaji wa chumvi sahihi na kwa kiwango kinachotakiwa, una faida nyingi mwilini, ikiwemo kuimarisha na kudhibiti shinikizo la damu, kuboresha ufanisi wa misuli ya mwili, kuboresha ufanisi wa ubongo na faida nyingine nyingi. Lakini ili kupata faida hizo ni lazima iwe chumvi asilia, ambayo haijachakachuliwa wala kuongezwa kemikali zingine.
Kwa maana nyingine, ulaji wa chumvi iliyoondolewa madini yake muhimu na kuongezewa kemikali zingine pamoja na kula kupita kiwango cha kawaida, chumvi hugeuka na kuwa na madhara badala ya faida mwilini. Hugeuka na kuwa ndiyo chanzo cha matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
Hivyo, hatuna budi kupunguza matumizi yetu ya chumvi na kutumia chumvi asilia (inayo chimbwa na kuuzwa kienyeji ni bora zaidi), kuliko ile inayopitia kiwandani ambako huondolewa viini vyake muhimu vya ‘Sodium’ na ‘Chloride’ na kuongezewa kemikali hatari.

GPL

No comments: