Advertisements

Tuesday, April 9, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA


MAPENZI ni muhimu kijamii, uwepo wake unafanya mambo mengi yakae sawa. Yasingekuwepo dunia kila kona ingekuwa na uwanja wa fujo. Siku zote huyaita sanaa kiranja, kwa maana yanamhusu kila mmoja wetu. Ukiona machafuko ujue yamepungua au yametoweka.
“Upendo na huruma ni mambo ya lazima. Yakikosekana, ubinadamu hautakuwepo,” alisema Dalai Lama.
Kwa tafsiri iliyonyooka ni kuwa uwepo wa mapenzi ndipo hujenga familia imara. Ukiona nyumba inayumba, migogoro inatawala kati ya wazazi au watoto, hapo hupaswi kuumiza kichwa, zaidi unatakiwa kupigia mstari kwamba upendo haupo.
Hata nchi, vita ya wenyewe kwa wenyewe chanzo chake ni kutokuwepo kwa upendo. Kuna vitu vitatu vinategemeana, ila viwili ndiyo zaidi. Upendo, amani na huruma. Vinahitajika muda wote kwa pamoja lakini kuna kinachoanza na vingine vinafuata.
Viwili vya zaidi ni upendo na amani, halafu huruma hufuata. Palipo na upendo amani huja yenyewe, halafu ieleweke kuwa amani haitakuwepo kama upendo hakuna. Kwa maana hiyo, upendo ndiyo chemchemi ya furaha, faraja na utulivu.
Ukishakubaliana na hoja hii kuwa upendo ndiyo kila kitu, sasa weka mkazo kuhakikisha hapo unapofanya kazi, unapoishi na popote pale ambako huwa unakwenda, kuna upendo. Amua leo na uhakikisha kati yako na mwenzi wako kuna upendo ulioshiba. Huo ni msingi wa kufurahia maisha.
Maisha ya kimapenzi ni kama kioo. Yaani ukiyachekea nayo yatakuchekea, ila ukiyanunia, nayo yatakukunjia sura. Hakuna njia mbadala ya kuyachekea mapenzi zaidi ya kuwekeza upendo pale ambapo unahitaji kupendwa. Ni kichekesho kwa mbaguzi, mwenye chuki kwa wenzake halafu eti anataka apendwe.
Kosa kubwa ambalo wengi wetu hulifanya ni kujenga matarajio. Kila mmoja wetu anataka afanyiwe mengi lakini yeye mwenyewe huwa hajiulizi ni kipi anachopaswa kufanya kwa lengo la kumridhisha mwenzake. Ni vizuri kujua kuwa kadiri wewe unavyotaraji kufanyiwa na mwenzako anatarajia umfanyie.
Katika mapenzi hutakiwi kuingia na sura bandia. Kila ‘aliyefeki’ uhusika wake kwenye uhusiano wa kimapenzi, aliishia kuharibikiwa. Hata kama una udhaifu wako, acha uonekane ili uwe huru muda wote. Vinginevyo, utajichimbia kwenye dunia ya mateso ya kujitakia.
Kukubali udhaifu wako uonekane, kunakupa sifa kwamba wewe ni mwelewa. Hilo ni jambo la muhimu kuliko kujionesha wewe ni mkamilifu, halafu baadaye yale uliyokuwa unayaficha yanaonekana, sasa inakuwa aibu kwako. Mtu bandia kila siku hufeli, mwenye uhalisi wake atazidi kwenda mbele.
Uhusiano wa kimapenzi siyo kitu rahisi. Huweka wazi kila kitu ambacho mtu anakifikiria ndani yake au anachokitarajia. Kwa kawaida, mtu anavyohusika kwenye mapenzi ndivyo ambavyo hutoa kielelezo cha namna anavyotaka maisha yake na mwenzi wake yawe.
Mapenzi yanakutaka uwe unatabasamu ili na yenyewe yatabasamu kwa ajili yako. Huwezi kuwa kwenye kipindi kibaya halafu ukayatendea haki mapenzi. Ukiwa na siku mbaya, watu wanaokuzunguka, hususan mwenzi wako atakugundua. Vivyo hivyo, ukiwa hauna furaha.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: