TANGA: Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki parokia ya Chumbageni, Padre James Kabosa ameponea chupuchupu kuswekwa ndani na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Tukio hilo limethibitishwa na Mkuu wa wilaya mwenyewe, Padre Kabosa na msemaji wa Askofu, Padre Peter Kagaba walipozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti.
Imedaiwa kuwa padre huyo aliepuka kuswekwa ndani kwa kuondoka ofisini hapo baada ya kutofautiana na mkuu huyo wa wilaya na hivyo kumuita mkuu wa polisi wa wilaya afike na kumsweka ndani ndipo wazee wa kanisa waliokuwa wameambatana naye kumsihi Padre aondoke.
Imedaiwa kuwa baada ya tukio hilo Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Baba Askofu Anthon Banzi, alifika ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya akitaka kujua chanzo cha Padre Kabosa kufukuzwa na kutishiwa kuswekwa ndani.
Habari zimebainisha kuwa baada ya mkuu wa wilaya kuona Askofu ofisini akiwa na waumini alimuelewesha kiini cha kumtimua Padre na kumuomba msamaha.Waumini waliokuwa wamemsindikiza Askofu wao walishikwa na butwaa baada ya kumuona mkuu wa wilaya huyo akipiga magoti mbele ya Askofu Banzi na kuomba abarikiwe na askofu kwa madai mumewe pia ni mkatoliki abarikiwe ili Mungu amsaidie katika kazi zake za kuiongoza jamii.
Akiongea na NIPASHE kuhusu tukio hilo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Mikael, Kiule Msofe, alisema tukio la kufukuzwa kwa Padre lilitokea Machi 27, mwaka huu majira ya saa 8 mchana na tukio la Askofu kufika kwa mkuu huyo wa wilaya lilitokea Aprili 3 na kuwa matukio yote mawili alikuwapo na kuyashuhudia.
Kuhusu chanzo cha tukio hilo, Kiule alisema ni kutokana na mgogoro wa ardhi wa eneo la wazi lililogawanywa na diwani wa kata ya Nguvumali, Selemani Mhina (sele boss) CCM, lililopo mbele ya kanisa la Kigango cha Majani Mapana kinyume cha sheria za ardhi.
Alisema kanisa katoliki lilishaomba eneo hilo zaidi ya mara mbili kwa Jiji la Tanga na kujibiwa kuwa ni eneo la wazi na lakini lilitolewa kwa wafanyabiashara kwa madai kuwa ni agizo la mkuu wa wilaya ili kujenga mashine za kusaga nafaka.
Kwa upande wa padre Kabosa alikiri kupatwa na kadhia hiyo lakini alidai kuwa tayari suala hilo linashughulikiwa na viongozi wakuu wa kanisa hilo kwa hatua zaidi za kurejesha amani na mshikamano ulioonekana kukosekana.
Naye Mkuu wa wilaya, Dendego alipotakiwa kuelezea shutuma hizo alikiri ujio wa padre Kabosa ofisini kwake na kutofautiana kimazungumzo lakini alidai kuwa alimuamuru kuondoka ofisini hapo kwa kuwa hakumtambua kama ni kiongozi wa dini.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alikanusha tuhuma za kueneza udini na kwamba hilo halikufanyika kwa ajili ya udini bali ni moja ya matokeo ya kiutendaji.
Alimtupia lawama na kumtaja diwani Mhina kuwa ndiye anayechochea mgogoro huo kwa kueneza udini kuwa yeye anawapendelea waislamu jambo ambalo ni hatari.
No comments:
Post a Comment