Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na waislamu mbali mbali alipofika Mwera kwa ajili ya ufunguzi wa Masjid Maulana
Viongozi wa misikiti wametakiwa kutunza nidhamu katika nyumba hizo za ibada, na kuachana na tabia ya kugombaniana uongozi, ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima…
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Al-hajj Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya ufunguzi wa “Masjid Maulana” ulioko Mwera, katika Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema misikiti ni nyumba za ibada, hivyo hakuna sababu kwa waislamu kugombania misikiti, na badala yake viongozi watakaochaguliwa wawajibike kutunza nidhamu na kuendeleza harakati za kiibada ikiwa ni pamoja na kuendeleza darsa na mijadala ya kuuendeleza Uislamu.
Maalim Seif amewataka waumini wa msikiti huo kushirikiana na kusaidiana katika mambo mbali mbali ya kijamii, sambamba na kuchangia harakati za misikiti kwa kuhakikisha kuwa wanasaidia kutatua kasoro zinazoweza kujitokeza.
“Ipo misikiti inawaumini wengi wenye uwezo, lakini hufikia hatua ya waumini kufanya ibada kizani kutokana na kukosa fedha za kununulia umeme, au kuna mingine sehemu za vyooni hufungwa kwa muda mrefu kwa sababu hali ya usafi hairidhishi”, alitanabahisha.
Amewahimiza viongozi wa msikiti huo kuendeleza darsa ambazo zitasaidia kuwafunza vijana maadili mema na kuweza kutekeleza ibada zao kwa uhakika.
Kwa upande wake Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali, amesema waislamu wana wajibu wa kuitunza na kuihifadhi misikiti, ili iweze kuwa katika hali nzuri na usafi wakati wote.
Amesisitiza haja kwa waislamu kuitumia misikiti kwa shughuli za ibada na elimu, na kuwataka viongozi kuwa mifano bora katika jamii juu ya kuendeleza maadili ya kiislamu na ibada.
Hassan Hamad (OMKR)
No comments:
Post a Comment