ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 28, 2013

Mabilioni ya bajeti yalivuruga Bunge Dodoma

Kitendo cha Bunge kuidhinisha matumizi ya fedha kiasi cha Sh118bilioni katika wizara tatu licha ya kupingwa na kulalamikiwa na wabunge wengi kwamba zingepelekwa katika maendeleo, kimepingwa na wasomi na wanaharakati nchini ambao wamewataka wawakilishi hao wa wananchi kuikataa bajeti ya Serikali.

Fedha hizo ni zile zilizolalamikiwa na wabunge wakati wa uwasilishwaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na ile ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kutokana na kuwapo mvutano mkali bungeni, kwa nyakati tofauti Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, walilazimika kutoa maelezo ya kina kuwashawishi wabunge wakubali ili fedha hizo ziidhinishwe katika bajeti husika kwa ajili ya matumizi ya mwaka mpya wa fedha unaoanza Juni mwaka huu.Fedha hizo ni Sh74 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mfuko wa pembejeo, Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa, Sh88 bilioni za Ruzuku ya Mfuko wa Pembejeo na Sh29 bilioni kwa ajili ya kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya Serikali.

Baadhi ya wabunge walilalamikia fedha hizo wakisema kuwa ni ulaji kwa wakubwa.

Wakizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya Fedha itapitishwa mwishoni, wabunge wanatakiwa kuikataa hadi mambo muhimu katika bajeti zilizotangulia kusomwa, yatakapofanyiwa kazi.

“Binafsi naona hiyo ndiyo njia nzuri iliyobaki, wabunge wanatakiwa kuamua mambo kwa masilahi ya taifa na siyo kwa manufaa na maslahi yao binafsi,” alisema Profesa Mbwete.

Aliwataka wabunge kutumia fursa hiyo kumbana Waziri wa Fedha ili kuhakikisha kuwa fedha zaidi zinaongezwa, au kupunguzwa katika maeneo mengine, kwa ajili ya kupelekwa katika maendeleo.

Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), alisema kuwa fedha zaidi zinatakiwa kuongezwa katika bajeti ya maendeleo, badala ya matumizi ya kawaida.

“Maendeleo yatapatikana kwa haraka kama tutawekeza zaidi ya asilimia 20 ya bajeti yetu kwenye matumizi ya maendeleo. Hii ni tofauti na sasa, ambapo asilimia 90 ya fedha zinazotengwa zinakwenda katika matumizi ya kawaida,” alisema.

Alisema umefikia wakati wa Serikali kuachana na matumizi yasiyokuwa na ulazima, kama ununuzi wa samani za ofisini.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi aliwataka wabunge kuwa makini na kukubali hoja kwa manufaa ya taifa, siyo kishabiki.

“Wabunge wanatakiwa kutenga muda zaidi kwa ajili ya kupitia bajeti za wizara husika kiundani zaidi, ili kujua mambo ya msingi, baadaye kuyajengea hoja,” alisema na kuongeza:

“Hata kama watakubaliana hoja ipite, basi ipite ikiwa tayari kila kitu kimekwenda sawa. Lakini kama wataamua tu kupitisha mambo kwa sababu wanazozijua wao ni wazi kuwa watakuwa hawawatendei haki Watanzania.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema kwamba siyo kila fedha inayotengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi fulani, haistahili kuhojiwa matumizi na malengo yake.

“Zipo fedha ambazo zinapelekwa kienyeji tu katika sekta mbalimbali, lakini haziendi kuleta jipya, kila mwaka kumekuwa na malalamiko ya kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali, wabunge wanatakiwa kuwa macho na kutokubali kitu hiki kabisa,” alisema Kibamba.

Ilivyokuwa

Mvutano mkali uliozuka bungeni kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi ulimlazimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kutoa ufafanuzi.

Katika ufafanuzi wake alisema kwamba fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kununua eneo la hekta 129 zilizopo eneo la Iyumba mkoani Dodoma, ili liwe likitumika kwa mazishi ya viongozi hao kwa mujibu wa Sheria ya Maziko ya mwaka 2006.

Ufafanuzi huo ulitolewa baada ya wabunge kulalamikia kutenga Sh1 bilioni kwa mazishi ya viongozi wa Serikali, wakati wananchi wanaishi hali duni ya umaskini wakisema ni ulaji kwa baadhi ya watu.

Hata hivyo, tangu kupitishwa Sheria ya Maziko ya Viongozi mwaka 2006, hakuna kiongozi ambaye amezikwa Dodoma huku wengi wakizikwa mikoa wanayotoka.

Mvutano mwingine uliibuka wakati wa Bajeti ya Kilimo ambayo ilipita baada ya Waziri Mkuu kusimama na kutoa rai kwa wabunge.

Katika bajeti hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iliomba jumla ya Sh328 bilioni kwa maendeleo ya kawaida huku ikiomba nyongeza ya Sh88 bilioni endapo ruzuku ya pembejeo itatolewa kwa utaratibu wa vocha na Sh130 bilioni endapo ruzuku ya pembejeo itatolewa kwa utaratibu wa mikopo na Sh5 bilioni kwa ushirika.

Masuala yaliyoleta sokomoko katika bajeti hiyo kubwa ni stakabadhi ghalani na mfumo wa ruzuku ya pembejeo kutumia vocha.
Mwananchi

No comments: