
Mpenzi msomaji, ukatili wa kijinsia siyo tu unadhalilisha, bali pia unachipua usugu kwa wale wanausulubiwa hasa pale wanapodundwa karibu kila siku iwe ni mke au mume lakini wanamezea. Hivi ni kwanini?
Katika familia zetu, wapo watu wanaodundana kila wakati utadhani wako katika ulimwengu wa kufikirika. Yaani wameshachukulia kuwa ndio mfumo wa maisha wanaoutaka, jambo ambalo siyo sahihi. Hayo ni mateso makubwa sana kwao.
Tukumbuke kwamba kabla ya watu kuamua kuishi pamoja kama mke na mume, hubembelezana sana. Kila mmoja huonyesha upendo, hata kujiona kuwa hali hiyo itaendelea daima na milele.Kumbe kwa wengine, hiyo ni ndoano ya kumnasa mwenzake na wanapokuwa sasa wameshikamana kuwa kitu kimoja, ndipo kila mmoja hufungua makucha yake na hapo ndipo mahusiano ya upendo hubadilika taratibu na wengine mwishowe huwa maadui wakubwa.
Ibilisi akishaingilia kati, husambaratisha upendo huo na kuruhusu vitimbwi vya kila aina ambavyo huchipua uhasama ambao huwa fedheha na mateso ndani ya nyumba au familia husika.
Kwa mfano, ipo familia moja nilisimuliwa hivi majuzi kwamba hazipiti siku mbili bila kudundana. Inasemekana kuwa kijana huyo anaye mke wake na watoto wawili sehemu nyingine.
Lakini pia huyu anayenisimulia anasema kuwa kijana huyu ambaye amepangisha nyumba jirani na hapo anapoishi, ana mwanamke mwingine anaishi naye ambaye alikuwa mhudumu wa baa.
Hazipiti siku mbili bila kupigana. Na kibaya zaidi mwanamke ndiye anayepigwa zaidi. Hufikia hatua anafukuzwa na kwenda kwao lakini baada ya mwezi anarudi tena na kazi ya kupigwa inarejea pale pale.
Swali ni je, kwanini wawili hawa wanadundana kila wakati? Bwana ana kazi zake zinazomuingizia kipato, hutoka asubuhi na kurejea jioni. Mama ni wa nyumbani lakini mume akirejea utasikia wanadundana.
Lazima kuna tatizo hapo. Labda mke ni mtembezi na mume hupata habari zake akiwa hayupo. Au huenda mwanamke ni mjeuri, hapiki chakula kinachomvutia mume, mvivu na kadhalika. Sasa ikifikia hivyo lazima mume anakasirika.
Hata hivyo, nadhani kama mwanaume akigundua kasoro za mwanamke kama hizo nilizotaja hapo juu, hakuna sababu ya kumpiga kama punda ni afadhali kama wanaishi kihalali wasuluhishe kupitia majadiliano ya kindugu.
Upo msemo kuwa mwanamke hupigwa kwa ncha ya khanga. Yaani mwanamke hapaswi kupigwa kwa kuumizwa. Ikibidi angea naye na ikishindikana kama umemtoa kwa wazazi wake mtaliki akaendeleze maisha kwingine.
Hata hivyo, wako wanawake ambao ambao wametumika vema katika nyumba zao na hawa ni wale ambao wamefunzwa namna ya kuishi ndani ya jamii pasipo mikwaruzano.
Hawa wanaheshimu wenzi wao na kutii amri pasipo shuruti. Lakini wengine wamekuwa mabaunsa na wepesi sana wa kuwadunda waume zao bila hofu ya Mungu wakati maandiko matakatifu yameweka mambo mengi bayana.
Tutizame maandiko katika Biblia Takatifu ambayo yameweka wazi namna ambavyo mwanamke anapaswa kuwa mtulivu na mtii kwa mumewe. Kwa mfano, waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timotheo, aya ile ya 2 kuanzia mstari wa 11 hadi 15 anasema;
Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanaume, bali katika utulivu.
Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganya, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.
Ujumbe huo juu una mafundisho mengi kwa mwanamke. Kwanza anahimizwa utulivu na utii kwa mumewe. Lakini wengi hawazingatii jambo hili ndio maana wanadundwa hovyo.
Pia anaambiwa hapaswi kumtawala mumewe. Lakini katika familia zetu nyingi kinamama wamekuwa wehu na hasa wale waliopata mwanya wa ujasiriamali. Kinamama kufanya biashara kwa ajili ya kujiongezea kipato ni jambo jema sana.
Lakini baadhi wamejikuta wana pesa na kuanza kuwanyanyasa waume zao. Ndio hao wanaoduriki hata kuwadunda waume zao kwa sababu ya jeuri ya pesa. Hili ni kosa kwani wanapaswa kuwaheshimu na siyo kuwatawala kwa aina yoyote ile. Tukumbuke mwanaume ni kichwa yaani ndiye nguzo ya familia.
Adamu(mwanaume) ndiye aliyeumbwa kwanza na Hawa baadaye kama Timotheo alivyotuambia hapo juu. Na kwamba Adamu hakudanganywa ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa, lakini ataokolewa kwa uzazi wake…
Mpenzi msomaji, huo ndio ujumbe wangu kwa kinamama na kinababa kwa leo. Upendo, Amani, Utulivu na ustahimilivu viwe msingi na nguzo kwa maisha yetu. Je, unayo maoni yoyote juu ya jambo hili?
No comments:
Post a Comment