ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 8, 2013

Maisha ya Polisi;Waeleza kwanini wengi wanapokea rushwa

Baadhi ya askari polisi kutoka mikoa mbalimbali nchini wameeleza sababu za wao kujiingiza katika kupokea rushwa kutoka kwa raia kuwa ni kutokana na kupata kipato kidogo ambacho hakitoshi kuhudumia familia zao.
Baadhi ya polisi waliozungumza nagazeti hilikutoka mkoani Mbeya kwa nyakati tofauti wanasema kuwa hali ya maisha yao ni mbaya, hasa kwa askari wasio na vyeo ambao ndio wanaoishi katika nyumba za polisi.
“Nyumba tunazoishi pale eneo la Sinde ni aibu, sisi wenye familia haifai hata kusimulia, kwani unapewa chumba kimoja cha kulala na sebule halafu unawatoto unafikiri nini kinaendelea hapo,”anasema askari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Anasema mara nyingi wamekuwa wakiwalaza watoto sebuleni bila kujali jinsia zao, kwamba wakati mwingine iliwazazi wanapohitaji kukutana faragha huwalazimu kwenda kulala katika nyumba za wageni.
“Huwezi kufanya faragha na mkeo huku watoto wakiwa wamelala sebuleni halafu wa jinsia moja hivyo kwa sisi wengine tunaamua kuingia gharama nyingine ya kwenda kulala katika nyumba za wageni ili kuepuka kuwaharibu watoto kisaikolojia,” anasema.
Askari mwingine kwa sharti la kutotajwa jina anasema mazingira ya nyumba hizo ni machafu na kuna msongamano mkubwa wa watu hasa katika huduma ya choo kwani hutumiwa na watu wengi.
“Ukitaka kuona adha ya choo ni muda wa asubuhi ambapo kila mmoja anahitaji huduma ya bafu kwa ajili ya kuoga na kuwahi kazini,  inakuwa kama sinema vile hivyo mazingira ya nyumba zetu bado hayafai…,” anasema.
Kwa upande wake Koplo Atupele anasema kuwa kwa wale ambao ndiyo wanaanza kazi hupangiwa kulala kwenye bwalo ambapo hutandika magodoro chini, hulala eneo hilo mpaka watakapopata nafasi katika nyumba za serikali.
“Ndiyo maana utakuta askari wengine wanaamua kwenda kuishi uraiani ili kukwepa adha ambayo wanaipata kwenye kota,” anasema.
Anasema maisha halisi ya polisi kwa kiasi fulani yanachangia kujiingiza katika vitendo vya kupokea rushwa na kukiuka maadili.
Mtwara
Maisha duni kwa askari polisi wa vyeo vya chini nchini yanaelezwa na baadhi ya polisi mkoani Mtwara kuwa ni chanzo cha wao  kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na unyanyasaji kwa wananchi.
“Kwa ujumla mazingira ni duni, tunakwenda lindoni tukiwa hakuna sehemu maalum kwa ajili ya lindo, mvua yetu, jua letu, ukirudi ofisini mabosi nao wanakunyanyasa…, ili uishi vizuri kwa sisi askari wadogo ni lazima ‘uji-attach’ na bosi ambaye akikupangia kazi yenye maslahi lazima umuachie kitu kidogo (fedha)” anasema mmoja wa polisi hao.
Anaongeza;“Kama hapa Mtwara ukipelekwa kulinda Msimbati au Madimba (kunakojengwa kiwanda cha kukamua gesi) ni lazima ukate pesa kwa mkubwa.”
Wakizungumzia makazi wanayoishi, askari hao wanasema nyumba hizo zipo katika mazingira machafu, chakavu na hivyo kutokuwa na hadhi ya kuishi binadamu.
“Nyumba zile licha ya kuwa hazina hadhi ya kuishi binadamu kutokana na uchakavu wake, pia zimebana, mtu ana mke na watoto wawili, wanalazimishwa kulala chumba kimoja.
Hapo  kitakachotokea ni nini zaidi ya askari kutafuta njia za mkato za kupata fedha ili ajinasue na hali hiyo?” anahoji askari huyo.
Askari mwingine wa usalama barabarani anasema wapo baadhi ya askari wa vyeo vya juu wanawapangia kiasi cha fedha cha kuwapelekea na kwamba kama aliyetumwa asipofanya hivyo  anaweza kuondolewa katika nafasi hiyo.
“Haya mambo yapo, tunapangiwa kiwango cha kuwapelekea wakubwa, inapotokea hujapeleka unahesabiwa kuwa umeshindwa kazi…,” anasema askari huyo bila kutaja kiwango wanachowapelekea wakubwa wao.
Maisha ya askari polisi kazini
Kilimanjaro

Katika mkoa huo polisi waliozungumza na gazeti hili wanasema tangu mwaka 2009 wanadai fedha zao za likizo, posho za safari na fedha za uhamisho, hadi sasa wanazungushwa bila maelezo.
“Binafsi nadai fedha za uhamisho tangu 2009, wapo wenzangu wanaambiwa wawafuate watuhumiwa mikoani lakini hawalipwi posho za safari inavyostahili,” anasema mmoja wa polisi hao.
Polisi mwingine anasema haamini kama Serikali haitengi fedha kwa ajili ya malipo hayo kila mwaka na kumuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kulitolea ufafanuzi suala hilo.
“Kuna mambo mengi sana yanatukwaza wewe unapewa lita 10 kwa siku uzunguke kila mahali na hazitoshi inabidi wakati mwingine tugeuke ombaomba…,baadhi ya vituo vya mafuta wametuchoka,”anadai.
Mwingine aliyejitaka kwa jina moja la Masoud anasema,  “Hatupewi mafuta kabisa na wakati mwingine mwananchi akihitaji tukamkamate mtuhumiwa tunamuomba atoe fedha kwa ajili ya kuweka mafuta, hata gari likiharibika huwa ni jukumu letu kutengeneza.”
Baadhi ya polisi hao wamedai kuwa wakati polisi wadogo wakisotea malipo yao kwa muda mrefu, wakubwa wao malipo yao huwa hayacheleweshwi hali inayotoa picha ya kuwapo ubaguzi.
“Hii inachangia polisi kujiingiza kwenye vitendo ambavyo ni kinyume na mwenendo mwema wa jeshi la polisi kama rushwa na hata kumalizana na watuhumiwa bila kufika kituoni,”alidokeza polisi mmoja.
Geita na Mwanza
Katika mikoa hiyo baadhi ya askari polisi waliozungumza na gazeti hili wanasema ili wapangiwe zamu katika mgodi wa Geita ni lazima watoe kitu kidogo(fedha) kwa baadhi ya maofisa wa jeshi hilo, “Huwezi kupangwa kulinda mgodi wa Geita kama hujatoa kati ya Sh150,000 hadi Sh200,000, hii ni kwa vile wanaamini kuwa lindo hilo lina mshiko,” alieleza mmoja wa askari polisi aliyepo mkoani Geita.
Mwingine anasema polisi wanaofanya doria kwa kutumia pikipiki nao hali ni hivyo hivyo, ni lazima watoe fedha kwa maofisa wa ngazi ya juu kwa kuwa wanaamini kuwa kwa doria hilo wanapata fedha nyingi.
Anasema polisi wanaokabidhiwa pikipiki za doria wamekuwa wakielezwa kuwa lazima wazitumie kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kupata fedha za kujaza mafuta kwa maelezo kuwa jeshi hilo halina fedha za mafuta.
“Polisi wakipewa pikipiki wamekuwa wakitafuta mafuta kwa njia zao ikiwa ni pamoja na kukamata watu wenye makosa mbalimbali na huwa hawawaachii mpaka wafinye mkono (wawagawie kitu kidogo polisi), hivyo ni fedha hizo za rushwa barabarani ndizo wanazowekea mafuta kwenye vipando vyao,” anasema.
Aidha anasema polisi ambao wanaomba kuwekwa katika doria ya pikipiki wanapangiwa kiwango cha kutoa kwa wakubwa wao, lakini kiwango hicho kimekuwa ni siri baina yao na wakuu hao kwa hofu ya kuvuja kwa siri.
Kwa upande wa askari wa usalama barabarani, inaelezwa kuwa wao wamekuwa wakitumwa fedha za tozo la makosa mbalimbali ya usalama barabarani ambapo kwa kila anayepewa kitabu amekuwa akipangiwa kiwango cha kurejesha kwa wakuu wake kila wiki.
“Huku baadhi wamekuwa wakipangiwa viwango vya kurejesha, mfano kwa mwezi mnaweza kuambiwa kuwa mnatakiwa kuhakikisha mnaandika faini nyingi kwa ajili ya kutuma kwa wazee makao makuu,” anasema mmoja wa askari hao na anaongeza;
“Kinachofanyika ili kupata fedha hizo ni pamoja na kufanywa msako mkali wa magari mabovu na kutoza faini za papo hapo, fedha inayopatikana huwa inatengwa mara tatu ( ya askari wenyewe, wakubwa wao wa kazi katika vituo wanavyotokea na maofisa wa makao makuu).”
Mwananchi

No comments: