ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 23, 2025

MKUCHIKA ATANGAZA KUNG'ATUKA UBUNGE



Na Regina Ndumbaro - Newala.
Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini, Mheshimiwa George Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalum, ametangaza kutogombea tena ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Tangazo hilo amelitoa katika mkutano maalum wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika katika ukumbi wa Nawema, Newala Mjini.

Akizungumza katika mkutano huo, amesema kuwa amehudumu katika siasa na utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 50 na sasa ni wakati wa kuwaachia vijana waongoze. Mheshimiwa Mkuchika ameeleza kuwa safari yake ya uongozi ilianza baada ya kuhitimu Chuo Kikuu mwaka 1973.

Tangu mwaka 1983, alihudumu kama Mkuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali kabla ya kuteuliwa na Hayati Rais Benjamin Mkapa kuwa Mkuu wa Mkoa, nafasi aliyoitumikia kwa miaka minane.

Mwaka 2005, wananchi wa Newala walimsihi kuwania ubunge, na alikubali kuacha nafasi ya ukuu wa mkoa ili kuwatumikia wananchi wa Newala Mjini.

Katika kipindi chake cha miaka 20 kama mbunge, Mheshimiwa Mkuchika amefanikisha miradi mingi ya maendeleo katika jimbo hilo. Miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoyasimamia ni ujenzi wa barabara, vituo vya afya, na kuboresha upatikanaji wa maji.

Kabla ya juhudi zake, Newala Mjini ilikuwa na changamoto kubwa ya maji, lakini sasa tatizo hilo limebaki kuwa historia. Baadhi ya wananchi wa Newala wameonyesha hisia zao kuhusu uamuzi wa Mheshimiwa Mkuchika wa kutogombea tena.

Wamemshukuru kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jimbo hilo na wametoa rai kwa viongozi wa CCM kuhakikisha kuwa mgombea atakayeteuliwa ana sifa zinazofanana na za Mkuchika, ili kuhakikisha kuwa Newala inaendelea kupiga hatua za maendeleo.

Uamuzi wa Mheshimiwa Mkuchika unafungua milango kwa kizazi kipya cha viongozi wa CCM kuwania nafasi hiyo. Wakati wananchi wa Newala wakisubiri kujua ni nani atakayechukua nafasi yake, mchango wa Mkuchika utaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu kama kiongozi aliyejitolea kwa maendeleo ya jimbo hilo.

No comments: