
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ibula Ngonyani (kulia),akipokea cheti maalum baada ya kuibuka mshindi wa nafasi hiyo kwenye Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania kitengo cha Wanawake uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan.

Mjumbe wa kamati ya Utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Sabina Lipukila kushoto akikabidhi cheti kwa Mwalimu Amodzize Kinyamagoha baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya Ujumbe kwenye uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kitengo cha Wanawake.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu(CWT) Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kitengo cha Wanawake Deograsias Haule,akitangaza matokeo ya Uchaguzi huo ambapo Mwalimu Ibula Nyoni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitengo hicho katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan.
Na Regina Ndumbaro - Namtumbo.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, amewapongeza walimu wa wilaya hiyo kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Namtumbo, uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan, Malenya amesisitiza kuwa walimu wana mchango mkubwa sio tu katika elimu bali pia kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo shuleni.
Aidha, amewaonya walimu watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, akisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa wale watakaokwenda kinyume na maadili na taratibu za kazi.
Katika uchaguzi huo, Mwalimu Jacob Mbunda amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CWT Wilaya ya Namtumbo baada ya kupata kura 66, akimshinda aliyekuwa mwenyekiti wa zamani, Anna Mbawala, aliyepata kura 35.
Katika uchaguzi huo, Mwalimu Ibula Nyoni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Wanawake, huku Mwalimu Amodzize Kinyamagoha akiibuka mshindi wa nafasi ya ujumbe wa kitengo hicho.
Matokeo hayo yametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa CWT Wilaya ya Namtumbo, Deograsias Haule, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan.
Katibu wa CWT Wilaya ya Namtumbo, Deograsias Haule, ameeleza kuwa chama hicho kina wanachama 1,292, kati yao 1,265 wakiwa wanachama hai, sawa na asilimia 98.
Ameonyesha matarajio ya kufanikisha uandikishaji wa walimu wote kuwa wanachama.
Haule amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa tena kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu pamoja na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Pia, ameishukuru serikali kwa ushirikiano wake na CWT katika kutatua changamoto za walimu, ikiwemo kupandisha madaraja, kuboresha miundombinu ya shule na kuruhusu walimu kubadilishiwa muundo baada ya kujiendeleza.
Pamoja na mafanikio hayo, Haule amebainisha changamoto zinazowakabili walimu, ikiwa ni pamoja na kikokotoo cha mafao ambacho kinasababisha wastaafu kupokea malipo yasiyotosheleza mahitaji yao.
Changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za walimu, ambapo hata nyumba za kupanga ni chache, jambo linalowalazimu walimu kuishi mbali na maeneo yao ya kazi.
Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa CWT wamepewa vyeti maalum ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao.
Mwenyekiti mpya wa CWT Wilaya ya Namtumbo, Mwalimu Ibula Ngonyani, amepokea cheti maalum baada ya kuibuka mshindi wa nafasi hiyo.
Aidha, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya CWT, Sabina Lipukila, amemkabidhi cheti Mwalimu Amodzize Kinyamagoha kwa kushinda nafasi ya ujumbe wa kitengo cha wanawake.
No comments:
Post a Comment