Advertisements

Sunday, April 28, 2013

Malipo ya korosho Lindi yasitishwa

Liwale, Uongozi wa Serikali mkoani wa Lindi, umeviagiza vyama vya msingi mkoani humo, kusitisha malipo ya pili kwa wakulima wa korosho kufuatia kuibuka kwa ghasia za wakulima wanaopinga kulipwa malipo ya chini ya Sh 600.
Agizo hilo lilitolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulega, alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa zao la korosho wa wilayani Liwale.
Ulega alisema Serikali inaangalia njia mzuri ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika ulipaji wa malipo hayo.
Alisema zipo kasoro ambazo Serikali inazifanyia kazi hasa kuhusu namna mzuri ya kuwalipa wakulima na katika mfumo mzima wa stakabadhi ghalani.

Kaimu huyo Mkuu wa Mkoa, alisema Serikali pia imegundua kuwepo kwa makato ambayo si ya lazima kuwakata wakulima na hivyo kuwasababishia mzigo wakulima.
Baadhi ya wakulima waliozungumza katika kikao hicho waliiomba Serikali kuhakikisha kuwa wanalipwa kiasi chote wanachokidai badala ya kuwalipa kidogo kidogo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Wilaya ya Liwale, Mohamedi Mpoto, alisema aliishauri Serikali kuwalipa wakulima malipo ambayo iliwaahidi kwa sababu wana hali mbaya kifedha.
“Hali ya wakulima kwa sasa ni mbaya,hata palizi ya mikorosho hawajui watafanyaje na hii imechangiwa na tatizo hilo la malipo ya pili,”alisema Mpoto.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limempa uhamisho Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Liwale, Maurus Ngoromela ambaye anaamishiwa ofisi ya kamanda wa mkoa ambako atapangiwa kazi nyingine.
Hatua hiyo inafuatia kile kilichoelezwa kuwa ni kubaini kwa uzembe na kushindwa kudhibiti vurugu zilizojitokea wilayani humo. Katika vurugu hizo, nyumba kadhaa za viongozi wa vyama vya siasa akiwemo mbunge na viongozi wa vyama vya msingi, ziliharibiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, alisema mkuu huyo wa polisi wa wilaya hakuwajibika ipasavyo wakati wa vurugu hizo na kwamba matokeo yake ni madhara kwa watu.
Mwananchi

No comments: