ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 12, 2013

‘Migogoro ya ardhi nchini imekithiri’

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akizungumza na mwanasiasa mkongwe nchini, mzee Kingunge Ngombale- Mwiru kwenye Kongamano la Taaluma la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix

Dar es Salaam. Mwajiri yeyote atakayebainika kumcWaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amekiri kuwa Serikali imeelemewa na migogoro ya ardhi na ukosefu wa chakula.
Profesa Tibaijuka alifanya hivyo jana alipokuwa akichangia mjadala wa biashara katika chakula na ardhi katika Tamasha la Tano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, linaloendelea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwasilisha mada hiyo, Profesa Jayati Ghosh wa Chuo Kikuu cha Nehru cha Delhi India, alisema janga la ukosefu wa chakula duniani lilianza kushika kasi mwaka 2008 kutokana na mfumo wa biashara kuteka ardhi na chakula.
Akichangia mjadala huo, Profesa Tibaijuka alikiri kukithiri kwa migogoro ya ardhi na kukitaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , kufanya utafiti na kuja na mapendekezo ya kuitatua.
“Siyo kwamba Serikali ina jibu la kila kitu, mimi nilikuwa hapa chuoni na nawaomba watafiti wa hapa wafanye utafiti ili tutatue matatizo haya ya ardhi. Asilimia 70 ya ardhi ya Tanzania ni ya vijiji na Rais ndiyo mwenye mamlaka ya kutoa ardhi. Kisheria kuna ulinzi lakini kiuhalisia kuna changamoto nyingi,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza:
“Nakumbuka miaka ya 1990, Profesa Issa Shivji alifanya utafiti kuhusu migogoro ya ardhi na kuja na mapendekezo yaliyozaa ,sheria ya ardhi, hivyo tunahitaji tafiti zaidi.”
Hata hivyo, alisema pamoja na migogoro hiyo, bado Serikali iko makini kuitatua.
“Ni kweli tunayo ardhi lakini hatuna uwezo wa kuilima, kwa hiyo tunahitaji wawekezaji. Lakini Serikali iko makini mno na mikataba hasa ile mirefu. Hatuwezi kuwekeza kwenye ardhi bila kuwa na mitaji ndiyo maana tunahitaji wawekezaji wakubwa lakini tutahakikisha kuwa na mgawanyo sawa wa faida,” alisema.
Kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula nchini na kuvifanya viwebidhaa adimu, alisema kunachangiwa na teknolojia hafifu ya kuhifadhi chakula.
“Tatizo la ukosefu wa chakula na kilimo kwa ujumla lipo na linaanza na mavuno ya wakulima. Chakula siyo bidhaa kama zilivyo nyingine, kwa hiyo lazima Serikali iingilie kati,” alisemaProfesa Tibaijuka.
Profesa Ibrahim Lipumba alisema kupanda kwa bei za vyakula kumesababisha uporaji mkubwa wa ardhi barani Afrika unaowahusisha wawekezaji wa nchi zilizoendelea bila kuwahusisha wakulima wadogo.
“Uporaji huu wa ardhi unafanywa kwa makubaliano kati ya Serikali na wawekezaji wa nje, bila kuwahusisha wakulima wadogo na wenyeji wanaotegemea ardhi hiyo kwa maisha yao yote,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Samir Amin kutoka Misri ,alisema suluhisho la migogoro ya ardhi katika nchi za Afrika ni kuwa na mamlaka kamili ya ardhi hiyo.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Wawekezazi kwneye kilimo na ni kiasi gani tutapata? Kwenye madini hatupati kitu hata kodi hawalipi na ardhi yetu tuwape bure, tutabaki na nini? Sioni sababu ya wawekezaji kwenye ardhi yetu. Uzoefu unaonyesha kwamba uwekezeshaji haunufaishi wananchi zaidi ya muwekezeshaji na familia siyo zaidi ya kumi Tanzania.