ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 3, 2013

MWENJUMA MAGALU: TAMWA IMEREJESHA NDOTO ZANGU KIELIMU

Bibi Amina Mohamed mlezi wa familia ya mwanafunzi, Mwenjuma Magalu, akifanya mahojiano na mwanahabari Joachim Mushi, kijijini Msasa, wilayani Handeni.
Mwanafunzi, Mwenjuma Magalu.

Na Thehabari.com, Handeni
“BAADA ya kumaliza darasa la saba nilichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, lakini sikufanikiwa kuendelea na elimu hiyo kutokana na uwezo wa mzazi wangu mmoja (mama) ambaye alishindwa kumudu gharama zilizokuwa zikihitajika kwa wakati…,”ndivyo anavyoanza kusimulia Mwenjuma Magalu akizungumza Kijijini Msasa, Wilaya ya Handeni.
Magalu anasema furaha zote alizokuwa nazo mwaka 2011 baada ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, iliyopo kijijini Msasa Wilaya ya Handeni zilikuwa zikiyeyuka kadri siku zilivyokuwa zikikaribia kufunguliwa kwa shule za sekondari.

Anasema hadi shule zinafunguliwa mama yake alikuwa hajakamilisha vitu vilivyokuwa vikihitajika shuleni ikiwa ni pamoja na fedha ya ada ya kuanzia shule. Kijana huyo ambaye alikuwa akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake wawili walitelekezwa na babayao miaka kadhaa iliyopita kijijini hapo baada ya baba huyo kudai anakwenda kutafuta maisha nje ya kijiji chake.
Hata hivyo kwa kuonesha ana uchu na elimu kijana Magalu hakumuachia mamayake jukumu la kuitafuta ada peke yake, naye alifanya vibarua huku na kule kijijini Msasa kwa kuamini huenda angelipata kitu na kufanikiwa kuingia shuleni. Lakini ilishindikana kwake kutokana na uduni wa kipato kwa mamayake, kwani fedha ambayo mara nyingine Magalu aliipata kwenye vibarua ililazimika kununua chakula. Hii ilikuwa ni changamoto nyingine kwa familia ya kijana huyo mdogo.
Baada ya ndoto za kujiunga na shule kutoweka bila mafanikio, Magalu aliamua kufanya vibarua na kampuni ya Kichina iliyokuwa ikitengeneza barabara ipitayo karibu na kijijini chao. Magalu anasema ndoto yake ya shule ilikuja kurejeshwa na utafiti wa kihabari uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Machi 2012 kwa kushirikiana na waandishi wa habari.
“Baada ya kufanya mahojiano na mwandishi wa habari aliyekuja kijijini kwetu Msasa na kumweleza hali halisi, kilio change kilisikika kwawasamaria na kujitokeza kuisaidia familia yetu…kwa sasa nimepata ufadhili wa kusomeshwa hadi kidato cha nne,” anasema Magalu.
Mwenjuma Magalu ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo muda mfupi baada ya kupata ufadhili wa masomo akiwa bado na furaha alijikuta anaingia katika mtihani mwingine wa maisha baada ya mamayake mzazi kufariki dunia.
Hata hivyo baada ya utafiti wa kihabari kufanyika kijijini Msasa Wilaya ya Handeni na taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kwa kile mamayake (kwa sasa marehemu) kutokuwa na uwezo kuripotiwa, alijitokeza mfadhili wa kugharamia masomo yake ambaye hadi sasa anafanya hivyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi akiwa shuleni Komnyang’anyo, mwanafunzi huyo aliishukuru TAMWA kwa kuibua tatizo la familia yao kwa umma na kupatikana kwa mfadhili ambaye amemrudisha masomoni licha ya familia yao kutelekezwa.
Kwa upande wake bibi wa mtoto huyo (Amina Mohamed) ambaye aliachiwa familia hiyo baada ya kufariki kwa mwanaye, anamshukuru mfadhili wa mjukuu wake. “Binafsi nawashukuru sana hao (TAMWA) waliopaza sauti hadi mjuu wangu kurudi shuleni…hii kwetu ilikuwa ni ndoto kwetu maana mtoto mwenyewe alikuwa amekata tamaa kabisa kurudi shuleni na alikuwa kaanza kufanya vibarua mitaani huku wenzake wakiendelea na shule,” anasema bibi huyo.
Bibi huyo anafafanua kuwa kwa sasa bado familia hiyo inahitaji msaada wa huduma hasa baada ya mwanaye (mama wa familia hiyo) kufariki dunia mwaka jana na kumuachia watoto wake.
Anasema yeye ndiye aliyebaki kulea familia hiyo baada ya mtoto wake kufariki. Lakini kwa sasa hali ya afya yake si nzuri, licha ya uzee alionao amepimwa na kubainika ni mgonjwa wa TB ambapo ameanza kutumia dawa hivyo kwa hali yake ameshauriwa kupumzika.
Anasema baada ya kushauriwa na daktari kupumzika, mzigo wa malezi ya familia sasa umejikuta ukielekea kwa mjukuu wake Mwenjuma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo. Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa katika uchunguzi uliofanywa tena juzi na mwandishi wa makala haya bibi huyo anabainisha kuwa mjukuu wake anamzigo mkubwa.
“Nasema anamzigo mkubwa kwa kuwa sasa anatakiwa kutekeleza majukumu ya shule na nyumbani kama yeye ndiye mlezi wa familia…namuhurumia sana lakini sina cha kufanya. Anaporudi shuleni anatakiwa kutafuta chakula cha familia, yeye pia ndiye mpishi, mchota maji na ndiye mkulima,” anamzigo mzito kweli ndiyo maana wakati mwingine nalazimika kuingilia licha ya afya yangu.
Muhingo Rweyemamu ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, anasema tatizo la uduni wa maisha kwa familia katika wilaya hiyo lipo kwa kiasi kikubwa. Anabainisha kuwa kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni haina mfumo maalumu kwa ajili ya kusaidia moja kwa moja familia kama hizo.
Anasema kinachofanyika ni kuhamasisha ndugu, jamaa na marafiki kuendelea kutoa msaada kwa familia ambazo zimekuwa katika wakati mgumu kimaisha na kuitaji msaada. “Kwa ujumla tunatoa elimu ya kuhakikisha wazazi wanazaa watoto ambao wanaweza kuwamudu kimatunzo…wajua wakati mwingine umasikini katika familia hizi huchangiwa na wanaume kuzaa bila mpangilio, unakuta mwanaume anakuwa na familia zaidi ya moja wakati hana kipato cha kumudu familia hizo,” anasema Rweyemamu.
Anasema kwa kuwa hili limesha jitokeza wamejipanga kuziwezesha shule kufanya uzalishaji wa kilimo ili wanafunzi waanze kupata chochote wawapo shuleni, halmashauri imepata vocha takribani 300 ambazo zitasaidia upatikanaji wa pembejeo kwa shule zitakazokuwa zikizalisha mazao kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi kama chakula wawapo shuleni mchana.
Halmashauri pia imejipanga katika uhamasishaji kilimo kwa familia pamoja na uwezeshaji katika nyanja anuai ili kukabiliana na janga la njaa pamoja na ugumu wa maisha kiujumla.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA

No comments: