Viwango vipya vya nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani zimeanza kutumika jana, huku wananchi wakizipinga wakidai zinawaumiza zaidi kiuchumi.
Wakati baadhi wakilalamikia kupanda kwa nauli za dalala katika maeneo yao, baadhi ya wafanyakazi wa mabasi yaendayo mikoani wameendelea kutoza nauli ya zamani.
Dar es Salaam
Zoezi la kupandisha nauli nchini lililoanza jana limewagawanya wamiliki wa magari na kufanya baadhi ya safari za mikoani kupandisha nauli, huku nyingine zikiendelea kuwa kama zamani wakati nauli za daladala Dar es salaam zikipanda kama ilivyoagizwa.
Hatua hiyo ya kupandisha nauli ilizua tafrani baina ya makondakta na abiria waliokuwa wakisafiri katika safari mbalimbali ndani ya jiji, hususan wale waliokuwa hawajui kuwa jana ndiyo siku ambapo nauli zilitakiwa kupanda.
Mwananchi liliweka kambi katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendeyo mikoani cha Ubungo tangu saa 12 asubuhi na kushuhudia baadhi ya abiria wa safari za Arusha na Kilimanjaro wakibishia kiwango cha juu cha nauli kilichopanda, hali iliyowafanya baadhi ya abiria kutishia kususia safari.
Hata hivyo, walilazimika kulipia kiwango hicho cha ziada kutokana na umuhimu wa safari zao japo kwa majibizano na mawakala wa kukatisha tiketi waliopo kituoni hapo.
Kwa mujibu wa Ofisa wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Gervas Rutaguzinda safari za mikoani ambazo zilipandisha bei ya nauli ni Arusha, Moshi, Mwanza, Bukoba, Musoma na Kigoma huku nyingine zikiendelea kama zamani.
Alisema awali nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kwa basi la kawaida ilikuwa Sh18,900 lakini jana tiketi zilikuwa zikiuzwa kwa Sh22,700 ambapo kutokana na ugumu wa kupatikana chenji abiria walitakiwa kulipa Sh23000.
“Nimewapokea watu watano wa kwenda Mwanza na wawili wa safari ya Kigoma ambao walileta malalamiko kuwa walishindwa kusafiri kutokana na kukosa ongezeko la nauli walilokutana nalo” alisema Rutaguzinda.
Alisema baadhi ya wamiliki wa basi walibainisha kuwa watapandisha nauli ifikapo mwezi wa sita, lakini kwa sasa wataendelea na nauli zao za kawaida.
Naye wakala wa kukatisha tiketi kwa safari za Arusha na Moshi aliyejitambulisha kwa jina moja la Ipiana alisema ongezeko hilo limeathiri pato lao kwa kuwa katika nauli ya awali alikuwa akipata Sh2,000 kama kamisheni kwa kila tiketi, lakini kwa jana fedha zote zlitakiwa kupelekwa kwa mmliki wa basi.
Mmoja wa abiria aliyekuwa akienda Dodoma, Adriano Johnson pia ni raia wa kigeni kutoka Uingereza alisema, hakuona kama kuna mabadiliko ya nauli kwa kuwa alilipia Sh17,500 ambayo inafanana na ile aliyolipia mwaka mmoja uliopita alipokuja nchini.
Kivumbi ndani ya Daladala
Abiria waliokuwa wakisafiri katika sehemu mbalimbali za jiji walijikuta wakizozana na makondakta wa daladala kutokana na kulipa nauli ya zamani, jambo lililowachefua baadhi ya makondakta na kuwafanya watukane matusi ovyo.
“Nyie abiria wa wapi?, Hivi hamjasikia kwenye vyombo vya habari kuwa nauli zimepanda kuanzia leo (jana) au hamna redio mkulima majumbani mwenu, hakieleweki hapa lazima ulipe mia nne ndiyo ushuke,” alifoka kondakta mmoja wa daladala inayofanya safari zake kati ya Ubungo na Posta.
Asilimia kubwa ya abiria walionekana kulalamikia daladala kuendelea kubakia na maandishi yanayoendelea kuonyesha viwango vya nauli za zamani, huku makondakta wakidai nauli mpya jambo lililoleta usumbufu kwa baadhi ya wageni wanaoingia jijini.
Akizungumza jana na mwandishi wa gazeti hili, kondakta wa daladala lenye safari ya Mnazi mmoja na Ubungo, Abeid Juma alisema baada ya Serikali kuongeza faini, wamiliki wa daladala walifikia hatua ya kutoa malalamiko yao.
Aprili 4,mwaka huu,Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), ilitangaza nauli mpya za daladala katika jiji la Dar es Salaam, nauli hizo zitakazoanza kutumika rasmi leo zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 17.9 ambapo kiwango cha nauli kwa abiria kwa kila kilomita kimepanda kutoka Sh22.9 hadi Sh27.
Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray viwango hivyo vipya vimefikiwa baada ya kufuata taratibu za kisheria.
na za kiutendaji ambazo Sumatra kama msimamizi na mdhibiti wa sekta ya usafiri wa barabara inapaswa kuzifuata kabla ya kuridhia viwango hivyo.
“Mwanafunzi sasa atapaswa kulipa Sh150 na njia ya Kilometa kati ya 0 – 10 ( Mbagala – Posta) ni Sh300, wakati kilomita kati ya 0 - 15 (Kawe – Kariakoo) ni Sh 350 huku kilometa kati ya 0 – 20 (Kimara – Posta) ni Sh400, kuanzia Kilometa 0 – 25 (Tegeta – Kariakoo) ambapo ni Sh500 na kilometa kati ya 0 – 30 (Kibamba – Kariakoo) ni Sh650” ilisema.
Mwanza
Wananchi mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupunguza kodi ya mafuta ili kuwarahisishia uendeshaji watoa huduma za usafirishaji nchini.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti baada ya kupandishwa kwa kiwango cha nauli kutoka Sh 300 hadi 400, Ismail Katembo alisema kama serikali itapunguza kodi katika mafuta itasaidia pia ugumu wa maisha kwa wananchi.
Alisema wanaopata shida ni wananchi ambao wengi wao kipato chao kwa siku ni kidogo ukiongezea na makali ya ongezeko la nauli hali inazidi kuwa mbaya sana kwao.
Katembo alitolea mfano wa familia moja kuwa na watu wanne ambao lazima kwa siku wafike mjini ukipiga hesabu hapo ni zaidi ya kipato chake kwa siku.
“Maumivu zaidi atayapata mzazi ambaye ana watoto zaidi ya mmoja na wote wanasoma maeneo ambayo wanatakiwa kupanda gari kwa kweli hali ngumu,” alisema Katembo.
Dodoma
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida wadau wa usafirishaji wa abiria kwenda mikoani wameshindwa kuanza kutumia nauli mpya kutokana na kuchelewa kupata tangazo lenye viwango vipya vya nauli kutoka Sumatra.
Kwa upande wa wasafirishaji wa ndani hasa daladala, wameanza kutumia nauli hizo japo wamekutana na changamoto za hapa na pale kutoka kwa abiria.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa makarani wa kampuni ya mabasi ya kusafirishia abiria mikoani ya Champion, Yunus Omar alisema wameshindwa kutoza nauli mpya kwa sababu tangazo la nauli mpya walilipata jana asubuhi.
“Kwa upande wetu sisi bado hatujaanza kutumia nauli mpya, labda mpaka kwenye tarehe 18 kwa sababu hii biashara ya usafirishaji hapa Dodoma ni ngumu na wateja wetu ni wale wale,” alisema Omar.
Naye David Lusingo ambaye ni abiria alisema Serikali haijataja sababu za msingi za kupandisha nauli kwa sababu hakuna ongezeko lolote la gharama za usafirishaji kwa kuwa hakuna ongezeko lolote la bei za mafuta na vipuri vya magari.
Moshi
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wamelalamikia upandaji mpya wa nauli uliotangazwa na Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) usiozingatia umbali wa eneo na ubora wa magari.
Wakizungumza kwa nyakatoi tofauti huku wengine wakiamrisha madereva kuwashusha kwenye magari pindi walipotakiwa kulipa Sh 400, wasafirishaji hao walisema hawakatai kupanda kwa nauli, lakini Sumatra walipaswa kufanya ukaguzi wa magari kabla ya kutangaza viwango vipya vya nauli.
Abiria hao wa kutoka maeneo ya Soweto na Majengo walisema hakuna umbali wa kilometa 10 kutoka Soweto hadi katikati ya mji na kuwa kama wanataka kupandisha nauli kama maeneo mengine ni vyema wahudumu wa magari hayo wakawa wanayafanyia usafi na siyo kutembeza magari machafu na mabovu huku wakitaka nauli ya juu.
Mbeya
Baadhi ya wananchi mkoani Mbeya wamelalamikia uamuzi wa Serikali Sumatra kwa kupandisha nauli kwa vyombo vya usafiri bila kujua athari inayowakumba wanafunzi na wananchi wa kipato cha chini hususan vijijini.
Wakizungumza na gazeti hili katika baadhi ya maeneo jijini Mbeya, walisema kupanda kwa nauli kutaweza kusababisha mfumuko wa bei za mazao ya chakula katika masoko na kupelekea hali ya uchumi kuwa duni kwa familia zisizojiweza.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Laurent Stephen alisema serikali iliyo makini katika kuleta maendeleo isingeweza kufanya uamuzi bila kushirikisha wananchi wa vijijini na kwamba hali hiyo ni kuwakandamiza na kuwanyima haki zao za msingi, kwani kuna uwezekano mkubwa walioshirikishwa ni wadau na wananchi waishio mijini.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment