Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisaini mkataba wenye makubaliano hayo juzi Mjini Oslo Norway, akiiwakilisha Serikali ya Tanzania, na Serikali ya Norway iliwakilishwa na Waziri wake wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Heikki Holmas.
Zoezi la kusaini mkataba huo lilifanyika mwishoni mwa Mkutano wenye dhima isemayo ‘Nishati na Maendeleo Kuanzia 2015’ ambao Waziri Muhongo alishiriki.
Malengo ya mkutano yalikuwa ni kufanya majumuisho ya majadiliano mbalimbali kuhusu nishati ambayo yamekuwa yakifanyika ulimwenguni kote na katika mitandao, na pia kutoa mapendekezo kuhusu nafasi ya nishati katika maendeleo kuanzia mwaka 2015.
Akizungumzia msaada huo, Profesa Muhongo alisema “sasa tunao uhakika wa kumaliza miradi ya umeme kwenye Wilaya mpya 13, zoezi litakalogharimu takribani Sh. bilioni 70 za na pia kukamilisha miradi mingine ya umeme vijijini.”
Kwa upande wake, Waziri Holmas alisema “kuwapatia watu waishio vijijini huduma ya umeme ni sawa na kuwapatia Watanzania wengi uwezekano wa kuondokana na matumizi ya nishati zenye uharibifu kama mafuta ya taa na dizeli.” Alifafanua kuwa msaada huo unalenga kuleta usawa kwa vitendo, ambao utainua hali ya maisha haraka na kuleta njia mbadala za kujipatia kipato kwa wananchi wa vijijini.
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya msaada uliotolewa itatumika kuweka umeme kwa kuongeza miundombinu ya usambazaji wa umeme ambayo ndiyo namna nzuri ya kuyafikia maeneo ya vijijini kwa huduma husika.
Profesa Muhongo alisema Tanzania imedhamiria kuongeza huduma ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwa Watanzania kutoka asilimia 18.4 hadi 30 kwa ngazi ya taifa, na kutoka asilimia 6.5 hadi 15 kwa maeneo ya vijijini.
Baada ya Mkutano na makubaliano hayo, Waziri Muhongo ameendelea na safari yake katika Mji wa Brussels, Ujerumani akiendelea na zoezi la kutafuta fedha za miradi mbalimbali ya umeme.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment