ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 12, 2013

PSPF yakaribia kifo

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Ni mfuko wa wafanyakazi wa serikali
Shilingi trilioni 6.48 hazijulikani ziliko
Yakopesha Takukuru, Bodi ya Mikopo 67bn/- bure

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amewasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2012, ikionyesha hali mbaya kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali Kuu (PSPF) ukikadiriwa kuwa na hasara ya Sh. trilioni 6.487.Mbali na hali hiyo ya kutisha katika usimamizi na uendeshaji wa mfuko wa kutegemewa kwa watumishi wa umma watakaostaafu, ukaguzi wa CAG kwa ujumla umegundua matatizo makubwa katika kusimamia fedha za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Utouh alisema pamoja na serikali kuchukua hatua mbalimbali ambazo zimesaidia kupunguza baadhi ya kasoro katikausimamizi wa fedha za umma, lakini bado zinapotea.

Utouh alisema katika ukaguzi wa PSPF alibaini kwamba ukadiriaji thamani uliofanywa na Kampuni ya Uthaminishaji Genesis Actuarial Solution Limited na kutoa ripoti 2010, uliashiria kwamba uwezo wa kifedha wa PSPF uliendelea kushuka.

“Ukadiriaji thamani ulibaini hasara halisi ya Shilingi trilioni 6.487, hivyo Mfuko uko kwenye hatari ya kutoweza kujiendesha kama juhudi hazitachukuliwa na serikali,” alisema Utouh na kuongeza:

“Pamoja na mfuko kuwa katika hali mbaya kifedha, nilibaini kuwa mfuko ulitoa mikopo kwa mashirika ya umma na taasisi nyingine ambayo yamedhaminiwa na serikali yenye jumla ya Shilingi bilioni 67.2 bila riba.”

Taasisi za serikali ambazo zilinufaika na mkopo kutoka PSPF ni Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambayo bado inadaiwa Sh. 54,644,657,534; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo inadaiwa Sh. 6,678,150,000; Tan Power Resources inayodaiwa Sh. 5,421,551,370 pamoja na taasisi isiyo ya kiserikali ambacho ni Kiwanda cha Madawa Tanzania kinachodaiwa Sh. 435,057,632.

MABILIONI KWENYE H/SHAURI YALIPWA KINYEMELA
Aidha, alisema halmashauri 22 kati ya 134 zilifanya malipo yenye jumla ya Sh. 1,509,529,810 ambayo hayakuwa na hati za malipo wakati malipo yenye hati pungufu yalibainika katika halmashauri 74 yenye jumla ya Sh. 3,367,208,321.

Aidha, alisema vitabu 2,990 vya stakabadhi za mapato kutoka halmashauri 36 havikutolewa kwa ajili ya ukaguzi na kwamba ulegevu katika udhibiti wa ndani wa halmashauri 30 ulisababisha jumla ya Sh. 8,008,669,844 kutoka kwa wadaiwa wa kodi mbalimbali za vyanzo vya ndani vya mapato kutokusanywa kama kodi ya huduma, ushuru wa mazao na ushuru wa hoteli.

Pia halmashauri 56 zilikuwa na jumla ya Sh. 4,466,028,478 zikiwa ni mapato yaliyokusanywa na mawakala, lakini yalikuwa hayajawasilishwa kwenye halmashauri. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa halmashauri 17 hazikukusanya kodi ya majengo kiasi cha Sh. 4,345,570,497 sawa na asilimia 38 ya makisio.

Jumla ya Sh. 650,356,980 katika halmashauri 20 zililipwa kwa taasisi mbalimbali na katika ngazi za vijiji, lakini fedha hizo hazikuthibitika kupokelewa kutokana na kukosekana kwa stakabadhi za mapokezi.

MISHAHARA HEWA
Ukaguzi wa CAG ulibaini kuwa Sh. 693,132,772 zililipwa katika halmashauri 24 kama mishahara kwa wastaafu, watoro, watumishi waliofariki, watumishi walioacha kazi au walioachishwa kazi kupitia akaunti zao za benki.

Vile vile kutokana na kuwapo na kiwango cha chini cha uzingatiaji wa taratibu na Sheria ya Manunuzi, manunuzi yenye thamani ya Sh. 443,107,149 yalifanyika katika halmashauri 25 kutoka kwa wauzaji wa bidhaa na huduma bila ushindani wa bei huku ununuzi wa bidhaa na huduma wa thamani ya Sh. 541,013,405 ukifanyika katika halmashauri 24 bila kibali cha Bodi ya Zabuni.

Alisema mapato ya Sh bilioni 3.9 yalipotea hatika Halmashauri ya Arusha kutokana na halmashauri kutoza bei ya chini ambayo ilikuwa na tofauti kubwa kulinganisha na bei ya soko na kukusanya kodi za vyumba na vibanda walivyopangisha ambavyo vinamilikiwa na halmashauri. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hati za malipo ya Sh. 4,996,685 na viambatanisho vyenye jumla ya Sh. 1,075,263,998 havikuwasilishwa wakati wa ukaguzi.

Pamoja na mapungufu katika usimamizi wa fedha, Utouh alisema pia kuwa changamoto katika utekelezaji wa bajeti na kutoa mfano kwamba Bunge lilipitisha Sh. 595,064,422,505 za maendeleo katika halmashauri 113, lakini ni Sh. 345,568,067,477 tu ndizo zilizopokelewa na halmashauri husika na kufanya kuwapo upungufu wa Sh. 249,498,355,027 ambayo ni asilimia 42.

Kwa mujibu wa Utouh, jumla ya Sh. 2,561,882,820, zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo, hazikutumika katika halmashauri 29 kutokana na fedha hizo kutokupelekwa kwa wakati.

Hata hivyo, alisema licha ya kuwapo kwa mapungufu, hatua ambazo zimeanza kutelekezwa na serikali zimewafanya watumishi wengi katika halmashauri kuogopa kujihusisha katika vitendo vya ubadhirifu.

UJANGILI TISHIO
Ukaguzi wa CAG ulibaini kuongezeka kwa matukio ya uwindaji haramu katika Hifadhi za Taifa (Tanapa). Utouh alisema katika kupitia ripoti za robo mwaka za idara za ulinzi za Tanapa ilibainika kuwa vitendo vya uwindaji haramu hususani tembo vimeongezeka.

Alisema taarifa kutoka mbuga saba zinaonyesha kuwa tembo 110 waliuawa mwaka 2011/12 na kuongeza kuwa hali hiyo ina athari kubwa katika juhudi za serikali za kuendesha utalii na hatimaye kuathiri pato la taifa.

MKATABA WA TBC, SMT
Utouh alisema kuwa ukaguzi wake ulibaini kwamba mwaka 2010 Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) lililipa Sh. milioni 618.3 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa niaba ya Kampuni ya Star Media (SMT) kwa ajili ya leseni ya biashara.

Alisema ukaguzi pia ulibaini kwamba kampuni hiyo ina mkataba wa utendaji uliosainiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) huku SMT ikiwa imepewa msamaha wa kulipa leseni ya biashara kwa kipindi cha miaka kumi. “Kiasi hicho cha fedha kilicholipwa na TBC kingeweza kuwa ni sehemu ya hisa za shirika kwa SMT kama kusingekuwapo na msamaha wa leseni ya biashara. Malipo haya yaliyolipwa kimakosa na TBC hayajarejeshwa na TCRA,” alisema.

CAG KUKAGUA MISAMAHA YA KODI
Katika hatua nyingine, kuanzia mwaka ujao wa fedha, CAG ataanza kukagua misamaha ya kodi kwa lengo la kuangalia manufaa yake.

Utouh alisema anao uwezo huo kisheria na kwamba ofisi yake imejipanga kuitekeleza.
“Kwa kuwa fedha ambazo zingelipwa kutokana na misamaha ya kodi ni fedha za serikali, ambazo zinatolewa kama ruzuku kwa wanaopewa misamaha hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameamua kukagua kwa kina misamaha yote ya kodi kuanzia mwaka wa 2013/2014 kwa madhumuni ya kuangalia manufaa ya misamaha hii kwa uchumi wa Taifa letu,” alisema Utouh.

MAPENDEKEZO YA CAG
Kutokana na kasoro zilizobainika, CAG ametoa mapendekezo mbalimbali kwa serikali kama njia ya mapato likiwamo la mikataba ya kuchimba madini kujadiliwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na ushauri kutolewa kwa waziri husika kabla ya kusainiwa.

Utouh anapendekeza hati za misamaha ya kodi ziwekwe bayana kwamba msamaha wa kodi ni wa muda gani, unaanza lini na kumalizika lini. Pia misamaha ya kodi iainishwe ikionyesha malengo yanayokusudiwa na kuwa na utaratibu wa serikali wa kusimamia utekelezaji wake.

Kwamba mikataba yote yenye vipengele vya misamaha ya kodi ipitiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya ushauri kabla ya kusainiwa na pande husika. Baada ya CAG kuwasilisha taarifa hiyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilisema misamaha ya kodi bado ni sugu na kwamba kuanzia Juni mwaka huu iwekwe wazi na ukaguzi utasaidia kuweka wazi ili aliyepewa ajulikane.

Ilisema kuwa deni la Taifa linazidi kuongezeka na kamati ilishatoa maelezo bungeni kutaka lifanyiwe ukaguzi, lakini serikali imeendelea kuwa kimya.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, ripoti ya CAG imebainisha kuwa bado kuna matatizo makubwa katika kusimamia rasilimali za nchi na kusema kuwa kwa kuanzia itamuita Waziri wa Nishati na Madini pamoja na wasaidizi wake kuwahoji kuhusiana na kitendo cha kutotoa taarifa za ukusanyaji wa maduhuli.

Nayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilieleza kuwa upungufu mkubwa wa watumishi katika halmashauri unafanywa makusudi na mtandao ulioko Tamisemi na halmashauri husika kwa lengo la kuhujumu fedha za halmashauri.

Kamati hiyo ilieleza kukerwa na uamuzi wa kuzuia ripoti ya CAG isijadiliwe bungeni kwamba lengo lake ni kutaka kuwalinda watumishi na viongozi wake kutokana na mwaka jana kuwang’oa mawaziri sita.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alisema wabunge hususani kamati za PAC na LAAC hawapaswi kulegeza kamba katika suala zima la uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
CHANZO: NIPASHE

No comments: