ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 22, 2013

RAIS TENGA ATOA MIPIRA YA DOLA 30,000

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa
mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai vya
kuendeleza vijana (academies).
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha
hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira
wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana
na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar
es Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa
vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali
popote.
“Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini
nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya
hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga
Amesema amesema mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa
kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli
anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.
Rais Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira
wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini
anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka
waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira.
Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004
ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa
wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.

“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni
hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni
moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama
watoto hawachezi.

“Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka
madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,”
amesema Rais Tenga.

Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja
kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa
ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25
(minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala.

Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa
shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani.

No comments: