Tuwachape Mawaziri, Wabunge, Maaskari na tumchape kila anayeenda kinyume!
Je viboko vitafaulisha kweli?
Wanasema viboko vitasaidia sana vijana wetu kushinda mitihani na kutokufeli hata kidogo kwa hiyo tuwachape sana.
Wizara ya Elimu badala ya kusambaza vitabu, vifaa vya maabara n.k. sasa isambaze viboko mashuleni.
Wafanya biashara wapewe tenda za kusafirisha “njiti” mashuleni kwa ajiri ya kuwachapa vijana wetu ili washinde mitihani yao.
Sijui kama utafiti umefanywa juu ya unjitishaji wanafunzi ili washinde mitihani au ni wale waliopata elimu kwenye mfumo wa kikoloni wa kuchapwa wanataka na watoto wao wachapwe ili wakione cha moto waliokipata wazazi wao kutoka kwa wakoloni na walimu wao waliofanya kazi kama wakoloni.
Nikiwa shule ya sekondari nililiichukia somo la Fizikia kwa sababu tatu ambazo ni; mwalimu wa somo hilo kufundisha huku akivuta sigara darasani, matusi kwa wanafunzi pamoja na kuchapa viboko vilivyopitiliza kwa wanafunzi waliokosea, niliamua kuacha somo hili kama njia ya kuzikimbia adha za mwalimu huyu.
Walimu waliochanganyikiwa kwa mishahara midogo, makazi duni na mazingira magumu ya kazi yanayotokana na upigaji kura wa wazazi wa wanafunzi wao na wanafunzi wenyewe ukiwaruhusu kupiga viboko kama njia ya ufaulishaji katika ugiligili (frustrations) hizo si watawatwanga vijana wetu mpaka watokwe damu?
Shule zinazofaulisha vizuri wanafunzi wao katika mataifa yaliyoendelea na hata shule binafsi hapa nchini kama Seminari, Academy nk, wanawachapa wanafunzi zaidi kuliko hizi za kata au wana vitabu vya kutosha, maabara nzuri, maktaba, madarasa bora huku wakiwapa walimu wao mazingira mazuri ya kazi?
Kuna jamaa yangu ni mwalimu wa kiingereza katika shule moja ya binafsi, huyu bwana mshahara wake ni mzuri na huduma nyingine za kibinadamu zimeboreshwa, ndivyo matokeo y a somo lake yanavyokuwa mazuri kila mwaka.
Kama viboko ni suluhisho, basi tuwachape wote sio watoto/wanafunzi tu. Tuwachape Mawaziri wanaoshindwa kutimiza majukumu yao, tuwachape Wabunge wanaosinzia Bungeni, tuwachape mafisadi, tuwachape wafanyakazi wanaochelewa kazini, tuwachape maaskari wanaokula rushwa, tuwachape akina mama wanaoshindwa kunyonyesha watoto wao, tuwachape wanaume/wanawake wanaotoka nje ya ndoa.
Tuwachape viongozi wa dini wanaowatongoza waumini wao kwa kutumia sadaka za Mungu, tuwachape makandarasi wabovu, tuwachape madereva wanaovunja sheria za usalama barabarni, tuwachape wanasiasa wanaoshindwa kutimiza ahadi zao, tumchape kila mtu.
Kwa nini viboko viwe kwa ajili ya wanafunzi/na watoto pekee na sio wengine wanaofeli kutimiza majukumu yao?
Tumchapee kila mtu halafu tusiwe na miudombinu mashuleni, vijana wetu watashinda kwa miujuza ya kiboko nakwambia.
No comments:
Post a Comment