Advertisements

Tuesday, April 16, 2013

Takukuru yakalia faili la Mhando


Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme(Tanesco)Wiliam Mhando 

Dar es Salaam.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kukalia faili la aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme(Tanesco)Wiliam Mhando na wenzake.
Kauli ya Takukuru imekuja siku moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh kuitaka Serikali kuwachukulia hatua Mhando na mkewe katika sakata la ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Msemaji wa Takukuru, Dorin Kapwani alisema faili la vigogo hao bado liko ofisini kwao baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eliezer Feleshi kulirudisha kutokana na upungufu wa kisheria uliojitokeza katika faili hilo, jambo ambao limewafanya waendelee na uchunguzi zaidi.
Kapwani alisema baada ya uchunguzi wa awali kukamilika, faili hilo lilipelekwa kwa DPP kwa ajili ya hatua zaidi ya kisheria,lilipofika huko lilirudishwa kutokana na upungufu uliojitokeza katika baadhi ya maeneo, jambo ambalo limewafanya mpaka sasa kuendelea kulishikilia faili hilo.
“Tuliwahi kulipeleka kwa DPP kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, lakini limerudishwa kutokana na upungufu uliopo katika baadhi ya maeneo, jambo ambalo limetufanya mpaka sasa tuendelee na uchunguzi kuhusu tuhuma hizo,”alisema Kapwani.
Aliongeza kwa sasa bado wanaendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma hizo, na kwamba ukikamilika wanaweza kulipeleka tena kwa DPP ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wengine wanaotuhumiwa katika sakata hilo ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Robert Shemhilu, Mhasibu Mkuu, Lusekelo Kasanga na Meneja Mwandamizi wa Idara ya ununuzi, Haruna Matembo.
Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kukiuka sheria ya ununuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005 katika kuingia mikataba ya zabuni.
Katika sakata hilo, CAG alitoa ripoti yenye mapendekezo ya kuitaka serikali kumchukulia hatua za kisheria pia Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology pamoja na watu walioingia katika biashara na Tanesco kinyume na sheria katika kutoa zabuni.
Mwananchi

No comments: