Advertisements

Tuesday, April 16, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 2

NI vizuri nianze kwa kukumbusha nukuu ya Dalai Lama, ambayo niliiandika wiki iliyopita, inayosema: “Upendo na huruma ni mambo ya lazima. Yakikosekana, ubinadamu hautakuwepo.” Ishi ukiwa na mtazamo kuwa maisha yako ya furaha na amani, yanategemea upendo unaopata.
Maisha ya kimapenzi ni kama kioo. Yaani ukiyachekea nayo yatakuchekea, ila ukiyanunia, nayo yatakukunjia sura. Hakuna njia mbadala ya kuyachekea mapenzi zaidi ya kuwekeza upendo pale ambapo unahitaji kupendwa. Ni kichekesho kwa mbaguzi, mwenye chuki kwa wenzake halafu eti anataka apendwe.
Kosa kubwa ambalo wengi wetu hulifanya ni kujenga matarajio. Kila mmoja wetu anataka afanyiwe mengi lakini yeye mwenyewe huwa hajiulizi ni kipi anachopaswa kufanya kwa lengo la kumridhisha mwenzake. Ni vizuri kujua kuwa kadiri wewe unavyotaraji kufanyiwa na mwenzako anatarajia umfanyie.
Katika mapenzi hutakiwi kuingia na sura bandia. Kila ‘aliyefeki’ uhusika wake kwenye uhusiano wa kimapenzi, aliishia kuharibikiwa. Hata kama una udhaifu wako, acha uonekane ili uwe huru muda wote. Vinginevyo, utajichimbia kwenye dunia ya mateso ya kujitakia.
Kukubali udhaifu wako uonekane, kunakupa sifa kwamba wewe ni mwelewa. Hilo ni jambo la muhimu kuliko kujionesha wewe ni mkamilifu, halafu baadaye yale uliyokuwa unayaficha yanaonekana, sasa inakuwa aibu kwako. Mtu bandia kila siku hufeli, mwenye uhalisi wake atazidi kwenda mbele.
Uhusiano wa kimapenzi siyo kitu rahisi. Huweka wazi kila kitu ambacho mtu anakifikiria ndani yake au anachokitarajia. Kwa kawaida, mtu anavyohusika kwenye mapenzi ndivyo ambavyo hutoa kielelezo cha namna anavyotaka maisha yake na mwenzi wake yawe.
Mapenzi yanakutaka uwe unatabasamu ili na yenyewe yatabasamu kwa ajili yako. Huwezi kuwa kwenye kipindi kibaya halafu ukayatendea haki mapenzi. Ukiwa na siku mbaya, watu wanaokuzunguka, hususan mwenzi wako atakugundua. Vivyo hivyo, ukiwa hauna furaha.
Ukiwa mtu wa kulia, yenyewe yatalia na wewe na hutayafurahi hata siku moja. Watu jasiri ambao huamini katika mapenzi yanayochanua, badala ya kulia, huangalia tatizo na kulipatia ufumbuzi ili aweze kucheka kisha mapenzi nayo yamchekee.
Hakuna anayeishi ndani ya chupa, wote tupo ndani ya dunia hii, kwa hiyo wakati mwingine hukumbwa na mawazo mabaya ambayo yanaweza kuchanganya kichwa. Siyo wewe tu, kila mmoja yupo hivyo. Jambo la kufanya ni kuishinda hali hiyo taratibu, bila kugeuka bughudha kwa mwenzi wako.
Tafsiri ya mapenzi kama kioo, ikupe picha kuwa ukiwa mtu wa ugomvi kwenye maisha yako ya kimapenzi, hivyo ndivyo utakavyoishi. Maisha ni kuchagua, ukiwekeza kwenye tabia ya kulaumulaumu, utajikuta wewe na mwenzi wako kila siku ni watu wa kulaumiana.
Endapo utaamua kujikubali kuanzia kwenye fikra zako. Ukasema “najiamini, nipo imara, nina huruma, amani” endapo mawazo hayo yataingia moja kwa moja kwenye ubongo wako, utajikuta hayohayo yanakutokea kwenye maisha yako ya kimapenzi. Jamii na mwenzi wako anakuchukulia hivyohivyo.
Kuna mambo 10, yatasaidia kujenga mtindo bora wa maisha yako ili mapenzi yawe yanatabasamu na wewe kila siku. Unachotakiwa kufanya ni kusoma kipengele kimoja baada ya kingine, utakapomaliza, utakuwa umefanikiwa kwa asilimia 100.

1. FANYA KILE UNACHOTAKA KUFANYA KWA AJILI YAKO
Kila mtu ana mahitaji binafsi. Hutakiwi kukwepesha mambo yako kwa lengo ama la kumfurahisha mwenzi wako au kudharau yako na kujali ya mwenzio. Hilo ni kosa sana, kwani naye anatakiwa atambue mahitaji yako muhimu na akuunge mkono katika kuhakikisha unafurahia mapenzi na maisha kwa jumla.
Pamoja na ukweli kwamba unapoanzisha uhusiano inakubidi baadhi ya vitu uviache ili kwenda sawa na mwenzi wako, ila hutakiwi kupuuza yale mahitaji ambayo kwako huona ni ya lazima. Endapo utakosea na kuthubutu kuyapuuza, utayafanya mapenzi yako kuwa na kasoro nyingi.

Itaendelea wiki ijayo...

Global Publishers

No comments: