Thursday, May 2, 2013

Azam washuhudia wapinzani wao wakitesa Morocco

Kocha wa Azam, Stewart Hall.
Kocha wa Azam, Stewart Hall aliongoza benchi lake la ufundi na viongozi wengine kadhaa wa timu hiyo kuwashuhudia wapinzani wao katika Kombe la Shikirisho, AS FAR Rabat wakishinda 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Morocco iliyochezwa mwishoni mwa wiki, ikiwa ni siku chache tu kabla hawajakumbana nao katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho keshokutwa.


Wengine waliokuwa na Hall kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdallah ambako Rabat walikuwa wakicheza dhidi ya Wydad Fez ni msaidizi wa kocha huyo, Kalimangonga Ongala huku viongozi wakiwa ni pamoja na katibu mkuu, Nassor Idrissa, meneja wao Patrick Kahemele na meneja msaidizi Jemadari Said.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu akiwa jijini Rabat jana, Afisa Habari wa Azam, Jaffer Iddi, alisema kuwa kocha Stewart na timu yake walishuhudia goli la Rabat likifungwa katika dakika ya mwisho ya mechi na El Mahdi Naghmi.

"Benchi la ufundi linaendelea kufuatilia kwa kina mbinu za wapinzani wetu (Rabat). Jana (juzi), Stewart na msaidizi wake (Kalimangonga) Ongala walikwenda kuwashuhudia wapinzani wetu wakicheza dhidi ya Wydad Fez katika mechi ya ligi kuu yao," alisema Iddi.

“Rabat walishinda 1-0... makocha wamewasoma na wanajua cha kufanya tutakapokutana nao Jumamosi," alisema Iddi, akiongeza kuwa ushindi walioupata Rabat umewafanya wafikishe pointi 53 baada ya kucheza mechi 25 na kuwakaribia zaidi vinara Raja Casablanca wenye pointi 56.

Hata hivyo, Rabat wana mechi moja mkononi ya ligi hiyo yenye timu 16 na hivyo wanaweza kuwafikia Raja kama wakishinda.

Afisa Habari huyo aliongeza kuwa maandalizi yao yanaendelea vizuri na kwamba wachezaji wote wana morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mechi hiyo ambayo wanahitaji ushindi au sare yoyote ya magoli ili kufuzu kwa hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Akieleza zaidi, Iddi alisema kuwa wana matuamaini makubwa ya kuitoa Rabat katika michuano hiyo kwa kuwa wachezaji wao wameshazoea mazingira ya Morocco, ambako uongozi wa klabu yao umelazimika kununua vifaa vya kujikinga na baridi ili kuhakikisha kwamba timu yao inapata matokeo mazuri na kusonga mbele.
CHANZO: NIPASHE

No comments: