Balozi Ramadhan Mwinyi Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa Mkutano wa Kudumu wa 12 wa Masuala ya Wazawa, katika mchango wake kuhusu mada ya utafiti uliofanywa kuhusu Ujasiri, Maarifa ya Jadi na Kujenga uwezo Jamii ya Wafugaji katika Afrika, Mwakilishi huyo ameeleza kwamba Jamhuri ya Muungano inajukumu la kuwaletea maendeleo wananchi wake wote na kwamba katika hakuna jamii itakayoachwa nyuma. Akasisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa na wadau wengine kushirikiana na Serikali kufanikisha azma hiyo lakini pia kuunga mkono hatua na maamuzi inayoyachukua kwa manufaa ya wananchi wake na taifa kwa ujumla. Nyuma ya Balozi ni Bi. Ellen Maduhu Afisa wa Ubalozi .
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kwamba inajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mipango yake ya maendeleo endelevu inamfikia kila mwananchi na kwamba hakuna jamii itakayo achwa nyuma.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imeitaka Jumuiya ya Kimataifa na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kufanikisha azma yake hiyo, lakini pia kutambua kuwa maamuzi mbalimbali inayoyachukua yanafanyika kwa nia njema.
Hayo yameelezwa na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alipokuwa akichangia majadiliano ya mada ya utafiti kuhusu Ujasiri, Maarifa ya Jadi na Kujenga Uwezo wa Jamii ya Wafugaji katika Afrika.
Mada hiyo ni sehemu ya mada kadhaa zikiwa zao afya, elimu, haki za binadamu, ujasiliamali, vijana mila na tamadu ambazo zimekuwa zikijadiliwa kwa nyakati tofauti katika Mkutano wa Kudumu wa 12 Kuhusu Masuala ya Wazawa. ( Forum on Indigenous Issues) Mkutano huu ambao ulianza mapema wiki hii unafanyika chini ya usimamizi wa Baraza la Uchumi na Maendeleo ya Jamii la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC).
Washiriki wa mkutano huu wapatao 2000 wanatoka katika Asasi zisizo za kiserikali wakiwamo wawakilishi kutoka baadhi ya taasisi za kifedha kama Banki ya Dunia, Banki ya Maendeleo ya Afrika na Banki ya Maendeleo ya Asia.
“Tunaendelea na jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba hakuna jamii inayoachwa nyuma kama ambavyo imeainishwa katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) na kutafsriwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mipango migineyo” akasisitiza Balozi Mwinyi.
Hata hivyo akasema licha ya jitihada hizo za serikali , bado kuna baadhi ya jamii chache ambazo zenyewe zimeamua kudumisha mila, tamaduni na maisha yao ya jadi .
Akasema jamii hizo ni zile ambazo hazifahamiki sana katika Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo kwa jamii ya wamasaai.
Akizungumzia masuala ya upatikanaji na ugawaji wa ardhi kwa wananchi zikiwamo jamii ambazo mfumo wa maisha yao unategemea zaidi ardhi na mali asili nyingine. Balozi Mwinyi amewaeleza washiriki wa mkutano huo wakiwamo washiriki kutoka Tanzania, kwamba serikali imejiwekea sheria na taratibu zinazosimamia ugawaji wa ardhi.
Akafafanua kwa kueleza kwamba kwa sheria na taratibu za Tanzania, Hati ya umiliki wa Ardhi katika ngazi ya kijiji hutolewa kwa wanajamii ambao wanaishi au wamekusanyika katika muundo wa kijiji ambao unatambuliwa rasmi.
“ Kwa mujibu wa sheria zetu, ni kijiji ndicho kinatambuliwa kisheria kama chombo huru kinachosimamia masuala ya ardhi ambapo cheti cha ardhi hutolewa kwaajili ya matumizi ya jamii nzima”. Akasema
Na kuongea “ Hata hivyo kuna baadhi ya maeneo hasa yale ya wawindaji ambapo kama idadi ya jamii ile haikukidhi matakwa ya kisheria ya kuwa na hadhi ya kijiji kutokana na uchache wao, bado kwa mfano, mwaka 2011, serikali ilitoa hati ya kumiliki ardhi kwa ya Wahdzabe ingawa walikosa sifa zinazotakiwa kisheria.
Akizungumza kuhusu Loliondo ambako Serikali imetangaza kutenga eneo la kiasi cha kilomita za mraba 2,500 za ardhi kwaajili ya makazi ya jamii ya wamasaai na ambao wengi wao hawakuwa na ardhi na hivyo kuwa katika mazingira magumu. Balozi amesisitiza kwamba uamuzi huo ulikuwa ni wa manufaa kwa jamii hiyo na taifa kwa ujumla
Akasema kuwa eneo lililotengwa ni kubwa kuliko nchi ya Luxeburg au mara nne ya eneo la nchi ya Singapore ambayo ina kilomita za mraba 624.
Akasema eneo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 Serikali imelitenga kwaajili ya hifadhi ya wanyama pori na mazalia yake ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili, utunzaji wa vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya uwepo wa wanyama na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu akafafanua Zaidi kwa kueleza kwamba, uamuzi huu wa Serikali wa kutenga ardhi kwaajili ya matumizi ya binadamu na mengine kwa hifadhi ya maliasili ni uamuzi halali na wala haukuanza sasa bali umekuwa ukitekelezwa katika maeneo mengi ya nchi tangu uhuru.
No comments:
Post a Comment