ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 22, 2013

JITAMBUE, KUWA KWENYE UHUSIANO THABITI!


KUNA watu wana tabia ya kulalamika sana kuhusu mapenzi. Utakuta mtu anajilaumu, anajikatisha tamaa, anajinyima furaha, hana tumaini tena, kisa mapenzi! Hiyo siyo sawa.
Ni makosa kuamini una kasoro na huwezi kupata mwenzi sahihi, huwezi kuingia kwenye ndoa na kujenga familia imara. Hiyo ni taswira mbaya ambayo unapaswa kuiondoa kichwani mwako.
Rafiki zangu, mnajua athari za hayo niliyoeleza hapo juu? Jibu ni rahisi sana, kuingia kwenye uhusiano usio thabiti ambao mwisho wake ni kuchezewa na kupoteza muda bure!
Mfano utakuta mtu anaingia kwenye uhusiano na mwenzi ambaye tayari ana mtu wake na anajua wazi hilo. Siyo sahihi. Unapoteza muda wako bure.

PATA MAARIFA
Katika hali ya kawaida unawezaje kumtaka mtu ambaye tayari unajua kuwa ana mtu wake? Busara hapo iko wapi? Ukijichunguza kwa makini lazima utagundua kwamba una tatizo.
Mtu ambaye tayari ana mpenzi wake, maana yake ni kwamba amefika; kitendo cha kumtongoza, kinaonesha ni kwa kiwango gani umejaa tamaa ambazo ndizo zinazokuongoza, maana kwa busara huwezi kumtaka mtu ambaye ana mpenzi wake.
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, kuna wengine wanaambiwa wazi kuwa wana watu wao, lakini ndiyo kwanza mtu anaendelea kulazimisha, tena akitoa ahadi kedekede ili ampate. Huo ni ujinga usio na maana.

JIFUNZE HILI
Kwa bahati mbaya, wanapokutana wote wa ‘hovyo’ wanajikuta wameingia kwenye mapenzi. Hebu jiulize wewe ambaye umeingilia penzi la mtu, akili yako inafanya kazi sawasawa kweli? Unawezaje kuingia kwa mtu ambaye tayari ana wake?
Kuna vitu kadhaa vya kujifunza hapa. Kwanza lazima utambue kuwa, huyo ambaye amekubali kuwa na wewe wakati huo huo ana mwingine, maana yake hana penzi la dhati. Si ajabu akiwa na wewe, akatafuta kuwa na mwingine pembeni yako!
Hekima iko wapi? Kuna tatizo gani kusubiri mwingine ambaye atakuwa wako peke yako? Tatizo wengi wanachukulia mapenzi kama maigizo tu. Hawaoni umuhimu wala thamani ya kupenda kwa penzi la kweli.
Lazima uwe na msimamo katika maisha yako. Siyo sifa kuwa na wapenzi wengi au kuingia kwenye uhusiano wa mwingine. Unadhani mwenzako anaumia kwa kiasi gani? Vipi kama na wewe ukija kuingiliwa na mtu mwingine?
Unahitaji kutulia na kuijua thamani yako, halafu kuacha tamaa ambazo hazina maana. Ni sifa njema kuwa na mwenzi wako peke yako bila kuchangia na mwingine. Hilo litawezekana kwako kama nawe utaacha tabia ya kuingia kwenye uhusiano wa wengine.

JITIBU TATIZO LAKO
Tabia hiyo ni tatizo. Kama unayo unatakiwa ujue kwamba ni tatizo na unatakiwa kuishughulikia mapema iwezekanavyo.
Mtu ambaye anaishi kwa kuongozwa na mapenzi ya kweli, hawezi kukubali kuwa na mtu ambaye ana mwezi wake.
Kwa hakika utakuwa bado unaishi katika dunia inayotawaliwa na mawazo ya ngono tu. Ni dunia ya giza. Wenzako siku hizi wanatafuta kuishi kwenye ulimwengu wa mapenzi ya kweli.
Ondoka kwenye hilo giza. Hayo mambo yalikuwa ya kizamani sana, siyo katika zama hizi tulizonazo. Rafiki yangu mpendwa, kuwa msomaji wa safu hii, maana yake wewe ni mwerevu na unajitambua sawasawa.
Kama ndivyo basi ni vyema ukachagua njia sahihi ya maisha yako ili uwe katika uhusiano ulio thabiti na wenye malengo ya mbali. Ni suala la kufikiri na kuamua.

KUWA MJANJA!
Hapa sasa ni kazi yako kuonesha kuwa kichwa chako kinafanya kazi vizuri. Kuwa na msimamo wa maisha yako. Jiamini wewe ni mwanamke mzuri, mwenye thamani kubwa, usikubali kudanganyika.
Utakuwa na faida gani kuwa na mtu ambaye mwisho wa siku hatakuoa? Atakusaidia nini? Fedha? Hizo zina mwisho wake. Unaweza kutafuta zako taratibu kwa misingi sahihi ili baadaye uweze kuingia kwenye ndoa yako.
Hizo fedha hutazipata milele, atakupatia katika kipindi hiki anachokutumia halafu baadaye atakuacha kwenye mataa. Ndiyo ukweli wenyewe. Kumbuka furaha ya ndoa ni ya kudumu.
Wewe mwanaume pia lazima ujitambue, wape wanawake thamani yao wanayostahili kwa kuamua kuwa na msimamo katika maisha yako. Haina maana kumng’ang’ania mtu ambaye tayari yupo kwenye uhusiano wake.
Kama kweli wewe huna mpenzi na una lengo la dhati, tulia muda ukifika, atakuja. Kama naye atakuwa na upweke kama wako, mnaweza kupanga kuanzisha familia bora.
Kuna mahali nimekuacha rafiki? Mada imeisha, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: