ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 31, 2013

KAMA UNATAKA FURAHA, FUATA MTINDO HUU WA MAISHA!-2

NAZUNGUMZIA juu ya kutengeneza amani na furaha katika uhusiano. Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza kuwa kuishi kirafiki na kusamehe na kusahau ni kati ya mambo ya msingi zaidi katika kusaka amani ya moyo.
Hebu sasa tuendelee.

TUPATE ELIMU KIDOGO
Hujawahi kusikia mtu amekuwa mlevi wa kupindukia kwa sababu ameachana au amegombana na mpenzi wake? Hujawahi kusikia mtu amejinyonga au amekunywa sumu kwa sababu ya matatizo ya aina hiyo?
Naamini una mifano mingi sana ya namna hiyo. Si ajabu umeshuhudia hata kwa mtu wako wa karibu kabisa. Kwa msingi huo rafiki zangu, inatupasa kutengeneza furaha na amani ya kudumu katika uhusiano.

HESHIMU HISIA ZA MWENZAKO
Ukitaka kujenga amani na kuepukana na migogoro, jenga tabia ya kuheshimu hisia za mwenzako. Mpe nafasi, msikilize. Kama kuna jambo halitaki na lina madhara achana nalo.
Kwa nini umuudhi mwenzako? Kama unaona lina manufaa basi ni vyema ukamweleza hoja zako kwanza, akiona zina mashiko, mtakuwa mmekubaliana kwa pamoja.
Ni vyema mkaacha kuishi kwa ubabe (hasa wanaume). Mpe nafasi mwanamke wako ajione naye ni kiungo muhimu katika uhusiano wenu.

KUWA MSHAURI ZAIDI
Si kila kitu kinahitaji kutumia nguvu nyingi kwa mpenzi wako. Kuwa mtu wa kushauri zaidi. Njia hii ni nzuri na imesaidia ndoa na uhusiano wa wapenzi wengi duniani.
Kama una tabia ya kufoka hovyo, acha maana haina maana na haijengi.

MARAFIKI NA WACHUMBA
Kabla ya ndoa ni vizuri kuchunguzana vya kutosha. Kama unaona mpenzi wako ana matatizo ambayo umemrekebisha mara nyingi na anarudi ujue ni vigumu kubadilika.
Ndoa haimbadilishi mtu ila anakwenda kuonesha kwa vitendo yale ambayo yalikuwa yakitokea kwenye kipindi cha urafiki na uchumba.
Kabla ya ndoa jihakikishie kuwa mwenzako ni yule aliye sahihi na atakufanya uishi kwa amani na ufurahie ndoa yenu. Ni bora uahirishe ndoa kama una mashaka kuliko kuingia ukakutana na mateso.



KWA WANANDOA
Maisha ni furaha ambayo hujengwa kwa ushirikiano. Kwa muunganiko wa ndoa, mnapaswa kuishi kirafiki zaidi na kila mmoja kuwa na nafasi katika mambo yote hasa ya maendeleo.
Jambo lingine muhimu kwenye ndoa ni kufurahisha kwenye mapenzi. Msome mwenzako, unapokuwa naye faragha, jua kwamba wewe una kazi ya kumfurahisha. Acha kujifikiria mwenyewe.
Kumbuka, kumuacha mwenzako na kiu unamsogeza kwenye ushawishi wa usaliti. Kuwa makini rafiki yangu. Ahsanteni, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayendikia Magazeti ya Global Publishers. Amendika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: