ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 30, 2013

Lissu awafunda wanawake CHADEMA

Na Elizabeth Joseph, Dodoma
WANAWAKE nchini wametakiwa kutobweteka na kuchangamkia fursa mbalimbali katika kuwania nafasi za uongozi ili kuingia kwa vitendo katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) uliofanyika mkoani humo.

Alisema kuwa wanawake katika chama hicho hawatakiwi kubweteka kwa lengo la kusubiri kupewa nafasi za upendeleo za uongozi na hivyo wanapaswa kuzigombania kama wanavyofanya wanaume.
Mafunzo hayo ambayo yanawashirikisha viongozi wa Bawacha kutoka katika kanda zote za chama hicho nchini, yamefadhiliwa na chama rafiki kutoka nchini Denmark. 

"Msisubiri kuwezeshwa kwani cha kupewa si kitamu na ni hatari kusema kuwa tukiwezeshwa tunaweza maana mtabaki kupewa na mtakuwa nyuma siku zote kwa wanaume".

"Hakikisheni wanawake wengi wanajitokeza katika shughuli za chama chetu hasa katika chaguzi" alisema Lissu.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Suzan Lyimo alisema kuwa miongoni mwa malengo ya mafunzo hayo ni pamoja na kuwawezesha wakufunzi wa kanda na kukiandaa chama kikanda kwa ajili ya chaguzi za serikali.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Tanzania Visiwani, Mariam Msabaha aliwataka wanawake kutoogopa kugombania nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuhofia kuwa nafasi hizo zimeshikiliwa na wenzao.

Pia aliwataka viongozi wanawake kutokuwa na choyo pindi watakapoona wanawake wenzao wanagombea nafasi zinazojitokeza.

No comments: