Saturday, May 18, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-6

Nikifunga mfano wa Raja na Jane kama mfano ambao niliutoa wiki iliyopita ni kwamba wote wawili wana kasoro. Sasa ni vizuri wakati unasoma, ukaelewa hilo ili nawe utakapokuwa unapitia vipindi kama hivyo walivyopita wenzetu, ukajua namna ya kuchanganua mambo.

Kasoro ya Jane ilikuwa tatizo la kuwa na ulimi usio na breki. Alipaswa kuisoma akili ya mwenzake kwamba hatafurahia maneno ya ovyo ambayo alikuwa anayatamka kisha angejidhibiti. Kikubwa ni kuwa na kanuni kwamba maneno ambayo hupendi kuyasikia kutoka kwa mwenzi wako, basi usiyaseme kwake.
Vilevile, kasoro ya Raja ni kulimbikiza mambo. Alipaswa kushughulikia kila jambo kwa wakati wake. Mfano; siku Jane alipojieleza kuwa yeye alikuwa ni mzinzi, alitakiwa ‘kudili’ naye palepale, vivyo hivyo, suala la kutoa mimba lilipojitokeza, ilitakiwa lipatiwe tiba kwa wakati wake.
Tatizo la Raja ni kuhifadhi vitu viwili vinavyomtesa, akaishi navyo. Baada ya kuongeza na kitu cha tatu, akapandwa na jazba, mwisho wakagombana wodini na kuachana kwa taadhira. Kama ulimi ungedhibitiwa, mgogoro usingefika pale ulipofikia.
Zingatia mfano wa Raja na Jane kila siku za maisha yako. Mwenzi wako ni taa ya maisha yako, kwa hiyo kile ambacho unakizungumza naye, hakikisha hakitakuja kuleta madhara baadaye. Epuka vimisemo vya kuudhi ambavyo vinaweza kumpeleka kwenye hali ya kuwaza.
Unaweza kutamka leo na asikuulize lakini likaishi ndani ya kichwa chake. Bahati mbaya zaidi ni kuwa anaweza kujaza mambo mengi na siku atakayokuuliza, hatakuwa kwenye hali ya kawaida, kwa maana atakuwa anasumbuliwa na hisia za kuchoshwa na manenomaneno yako.
Ulimi ni kaburi katika uhusiano wako kwa sababu ya tafsiri pana. Inawezekana usimuudhi kwa namna unavyomsimulia stori ya kuudhi kuhusu maisha yako ya kimapenzi, ukawa na tatizo la majibu. Jinsi unavyomjibu, utamfanya akutafsiri kutokana na uhusika wako.
Ukiwa na majibu mazuri, atakuona mzuri na utazidisha mapenzi ndani yake. Ukiwa msema ovyo, haitapita siku nyingi, wewe na yeye mtakuwa mmeshaachana. Elewa ukweli kuwa maudhi hupunguza mapenzi, ulimi wako unapomsababishia maudhi, kiwango chake cha kukupenda hushuka na hatimaye huisha kabisa.
Siyo kusema ovyo mbele yake tu, inawezekana huzungumzi kwa heshima mbele ya marafiki, ndugu zake pengine hata kwa wazazi wake. Maneno yako yachunge sana, maana kuna siku atayatumia kukuhukumu. Hebu jichunge na usikubali ulimi wako ukuingize katika kaburi la mapenzi yako mwenyewe.
Kwa Raja na Jane, umeona namna ambavyo ulimi unavunja uhusiano, upande mwingine hasa unapotumika barabara, unaweza kuyafanya mapenzi yanayolegalega, yawe imara. Unaweza kumfanya mtu ajenge matarajio chanya hadi ndoa kwa yule aliyekuwa hamuwazii, anampuuza.
Itaendelea wiki ijayo.
Mfano; Kuna msomaji wangu anayeitwa Romeo, aliwahi kunisimulia stori yake ambayo nimeona itapendeza sana kama nawe nitakuhadithia japo kwa ufupi. Lengo langu ni kukuonesha namna ambavyo ulimi unavyoweza kusimama kama nyenzo imanara ya ujenzi wa uhusiano, kama utautumia ipasavyo.
Romeo alinisimulia: “Huko nyuma niliwahi kuteswa na mapenzi, ingawa baadaye nikagundua nilikuwa najitesa mwenyewe. Nilijikuta nina wapenzi wawili lakini huwa sijilaumu kwa maana hiyo ilinisaidia kumtambua mpenzi wa kweli ambaye leo hii ndiye mke wangu wa ndoa na tuna watoto wawili.
“Mke wangu anaitwa Shantale, awali sikuamini kama ni mwanamke anayenifaa. Mwanamke ambaye niliwaza kwamba angekuwa wangu wa ndoa anaitwa Jannine. Nilimpenda sana na nikawa nampa kipaumbele kuliko Shantale ambaye kipindi chote alionesha utulivu na uvumilivu mkubwa.
“Niliponunua zawadi, moja kwa moja nilimpelekea Jannine. Shantale nilimuwazia tu kama mwanamke wa kupita. Niliona hawezi kukidhi matarajio yangu. Niliendelea kumbagua, wakati mwingine alinipigia simu sikupokea na SMS zake sikujibu. Siku tukikutana, aliniuliza maswali machache tena kwa upole na nilichomweleza alikielewa.
“Siku nyingine nilikuwa mkali sana kwake. Aliponipigia simu nilipokea na kumjibu kwa ukali. Kuna siku nilikuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa, kwa upendo kabisa, alininunulia shati, suriali, viatu, vilevile akanitengenezea keki nzuri sana, yote hiyo kuonesha namna anavyonijali.
“Basi nilimfanyia kitu kibaya sana, siku nzima nilimzimia simu, nikamchukua Jannine tukaenda hotelini na kufurahi pamoja siku nzima. Jannine pamoja na kutumia muda wangu wote nikiwa naye lakini hakuninunulia zawadi yoyote kunipongeza. Hata maneno happy birthday hakuniambia.
“Asubuhi nilitokea hotelini nikaenda kazini na Jannine naye alielekeza ofisini kwake. Jioni niliporudi nyumbani, nilikuwa zawadi zangu. Keki, nguo, viatu, ua pamoja na kadi nzuri kutoka kwa Shantale. Hiyo kidogo ikanifanya niwaze sana kuhusu upendo wa mwanamke huyo.
“Kipindi hicho Shantale hakuwa na kazi, ndiyo alikuwa amemaliza shahada yake ya chuo, akiwa anaendelea kutafuta ajira. Pamoja na kutokuwa na kazi aliweza kunifanyia mambo hayo. Kwa namna fulani ilinipa mwanga kwamba mwanamke huyo ananipenda sana.
“Jannine ana kazi lakini hakuonesha kujali chochote. Hata kunitamkia maneno ya kunitakia heri ya siku yangu ya kuzaliwa alishindwa. Hakunijali kwa zawadi na nilipomwambia habari ya kwenda kufurahia hotelini, alilipokea kwa moyo mmoja. Hapo nikaanza kuhisi kasoro ya upendo wa Jannine.
“Kingine ambacho kilinifanya niwaze sana ni kwamba miezi miwili kabla ya siku yangu ya kuzaliwa, ilikuwa siku ya kuzaliwa Jannine, nilimnunulia viatu vyenye thamani kubwa, cheni ya dhahabu, mkoba, gauni zuri sana la kuvaa ofisini na hata mitoko ya jioni, vilevile sikuacha kadi na ua.
“Miezi mitano nyuma, ilikuwa ni siku ya kuzaliwa ya Shantale lakini sikumfanyia chochote. Nakumbuka siku mbili kabla ainijulisha na asubuhi ya siku husika, alinikumbusha. Ikabidi nimtakie heri ya siku ya kuzaliwa kwa kumridhisha tu, maana haikutoka moyoni. Hata hivyo, mwenyewe alipokea na kushukuru sana.
“Mambo hayo mawili yakanifanya niwaze sana. Nikakumbuka kipindi nasoma chuo, Shantale alikuwa radhi agawe fedha anazotumiwa na wazazi wake kwa ajili ya matumizi ya chuo ili anipe na mimi niweze kupunguza makali ya maisha. Alionesha upendo mkubwa sana na hakujali.
“Nilipoanza maisha, wakati napanga, mimi niliweza kununua sofa za sebuleni, maana ilikuwa chumba na sebule, kule chumbani nilinunua godoro tu. Nguo niliweka kwenye begi moja kubwa na zile chafu niliweka kwenye kapu, nyingine nilitundika kwenye misumari ukutani. Nilifanya hivyo kwanza nikiwa na matarajio kwamba baada ya muda ningerekebisha na kununua kitanda na kabati kwa vile sikuwa na pesa.
“Shantale alipogundua hivyo, aliamua kuchukua akiba yake yote na kunifanyia mambo makubwa sana. Nikiwa kazini, huku nyuma aliingiza kitanda, kabati na seti nzuri ya muziki. Niliporudi nyumbani nilishangazwa na kila nilichokiona. Nilimshukuru lakini sikuona kama amenifanyia kitu kikubwa sana kwa wakati huo.
“Ujana ulinifanya nione alichokifanya Shantale ni kawaida kwa sababu alikuwa anabembeleza mapenzi. Nikaendelea kumchukulia wa kawaida mpaka baadaye nikampata Jannine ambaye aliniteka akili. Nikampenda kwelikweli. Alichotaka nifanye nilitekeleza, wakati mwingine ilikuwa juu ya uwezo wangu.
“Mwanzoni nilikuwa mnyenyekevu sana kwa Jannine, ila siku zilipozidi kwenda mbele, nilijikuta napunguza mapenzi, maana kuna mambo mengine nilihisi ananifanyia makusudi kwa sababu anajua nampenda. Kikubwa ni kauli zake, alikuwa ana matamshi ya dharau sana.
“Kipindi kingine alinifokea bila sababu. Usiku mmoja nikawaza matukio ya manyanyaso anayonifanyia Jannine, nikaona kuna sababu ya kuufikiria upya uhusiano wetu kama unaweza kuwa mzuri baadaye kwa tabia ambazo Jannine alikuwa ananionesha. Kuna siku aliniomba pesa, nilipomwambia sina, ilikuwa ugomvi, akaniuliza kwa dharau, eti mimi ni mwanaume gani sina fedha?
“Hayakuwa hayo tu, Jannine alikuwa na kauli chafu hata mbele ya rafiki zangu. Aliniamrisha au kunitamkia maneno ya kunivunjia heshima mara nyingi sana tena mbele za watu. Hata akiwa na marafiki zake, hakutaka kuonesha umuhimu wangu na kunyenyekea, alitaka nionekane kibaraka wake.
“Usiku huo, nikamuwaza sana Shantale, ni mwanamke mrembo lakini simthamini. Kipindi chote nikiwa nusu mwehu kwa sababu ya mapenzi ya Jannine, sikumhesabu kama mpenzi wangu, isipokuwa nilikuwa nashindwa jinsi ya kumtamkia tuachane kutokana na mambo aliyonifanyia.
“Kuna siku nilimwambia tuachane, alilia sana. Alituma SMS kila siku kubembeleza turudiane, baadaye akaniambia endapo nitashindwa kumwelewa ombi lake, nitasababisha afeli chuo, kwa maana alikuwa hawezi kufanya kitu chochote tangu nilipomwambia tuachane.
“Kwa maana hiyo, nilikuwa Shantale kama mwanamke wa kwenye kapu, sikumjali kabisa, marafiki na wafanyakazi wenzangu walimjua Jannine peke yake. Ndugu zangu, hususan dada zangu waliwajua wote na siku zote waliniambia mwanamke mzuri ni Shantale na kwamba Jannine hanifai, kwani si mjenzi wa familia, bali ni mwanamke mwenye dharau, maringo na kauli chafu.
“Nilipomuwaza sana Shantale nikakumbuka ukarimu na wema wake kwangu. Hata siku moja hajawahi kuninyanyasa. Alinisaidia nikiwa na shida, tena hakunisimanga. Nilipomwambia tuachane, hakusema vitu alivyoninunulia nimrudishie, alinibembeleza tu nisimuache kwa sababu ananipenda sana.
“Nilichanganua kwa marefu na mapana, mwisho nikagundua kwamba Shantale ni mwanamke mwenye thamani kubwa lakini namnyanyasa. Nilimuona ni almasi iliyochanganywa na chupa, kwa hiyo si rahisi kuitambua na kujua thamani yake. Kikubwa kilichonivutia kwake ni kauli, Shantale ana kauli nzuri sana.
“Kikubwa kilichonikimbiza kwa Jannine ni kauli, maana mdomo wake ni mchafu mno. Asubuhi palipopambazuka, nilimtumia SMS Jannine, nikamwomba tuonane, kwanza alichelewa kunijibu, baadaye akaniambia ataangalia ratiba zake kama itawezekana.
“Alizidi kunifanya nimuone hanifai baada ya mimi kumuuliza kama ana ratiba gani tofauti na za kawaida akitoka kazini, akasema alikuwa amepanga kukutana na marafiki zake waende ufukweni. Akanisisitizia ni mtoko wa yeye na wanawake wenzake na ni muhimu kwake.
“Nikamtumia SMS Shantale kuomba kuonana naye, baada ya muda mfupi ilijibiwa kwamba yupo tayari, akaniuliza saa. Kwa mara ya kwanza nilimtoa ‘out’ Shantale, tukaenda kwenye hoteli yenye mandhari tulivu, nikamuomba msamaha kwa kujifanya kipofu siku zote hata nikaacha kuuona upendo wake.
“Nilipomuomba msamaha Shantale alilia, bila shaka hakuamini maneno yangu. Nikatoa pete ya uchumba nikamvalisha na nikamuomba anikubalie nianze taratibu za kumchumbia kihalali nyumbani kwao ili nimuoe kabisa. Ilikuwa siku nzuri sana kwetu, Shantale alikuwa mwenye furaha sana.
“Baada ya siku mbili, sikuona sababu ya kutaka kuonana na Jannine wakati mtu mwenyewe alikuwa haonekani kujali, nilimtumia SMS kumfahamisha kuhusu uamuzi wangu wa kusitisha uhusiano wetu, akanijibu maneno makali. Kwa kifupi alinitukana sana.
“Mimi na Shantale ukurasa ukufunguliwa upya, kuanzia hapo nikaanza kuuona ule uchangamfu wake wa siku za nyuma umerudi, maana kuna kipindi alikuwa mpole sana, tena mnyonge. Taratibu zote nilifuata, tukafunga ndoa, Mungu akatujalia kupata watoto wawili wazuri na maisha yetu ni mazuri sana, kwa maana tunaelewana, hatuna migogoro, tunasikilizana.
“Shantale ni mwanamke bora sana lakini kidogo nimpoteze. Angekuwa mapepe, asingekuwa na mimi leo. Ila uvumilivu wake umekuwa nafuu kwanza. Vilevile kwake, kwa maana sasa hivi nampa mapenzi ya kipekee sana, nikifidia nyakati ambazo nilimsaliti. Nasema asante Mungu kwa kunifanya mimi Romeo kuwa mume wa Shantale.”
Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: