Wednesday, May 29, 2013

MUDA WA USICHANA NI MFUPI, JIPANGE!

KUFAHAMU kitu kipya ni jambo muhimu sana katika maisha ya binadamu anaye-jitambua na mwenye kwenda na wakati. Kila siku unapaswa kutafuta kujua mambo mapya ili kukuza ufahamu wako.

Hata katika mapenzi ni hivyohivyo, kama ni kweli unahitaji uhusiano wako uwe bora basi ni vyema kutafuta elimu juu ya mapenzi kila siku. Hapa kwenye All About Love ndiyo mahali pake.

Kuna kitu wanawake wengi inaonekana kama hawakijui na hata kama wanakijua basi hawakipi kipaumbele; ni suala la usichana. Kipindi cha usichana kwa maana ya binti huwa ni kifupi sana lakini baadhi yao huwa wanadhani wataendelea kuwa wasichana kwa muda mrefu.

Kutokana na hilo, hujikuta wakitoka kwenye usichana na kuingia kwenye hatua nyingine ya umama ama kwa kutaka au bila kutaka na kujikuta wakibaki tu wanashangaa!

NGOJA NIFAFANUE
Lazima niweke sawa hapa kwanza kabla ya kuendelea na mada yetu ambayo naamini itaongeza kitu kipya. Maana yangu ni kwamba, msichana anapokuwa katika ‘udada’ anaweza kuamini labda ataendelea kuwa hivyo milele.
Fikra hizo humsahaulisha kabisa suala la kuingia kwenye ndoa na akija kushtuka tayari muda unakuwa umekwenda hivyo kushindwa kuingia kwenye ndoa – tayari amekuwa mama na si msichana tena.
Wanaume wengi huoa wasichana na si wamama ingawa wavulana wengi nao huoa wasichana na si wamama. Nadhani utakuwa umeona tofauti hapo. Yaani msichana anaweza kuolewa hata na baba mtu mzima lakini ni aghalabu sana kukuta mvulana mdogo kuoa mama mtu mzima.

MUDA MFUPI KIVIPI?
Rafiki zangu, ukweli ni kwamba kwa kipindi hiki umri wa msichana kuingia kwenye ndoa ni mfupi zaidi ya ilivyokuwa nyuma ingawa kwa zamani umri ulianzia mdogo lakini ulikwenda mbali zaidi.
Tafiti zinaonesha wazi kwamba wasichana wanaoingia kwenye ndoa kwa sasa ni kati ya umri wa miaka 21-30. Wapo wanaoolewa chini kidogo ya umri huo kulingana na muda waliokaa masomoni lakini kwa asilimia kubwa zaidi huwa ni kati ya umri huo.

Kama ndivyo, maana yake ni kwamba, msichana akifikisha umri wa miaka 32 na kuendelea anakuwa katika hatihati ya kuingia kwenye ndoa. Katika hili lazima nisisitize jambo moja muhimu, wapo wanaoolewa (kwa maana ya ndoa) hata na miaka 40 au zaidi.
Kuna mtindo wa watu wengi siku hizi kuamua kuishi pamoja bila ndoa kwa muda mrefu au wale ambao wamezaa na kuachana kwa muda, wana nafasi kubwa ya kuingia kwenye muunganiko wa ndoa hapo baadaye.

JAMBO LA KUJIFUNZA
Kwa mantiki hiyo ni vyema wasichana wakajipanga katika kipindi hicho cha umri wa usichana. Hapa ninamaanisha kuwa msichana anapaswa kuishi maisha sahihi, ajitunze mwili wake na awe kielelezo bora kwa wanaomtazama.
Kuishi katika mtindo bora ndipo hapo sasa atakapojiweka kwenye nafasi nzuri ya kuolewa na kujenga familia yake.

USICHEZEE HISIA ZAKO
Kuna binti aliniandikia meseji akasema: “Kaka Shaluwa, mpenzi wangu yaani simwelewi kabisa. Mchumba wake akirudi chuoni, yeye ananipita kama hanijui.
“Lakini cha kushangaza huyo mchumba wake akiondoka baada ya kumaliza likizo na kurudi chuoni basi atarudi kwangu na kutaka tuendelee na mapenzi yetu. Mimi nampenda, lakini ndiyo hivyo huyu mwanaume nahisi kama ananitesa tu. Naomba ushauri wako.”
Nilitumia muda kidogo kumjibu lakini kitu cha kwanza kumuuliza ni kuhusu umri wake, akanijibu ana miaka 19. Nikajua ni kwa namna gani nadili na mtu ambaye bado hajakomaa vizuri kiakili.
Kifupi huyu msichana anacheza na hisia zake na hajafahamu bado thamani ya mapenzi. Hajui thamani ya mwili wake, ndiyo maana anaweza kuuacha ukachezewa na mtu ambaye ana mtu mwingine.
Yupo tayari awe spea ya mwanaume ambaye huwa anamtumia kwa ajili ya ngono tu wakati mpenzi wake akiwa chuoni.

HEBU JITAMBUE
Elimu ya utambuzi ni kitu muhimu sana kwa binadamu aliyekamilika. Kwa bahati nzuri, suala la kujitambua ni zawadi ya pekee ambayo inakuwa ndani ya mtu tangu anazaliwa. Ni suala la kuitumia tu.
Lazima ujitambue na kujipa kipaumbele. Sikia nikuambie, uzuri ulionao leo hii wewe msichana wa miaka 23, hautaendelea kuwepo miaka saba ijayo hasa kama utajiachia hovyohovyo kwa wanaume na kuutumia mwili wako vibaya.
Tunza usichana wako, ishi kwa staha ili kujiwekea mazingira mazuri kwa ajili ya maisha yako ya baadaye.
Darasa litaendelea wiki ijayo, USIKOSE!
GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake