Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba
Wananchi wavamia kiwanda, wajeruhi walinzi
Aahidi kuwawekea wakili dhidi ya mwekezaji
Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, anatuhumiwa kushiriki kuchochea wananchi ili wafanye uasi na kujichukulia sheria mkononi kwa kuwahamasisha kuvamia kiwanda cha kusindika chai cha Mponde ambao wamefanya uharibifu mkubwa wilayani Lushoto.
Makamba ambaye anathibitisha kushiriki mkutano wa wakulima wa chai Bumbuli ambao wamefanya uharibifu na hujuma kubwa dhidi ya kiwanda hicho, pia anakiri kuwa aliitisha mkutano huo na kuridhia wakulima kufanya hujuma hizo.
Habari zinasema kuwa wananchi zaidi ya 200 walikivamia kiwanda hicho usiku wakiwa na silaha za jadi na kufanya uharibifu ikiwamo kujeruhi walinzi wa kiwanda hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costitane Massawe, akizungumza na NIPASHE kwa simu alithibitisha wananchi wengi wao wakiwa ni vijana kuvamia kiwanda hicho na kwamba amemtuma Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Lushoto kwenda eneo la tukio.
Hatua ya wananchi kukivamia kiwanda hicho imefuatia mkutano ulioitishwa Jumapili wiki iliyopita na Makamba ambaye pia Mbunge wa Bumbuli (CCM) na kutoa maazimio kifungwe kwa madai kuwa hawana imani na mwekezaji na Chama cha Wakulima wa Chai Usambala (UTEGA).
Hatua za kujichukulia sheria mkononi zinachochewa na Naibu Waziri Makamba wakati serikali ikihaha kuzima moto wa uasi wa wananchi mkoani Mtwara wakipinga kusafirishwa kwa gesi asilia wakati hawajui watakavyonufaika, hali inayotafsiriwa kama kuendeleza wimbi la kupuuza taratibu za kisheria kama msingi wa utawala bora nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Shadad Mullah, akizungumza na NIPASHE jana kwa simu kutoka Lushoto alisema wananchi hao walivamia kiwanda hicho kati ya saa 3:00 na saa 4:00 usiku na kufanya uharibifu ikiwamo kukata nguzo ya umeme unaoingia kiwandani hapo.
Mullah alisema kabla ya uvamizi huo kutokea, juzi mchana saa 9:00 alasiri waliteka magari nane yanayomilikiwa na kiwanda hicho yaliyokuwa yamebeba majani ya kupeleka kiwandani hapo na kuyamwaga na hivyo kusababisha hasara kwa kiwanda.
Mkurugenzi huyo alisema dalili za kutokea hujuma hizo zilianza kuonekana mapema baada ya mkutano wa mbunge huyo na siku iliyofuata watu wawili alifika kiwandani hapo ambao ni Almasi na Maulid na kueleza kuwa wametumwa na mbunge kukifunga kiwanda hicho.
Mullah alisema kutokana na hujuma hizo ambazo zimeleta athari kwa kiwanda kusimama uzalishaji, wanakusudia kufungua kesi mahakamani kumshitaki mbunge wa Bumbuli na wananchi waliohusika kuharibu mali za kiwanda.
“Wapo wabunge wa vyama vya upinzani waliofunguliwa mashtaka mahakamani kwa kudai kuchochea vurugu na ghasia, kwa nini Makamba naye asichukuliwe hatua kama wabunge wenzake,” alihoji Mullah.
Makamba akizungumza na NIPASHE kwa alithibitisha kufanya mkutano wa hadhara wa wakulima wa chai wa jimbo hilo na kwamba uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho uliamuliwa na wananchi wenyewe.
“Mimi sikuamuru wananchi wakifunge au wakafanye hujuma kama hizo katika kiwanda hicho isipokuwa katika mkutano niliouitisha walitoa azimio la kukifunga na kutoa sababu kuwa hawana imani na mwekezaji, UTEGA na pia wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao ya mauzo ya chai,” alisema.
Makamba alisema kimsingi anaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na wananchi hao kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata kero nyingi katika kiwanda hicho.
Alisema atawasaidia wananchi hao kwa kuwatafutia mwanasheria atakayesimamia kesi itakayofunguliwa na mwekezaji wa kiwanda hicho
Awali taarifa ambazo ziliifikia NIPASHE zilidai kuwa vijana waliovamia magari yaliyobeba chai kwenda kiwandani hapo walilipwa kiasi cha shilingi milioni mbili kutekeleza kazi hiyo tuhuma ambazo hata hivyo zilikanushwa na Makamba.
“Najua yatasemwa mengi kuhusu kinachoendelea kiwanda cha Mponde, lakini ukweli ni kwamba mimi sikuwalipa fedha yeyote vijana waliovamia gari moja lililobeba chai na kuimwaga,” alisema Makamba.
Makamba alichaguliwa kuwa mbunge wa Bumbuli kwa mara ya kwanza mwaka 2010 baada ya kumwangusha kwenye kura za maoni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Shellukindo, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Chai Usambara (UTEGA).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake