Advertisements

Friday, May 17, 2013

Simba yaichunguza Yaanga videon


Wakati vikosi vya Simba na Yanga vinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam leo jioni tayari kwa mechi yao ya kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa kesho, wachezaji wa 'Wekundu wa Msimbazi' jana waliwafanya 'ushushushu' dhidi ya mahasimu wao kwa kuangalia video za mechi za mabingwa hao wapya kama njia ya kuwakabili.

Jana mchana wachezaji wa Simba walikuwa kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli waliyofikia wakiangalia mechi tatu tofauti za Yanga dhidi ya timu mbalimbali ikiwamo dhidi ya Azam ambayo wachezaji wake walianzisha fujo zilizoshuhudia refa wa mechi hiyo Israel  Nkongo akipigwa na beki Stephano Mwasika.

Pia waliangalia mechi ya marudiano baina ya Yanga na Azam pamoja na mechi yao (Simba) dhidi ya Yanga ya mzunguko wa kwanza.

Akizungumza jana kwa njia ya simu kutoka Zanzibar, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na wanaamini ushindi utapatikana.

Alisema kwamba wachezaji wao yosso wameahidi kuweka rekodi mpya msimu huu kwa kuonyesha wanaweza na akawataka makocha wa timu nyingine kuwapa nafasi nyota wao chipukizi.

"Tuko imara na tumejiandaa kila idara na hatuna hofu, mazoezi ni mara mbili na mchana wa leo tumeisoma Yanga kupitia video," alisema kocha huyo msaidizi.

Julio alisema kwamba mchezo ambao Yanga ililala magoli 5-0 hawakuiangalia kwa sababu mchezo huo Simba waliwazidi na hivyo waliona haikuwa na changamoto za kujifunza.


Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kwamba wamejipanga kuhakikisha wanamaliza ligi kwa ushindi na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kwenda uwanjani kwa wingi kesho kusherehekea kombe lao.

Cannavaro aliiambia NIPASHE kwamba wanaifahamu vyema Simba na kwamba msimu huu wapinzani wao hawana kikosi kitakachoweza kuhimili kasi yao.

Beki huyo alisema kwamba wamefanya mazoezi ya aina mbalimbali na wamepata mbinu za kuikabili Simba na ubingwa wao wataupokea rasmi baada ya kuwafunga watani zao.

"Tunataka kukamilisha sherehe zetu kwa kuifunga Simba, msimu huu ni zamu yetu na hilo tumejipanga kudhihirisha Jumamosi," aliongeza Cannavaro.

Aliwataka wachezaji  wenzake kujipanga kulipiza kisasi cha msimu uliopita na wanaamini inawezekana kwa sababu kila penye nia matunda hupatikana.

Naye nahodha wa Simba, Juma Kaseja, aliliambia gazeti hili kwamba kikosi chao kiko imara na wanajipanga kumaliza ligi kwa ushindi.

Kaseja alisema kuwa licha ya kuvuliwa ubingwa Simba haijakata tamaa na ndiyo maana iliweza kujipanga upya na kufanya vizuri kwenye mechi zao za hatua ya lala salama.

Klabu hizo kongwe baada ya kumaliza ligi zitaanza maandalizi mapya ya kujiandaa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.

Nafasi ya pili tayari imeshikwa na Azam ambayo itamaliza ligi ugenini Arusha dhidi ya JKT Oljoro wakati Simba imejihakikishia kumaliza katika nafasi ya tatu ambayo inawawezesha kucheza michuano ya Ligi ya Super8.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hivi hii nayo ni 'news' jamani? Mbona utaratibu huo hufanywa na timu nyingi duniani ili kuwafahamu wapiinzani wao na pia kurekebisha makosa yao wenyewe. Miaka 51 ya uhuru utaratibu huu bado ulikuwa haujaingia Tanzania hadi muandishi kuandika kwa mshangao na kuuita 'ushushushu?'