Kocha msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelu
Kikosi cha Simba kiliondoka jijini Dar es Salaam jana jioni mchana na kuwafuata watani zao Yanga waliotangulia kisiwani Pemba ambapo kocha msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ametamba kwamba mabingwa hao wapya lazima wataondoka 'vichwa chini' baada ya mechi yao ya marudiano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi.Yanga ilitua Pemba tangu Ijumaa na Simba yenyewe iliwasili salama Unguja jana jioni.
Akizungumza na NIPASHE muda mfupi kabla hawajaondoka jijini, Julio, alisema wanakwenda Zanzibar wakiwa na wachezaji 25 na ni katika kukamilisha programu ya mazoezi waliyoianza wiki nane zilizopita na tayari matunda yake yalianza kuonekana kwenye mchezo wao dhidi ya Azam.
Julio alisema kuwa kamwe hawaihofii Yanga na wanajiamini kwamba wana uwezo wa kuwafunga na kuharibu sherehe za ubingwa huo ambao waliupata tangu Aprili 26 mwaka huu.
"Hatuwaogopi na safari ya Unguja ni kwenda kukamilisha kazi tuliyoianza, Simba haitishwi na Yanga, huu ni wakati wa kucheka kwa sababu wao hawana timu ya kutusumbua," alitamba beki huyo wa zamani wa Simba.
Aliongeza kwamba wachezaji wote wanaoondoka nao ni wazima na wakiwa Unguja watafanya mazoezi ya kusaka stamina ili kuhakikisha wanacheza kwa kasi dakika zote 90 za mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na Simba ndiyo ilianza kufunga wakati katika mchezo wa funga dimba msimu uliopita Yanga ilipata kichapo cha aibu cha magoli 5-0.
Hata hivyo, kikosi cha kwanza cha Simba kilichoivaa Yanga msimu uliopita kina mabadiliko makubwa baada ya Wekundu wa Msimbazi kuanza kuwatumia zaidi yosso wao wa timu B kufuatia kuwasimamisha 'mafaza' wakiwatuhumu kuhujumu timu.
Hata hivyo, 'presha' kubwa zaidi inatarajiwa kuwa kwa yosso wa Simba ambao wengi wao watakuwa wakicheza kwa mara ya kwanza mechi hiyo ambayo inategemewa kujaza zaidi mashabiki wa Yanga ambao watakuwa wakisherehekea kombe lao litakalokuwa uwanjani siku hiyo tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwao.
YANGA MAZOEZINI LEO
Baada ya jana kupewa mapumziko na kupata nafasi ya kwenda kutembelea ufukweni, wachezaji wa Yanga leo wanaanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mechi yao yao dhidi ya Simba.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana mchana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa wachezaji wote ni wazima na kocha aliamua kuwapumzisha ili kuwaandaa na mazoezi yatakayoanza leo asubuhi kwenye Uwanja wa Gombani.
Saleh alisema wachezaji pia wanahitaji mapumziko ya mwisho wa wiki ndio maana jana Jumapili aliamua kukatisha mafunzo na leo ataendelea na programu yake.
Meneja huyo alisema kwamba kwa siku zilizobaki hadi Jumamosi wachezaji watafanya mazoezi mepesi na kikubwa ni kukumbushwa namna watakavyowakabili watani zao Simba siku hiyo.
"Tunamshukuru Mungu wote tuko salama na leo (jana) tulikuwa na muda wa kupumzika, kazi iliyotuleta itaanza kesho (leo) Jumatatu na kubwa ni mbinu za kiufundi kwa sababu wachezaji kimwili wako tayari na mchezo," alisema meneja huyo.
Alisema kwamba kocha wao Mholanzi Ernie Brandts amefurahishwa na hali ya hewa kwa kuwa inafafa na ya Dar es Salaam na pia hali ya uwanja wa mazoezi licha ya kuwa na nyasi bandia.
Aliongeza kwamba kikosi hicho kitarejea jijini Dar es Salaam Ijumaa.
Yanga imetwaa ubingwa huo kufuatia kujipanga upya baada ya kuanza vibaya msimu wa ligi ambapo walifikia kumtimua kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment