Thursday, May 2, 2013

SIYO SAWA KUFANYA YAFUATAYO UKISHAACHANA NA MPENZI WAKO!

NDUGU zangu, mapenzi yapo lakini pia kuachana kwa wapenzi si jambo la ajabu. Leo hii na muda huu unaosoma makala haya, wapo ambao ndiyo kwanza wanaanzisha uhusiano lakini pia wapo ambao wanaachana.
Wanaoachana si kwamba wanafanya dhambi kubwa bali ni ukweli usioweza kupingika, huwezi kuendelea kuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako unakosa amani.

Unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye awali unahisi anafaa kuwa wako wa maisha lakini kadiri siku zinavyosogea unabaini si mtu sahihi na uamuzi sahihi ni kumuacha.
Hata hivyo, kuacha haiumi sana ila usiombe ukaachwa tena na mtu uliyetokea kumpenda sana. Inauma kupita maelezo lakini ikishatokea ndiyo hivyo huna la kufanya, utaumia weee mwisho wa siku utasahau na maisha yataendelea kuwepo.

Kitu ninachotaka kukizungumzia leo ni mambo ambayo hutakiwi kuyafanya pale inapotokea umeachwa au umemuacha mpenzi wako.
Kama nilivyosema, kuacha kupo na kuachwa kupo pia lakini kikubwa ni kujua jinsi ya kukabiliana na hali hizo zinapotokea. Unapoachana na mpenzi wako hakikisha hufanyi haya yafuatayo;

Kuiruhusu hali ya kuchanganyikiwa
Hili ni kwa wale walioachwa. Ukishaachwa na mtu ambaye huenda ulitokea kumpenda sana huna sababu ya kuhisi kudata na kuona maisha hayana maana tena kwako.
Unatakiwa kutuliza akili yako na kutafakari kwa nini umeachwa. Kuruhusu hali ya kuchanganyikiwa na kukufuru kwa kusema bora Mungu akuchukue ni kuonyesha udhaifu mkubwa sana.

Kujutia uamuzi wako
Kwa wewe ambaye umemuacha mtu ambaye ulikuwa unampenda lakini ukahisi hana vigezo vya kuwa wako wa maisha, hutakiwi kujuta na kuhisi umefanya dhambi kubwa.
Amini umechukua uamuzi sahihi na isije ikafika wakati ukaamua kufuta uamuzi wako. Simamia unachokiamini. Unaamini hakufai, muweke kando kisha yaache maisha yako yaendelee mbele.

Kumchafua mpenzi wako
Wapo ambao wakiachwa na wapenzi wao huanza kuwachafua na kufikia hatua ya kuzusha hata yale yasiyo na ukweli. Hii ni mbaya sana. Umeachwa, kubaliana na ukweli kwamba hukustahili kuwa naye na wala usikimbilie kuanika upungufu wake.
Hata wewe ambaye unaacha, sababu za kumuacha ni bora ukabaki nazo moyoni. Itakuwa si jambo jema kama utaanza kumwambia kila mtu kwa nini umemuacha. Mwisho wa siku haya ni maisha tu, mmeachana kimapenzi lakini maisha ya kawaida lazima yaendelee.

Kutafuta mwingine haraka
Ikitokea umeachwa au umeacha leo, hutakiwi kuharakisha kutafuta mwingine. Tuliza kichwa chako ili utakapoingia kwa mwingine usitimize ule msemo wa ‘kuruka majivu na kukanyaga moto’.
Kama umeachwa, jiulize ni kwa nini umeachwa na jaribu kubadilika kama unahisi kweli wewe ndiyo chanzo. Kujua kwa nini umeachwa itakufanya utakapoenda kwa mwingine uwe na uhakika wa kudumu naye.

Kutengeneza uadui
Wapo ambao wakishaachana na wapenzi wao, wanawageuza na kuwa maadui. Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utamfanya adui mpenzi wako wa zamani, kwa kipi?
Labda iwe amekufanyia ubaya ambao kila mmoja ataona huna sababu ya kumchekea lakini kama umemuacha kwa sababu ameshindwa kuwa mauminifu kwako au sababu nyingine ndogondogo, hutakiwi kumfanya adui yako mkubwa.
Ninachotaka kusema ni kwamba, kila siku watu wanaachana lakini tunapoachana tunaweza kuendelea kushirikiana katika mambo mengine yanayogusa maisha yetu.

Kubembeleza uhusiano
Kama umeachwa, ujue huna nafasi tena kwake. Kubaliana na kile kilichotokea na jipange upya kutafuta mwingine. Kitendo cha mpenzi wako kukuambia hakutaki na kuanzia leo kila mmoja ashike hamsini zake kisha wewe ukabembeleza afute uamuzi wake, utakuwa unakosea.
Tambua mtu akishakuambia hakutaki ujue hilo limetoka moyoni mwake na kwamba hata kama utabembeleza itakuwa ni kazi bure. Anaweza kukuonea huruma akakuambia muendelee lakini kiukweli utakuwa huna nafasi moyoni mwake na wakati wowote anaweza kukuumiza zaidi.

Tuonane wiki ijayo.

GPL

No comments: