ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 6, 2013

Tanzania yaongoza EAC kwa saratani ya shingo ya kizazi

Dar es Salaam. Pamoja na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo kwa wanawake nchini, ni asilimia 66 tu ya wanawake wa miaka kati ya 15 na 49 wana taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) mwaka 2011, Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kansa hiyo.
Matokeo hayo Tanzania ina wastani wa wagonjwa 50 kwa kila wanawake 100,000 wa saratani ya shingo ya uzazi.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa kwa mwaka 2011 wastani wa vifo kutokana na ugonjwa huo ilikuwa 37.5 kwa kila wanawake 100,000 na katika wagonjwa wote wa saratani waliotibiwa Ocean Road, asilimia 36 waliugua saratani ya shingo ya kizazi .
Tume ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika utafiti wake ulifanyika kati ya mwaka 2011 na 2012, inabainisha kuwa ukosefu wa elimu na kipato duni ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanawake wengi kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo.
Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 52 ya wanawake wasiokuwa na elimu ya sekondari na chuo kikuu, ndio walipata taarifa juu ya ugonjwa huo huku asilimia 75 ya wanawake wasomi walikuwa na taarifa sahihi.
Tafiti zinasema ukaaji wa mijini na vijijini pia unachangia hali hiyo, kwani wanawake wengi wa mjini wana fursa ya kupata taarifa kutokana na urahisi wa kufikiwa na vyombo vya habari tofauti na wenzao wa vijijini. 
Mwananchi    

No comments: