ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 17, 2013

UKO KWENYE HUBA AU UTUMWA WA MAPENZI?-2


IMEZOELEKA sana kusikia watu wakizungumza kuhusu suala la utumwa wa mapenzi. Hata hivyo hakuna ufafanuzi wa moja kwa moja watu wanaoutoa wakati mjadala huu ukiendelea huko mitaani.

Utumwa ni kupelekeshwa. Kufanyishwa au kufanya kitu ambacho si mapenzi yako. Kufanya mapenzi yako halafu matokeo kuwa hasi. Huo ndiyo utumwa.
Ndugu zangu, wiki iliyopita nilianza kwa kufafanua kwa mapana sana, leo hebu twende tukaone zaidi.
Sikia nikuambie rafiki, baadhi ya wasichana, akitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajitahidi kumpenda taratibu akiwa naye ndani ya uhusiano.
Siyo sahihi kabisa, huo ni utumwa ndugu yangu. Huwezi kujilazimisha kumpenda mtu kwa sababu ya mali.
Hata siku moja, mali au fedha haziwezi kununua penzi la dhati ndani ya moyo wa mtu.
Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.
Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama si kuambulia kipigo, basi utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo. Yote hayo ya nini? Una sababu gani ya kuishi kwa presha kiasi hicho?
Tafuta furaha katika maisha yako, kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo wa kuanzisha uhusiano ukiwa na uhakika huna mapenzi ya dhati. Ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa.
Tambua thamani ya mapenzi kwa kuheshimu hisia zako za ndani. Unapoamua chochote kuhusu mapenzi ujue unaamua jambo linalohusu maisha yako. Amini maneno yangu rafiki yangu.
Unda furaha katika maisha yako. Siku zote nimekuwa nikisema, maisha ni mapenzi na mapenzi ni furaha. Unapoishi kwa furaha na kujiamini, unajiweka katika nafasi ya kuishi maisha marefu zaidi ya wale ambao siku zote nyuso zao zimetawaliwa na mikunjo ya huzuni. Chukua hili kutoka kwangu. Ahsante kwa kunisoma rafiki yangu. Wiki ijayo nitakuwa hapa na mada nyingine.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

GPL

No comments: