ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 21, 2013

Usuluhishi ziwa Nyasa waiva

Msuluhishi wa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, Rais Mstafu wa Msumbiji, Joachim Chissano, ameziita pande husika kwenda Msumbiji kwa ajili ya kupokea taarifa kuhusiana na upatanishi huo.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema Tanzania na Malawi zimetakiwa kwenda nchini humo kupokea taarifa hizo baada ya jopo la wanasheria wa Chissano kukaa na kupitia taarifa na vielelezo kuhusu mgogoro huo kutoka pande zote mbili.

Alisema wanatarajia kwenda nchini humo kupokea taarifa hizo ama mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao. “Jopo la wanasheria wa Chissano limekutana kwa ajili ya kupitia taarifa zetu za serikali mbili, ya Tanzania na Malawi, sisi Tanzania tutaitwa rasmi hivi karibuni kati ya mwisho wa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao,” alifafanua Waziri Membe.Kwa mujibu wa Waziri Membe, wanaotakiwa kwenda huko ni Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje kutoka nchi hizo.

Alisema Tanzania itateua jopo la wanasheria watakaokuwamo katika ujumbe utakaokwenda kupokea taarifa hizo. Chissano ni kiongozi wa Jopo la Marais Wastaafu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Viongozi hao wastaafu watatoa taarifa yao baada ya kupitia maelezo ya taarifa zilizotolewa kutoka pande zote mbili kuhusu mpaka wa ziwa Nyasa.

Baada ya viongozi hao kutoa taarifa yao, pande husika zitaamua kuendelea na upatanishi huo ama kwenda kwenye vyombo vingine vya usuluhishi ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Jopo la wanasheria na wataalamu wa masuala ya migogoro wanaoshirikiana na jopo la marais wastaafu ni Jaji Raymond Ranjeva, Jaji Mstaafu wa ICJ; Profesa George Kanyeihamba, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda; Jaji Baney Afako, Mshauri wa Masuala ya Sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan na Dk. Gbanga Oduntun, Profesa wa Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon.

Wengine ni Profesa Martin Pratt, Mkurugenzi wa Utafiti wa Jiografia na Mipaka; Dk. Dire David Tladi, Mjumbe wa Kamisheni ya Sheria ya Umoja wa Mataifa na Miguel Chissano, Kiongozi wa Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu.

Mwaka jana, Rais wa Malawi, Joyce Banda, aliibua mgogoro mzito kati ya nchi hiyo na Tanzania kuhusu mpaka wa ziwa Nyasa, kwa madai ya kwamba eneo lote la ziwa hilo lipo upande wa Malawi, akisema kuwa Malawi ina miliki asilimia 100 ya ziwa hilo.

Mpaka halali na ambao umekuwa ukitumiwa kwa muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi, tangu enzi za mataifa ya Uingereza na Ujerumani yaliyotawala nchi hizo ni ule unaopita katikati ya ziwa Nyasa. Tanzania inasisitiza kuwa kila nchi ina miliki asilimia 50 wa ziwa Nyasa.

Baada ya kuzuka mgogoro huo, maofisa wa nchi hizo walianzisha mazungumzo ambayo hata hivyo, yalikwama baada ya Malawi kujitoa kwa visingizio mbalimbali.

Hata baada ya ya jopo la Chissano kuingilia kati kufanya upatanishi, Malawi imekuwa ikilituhumu kwamba kinavujisha siri za usuluhushi kwa Tanzania.

MKUTANO WA KIMATAIFA KUFANYIKA NCHINI
Katika hatua nyingine, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa utakaokutanisha viongozi wakuu kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili nafasi ya sayansi na teknolojia katika kuondoa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta mbalimbali zikiwamo za uchumi katika mataifa hayo.

Mkutano huo unaojulikana kama majadiliano yenye manufaa kwa wote ‘Smart Partnership Dialogue’, unatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kukutanisha takribani washiriki 500.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mkutano huo uliowakutanisha mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, Waziri Membe alisema hadi sasa marais 10 waliopo madarakani na watano wastaafu kutoka nchi mbalimbali wamethibitisha ushiriki wao.

Aliongeza kuwa ndani ya saa 24 kuanzia jana, anatarajia kutuma taarifa zaidi kwa vyombo vya habari kuhusu idadi ya washiriki watakaothibitisha kuhudhuria mkutano huo.

Aliongeza kuwa maandalizi ya mkutano huo yanakwenda vizuri na kwamba serikali inahakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa safi na salama zikiwamo barabara zake kwa kuwa dunia nzima itakuwa jijini humo. Alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete aliridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwenye mkutano wa mwisho kuhusu majadiliano ya jinsi hiyo uliofanyika kwa mara ya mwisho Juni mwaka juzi katika mji wa Putrajaya, Malaysia.

Membe aliwahakikishia wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuwa mkutano huo utakuwa ni wa mavuno kwao na kuwataka kujipanga vyema kibiashara ili kunufaika na fursa hiyo ambayo kwa Tanzania ni ya kipekee. Kwa upande wake, Meneja Mradi wa mradi huo, Rosemary Jairo, alisema kuwa takribani wataalamu 106 wa fani mbalimbali zikiwamo za uchumi, sayansi na teknolojia kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wataandaa mada tofauti zitakazojadiliwa kwenye mkutano huo.

Pia kutakuwapo na maonyesho yatakayohusu masuala ya sayansi na teknolojia, uchumi, mafuta na gesi.
Washiriki wakuu wa mkutano huo ni marais, mabalozi, mawaziri, makatibu wakuu na viongozi kutoka taasisi mbalimbali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: