Tatizo ni mke wa Rais Ravalomanana kuamua kuwania uraia baada ya mumewe na mpinzani wake kukubaliana kutogombea urais ili kuleta utulivu wa kisiasa.
Goodluck Eliona, Mwananchi Tarehe 14 Desemba, 2012 Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina aliwasili nchini kwa mara ya kwanza kwa ziara ya siku mbili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kujadili hali tete ya kisiasa nchini mwake na mustakabali wake wa kisiasa.
Mazungumzo yao yaliwakutanisha tena Januari mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine Rajoelina alikubali kutowania urais kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Julai 24, mwaka huu akifuata hatua iliyokuwa imeafikiwa na mpinzani wake wa kisiasa, Rais Marc Ravalomanana.
Rajoelina alisema badala yake atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2018.
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) alipewa jukumu na viongozi wenzake kukutana na viongozi wakuu wa kisiasa wa Madagascar kuwaelezea uamuzi wa mkutano wa viongozi hao wa Sadc ambao ulipendekeza viongozi hao kutokugombea urais ili kurejesha amani iliyokuwa imelegalega nchini humo.
Uamuzi wa viongozi hao wawili wa kutokugombea urais ulipunguza msuguano wa kisiasa uliokitikisa kisiwa hicho kwa takriban miaka mitatu na hivyo kuweka matumaini ya kuboresha utawala wa kidemokrasia ulioingia doa.
Hata hivyo, inaonekana kuwa viongozi wote wawili walikubali kwa shingo upande kutokuwania nafasi ya urais. Mdomoni walisema tunakubali lakini moyoni walihifadhi neno ‘hapana’.
Ikiwa imebakia miezi miwili kufanyika kwa uchaguzi mkuu Madagascar, tayari vikumbo vya wawaniaji urais vimeanza kuonekana katika daftari la orodha ya wanaotaka kiti hicho.
Mke wa Rais Ravalomanana, Lalao Ravalomanana ndiye aliyepuliza kipenga cha vikumbo na kuvunjika kwa ahadi za kutokugombea zilizokuwa zimewekwa, hii ni baada ya mwanamama huyo kuorodhesha jina lake kuwa miongoni mwa wagombea wa kiti hicho.
Kitendo cha mama Ravalomama kimechukuliwa na wadau wa masuala ya kisiasa nchini Madagascar kuwa ni mbinu ya Ravalomanana ya kurudi Ikulu kupitia mkewe.
Rais Rajoelina, ambaye aliingia madarakani mwaka 2009 kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi, amekwishatangaza kutengua ahadi yake ya kutokugombea urais.
Mshauri wa Rajoelina, Augustin Andriamananoro amenukuliwa na vyombo vya habari Mei 4, mwaka huu akisema kuwa makubaliano yamevunjwa na mke wa Ravalomanana.
“Sasa ushindani ni kwa mtu yeyote anayetaka kugombea urais,” alisema Andriamananoro na kuongeza kuwa Rajoelina alisafiri kwenda Dar es Salaam kuonana na Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Sadc, Rais Kikwete kumweleza hatua mpya aliyoichukua.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Ijumaa wiki iliyopita Rais Kikwete alikutana na Rajoelina kwa mara ya tatu na kwamba katika kikao cha mwisho kilichofanyika Januari, Rajoelina alikubali kutokugombea kwenye uchaguzi mkuu utaofanyika mwaka huu.
Rajoelina aliyezaliwa Mei 30, 1974 ni mfanyabiashara maarufu anayemiliki kampuni kadhaa vikiwemo vyombo vya habari nchini Madagascar. Pia, amewahi kuwa meya wa Jiji la Antananarivo hadi alipotimuliwa na Rais Ravalomanana.
Mgogoro kati ya Rajoelina na Ravalomanana
Mwaka 2008 Serikali iliifungia televisheni ya Rajoelina ijulikanayo kama Viva TV kwa kosa la kufanya mahojiano na Rais wa zamani wa Madagascar, Didier Ratsiraka ambayo yalionekana kuharibu amani na usalama wa nchi.
Uamuzi wa Serikali ya Ravalomanana uliwakasirisha wananchi ambao walikuwa tayari wameshakerwa na mambo mengine yaliyofanywa na utawala huo ikiwa ni pamoja na hatua ya Ravalomanana ya kusaini mkataba na Korea Kusini kutumia sehemu ya ardhi kwa ajili ya kilimo.
Wiki moja baada ya Viva TV kufungiwa, Rajoelina alikutana na viongozi 20 wa upinzani akiwataka waandae tamko la pamoja la kumshinikiza Rais Ravalomanana afuate utawala wa kidemokrasia. Tamko hilo lilitangazwa baadaye katika uwanja wa wazi, huku Rajoelina akiahidi kuandaa mikutano mingi zaidi ya hadhara.
Januari, 2009 aliitisha mkutano mkubwa katika viunga vya Antananarivo uliohudhuriwa na watu 3,000 na kupaita mahala hapo kuwa ni eneo la demokrasia. “Kwa sababu Rais hataki kuwajibika, natangaza kuanzia leo masuala yoye ya taifa hili nitayaendesha mimi,” alisema Rajoelina na kuwashangaza wafuasi wake ambao wengi ni watu wa kipato cha chini.
Siku tatu baadaye, Rais Ravalomanana alimtimua Rajoelina kutoka katika kiti cha meya na kumteua Guy Randrianarisoa kushukilia nafasi hiyo. Hata hivyo, Rajoelina alipinga uamuzi wa kuvuliwa madaraka na badala yake akamteua Michele Ratsivalaka kurithi kiti cha meya.
Rajoelina aliongoza maandamano ya kuivamia Ikulu kwa lengo la kumng’oa Ravalomanana, ambapo katika purukushani watu 31 waliuawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa. Mwezi mmoja baadaye, Machi 18, 2009 jeshi lilimkabidhi Rajoelina mamlaka ya kuiongoza Madagascar na kuapishwa akiwa na umri wa miaka 35 huku akiingia katika historia ya kuwa Rais mdogo aliyeitawala nchini hiyo.
Mapinduzi hayo yalilaaniwa na jumuiya za Kimataifa huku Umoja wa Afrika ukiifuta uanachama na kuitishia kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.
Kwa kuwa asilimia zaidi ya 70 inategemea misaada ya kimataifa, vikwazo vilivyowekwa vimeathiri sana uchumi wa Madagascar.
Kwa namna hali ya kisiasa inavyoendelea Madagascar inailazimu Sadc kukaa upya na kutafuta ufumbuzi kabla ya uchaguzi mkuu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment