Saturday, May 25, 2013

Wajerumani kuiteka Wembley

Ni fainali ya kwanza inazikutanisha timu zote kutoka Ujerumani katika historia ya michuano hiyo.
London, England. Kwa timu iliyopeta mechi tano za fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya mechi sita, Bayern Munich haiwezi kwenda uwanjani bila kuwa na hamasa ya ushindi katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo dhidi ya  Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Wembley, London leo hii.
Ni fainali ya kwanza inawakutanisha timu zote kutoka Ujerumani.
Mwaka jana, walipoteza mchezo wa fainali kwa kufungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani na Chelsea, na safari hii inacheza ugenini dhidi ya Wajerumani wenzao.
Ingawa ilitwaa taji mwaka 2001, lakini kilichofanywa na wakongwe wa klabu hiyo miaka ya 1970 kama Franz Beckenbauer, Gerd Muller, Sepp Maier na Uli Hoeness, kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo, kinabaki kuwa kumbumbuku.
Wengi wanaamini, Bayern ya safari hii iko kwenye kiwango kizuri pengine kupita wakati mwingine wowote, na kwamba fainali ya leo ni wakati mwafaka wa kufuta machungu ya kukosa taji mara tano baada ya kupoteza kwenye mechi ya fainali.
Bayern ya mwaka huu imesimama imara ikivunja rekodi 30 kuelekea kutwaa taji la 23 la Ligi Kuu Ujerumani msimu huu. Moja ya rekodi mpya ni kuongoza msimamo wa ligi, mwanzo mpaka mwisho wa msimu.
Na baada ya hapo waliendelea kuvunja rekodi moja baada ya nyingine na kutwaa taji mapema zaidi kabla ya kumalizika msimu, kitu ambacho hakijawahi kufanya na klabu nyingine yoyote katika historia ya soka la Ujerumani.
Imemaliza msimu ikiwa mbele kwa tofauti ya pointi 25 dhidi ya wapinzani wao Dortmund wanaopambana nao leo. Imemaliza ligi na pointi 91, ikiwa ni rekodi mpya, lakini pia wakifungwa mabao machache zaidi na kuandika rekodi nyingine.
Ushindi wa jumla wa mabao 7-0 dhidi ya Barcelona katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo ni rekodi nyingine waliyoweka mwaka huu, huku ushindi wa mabao 4-0 katika hatua ya robo fainali dhidi ya mabingwa wa Italia Juventus nayo ni rekodi mpya.
Katika mchezo huo, Borussia Dortmund itamkosa kiungo wake mchezeshaji, Mario Gotze ambaye ni majeruhi.
Gotze (20) hajacheza tangu alipoumia nyonga mwezi uliopita kwenye mchezo wa nusu fainali ya marudiano dhidi ya  Real Madrid.
Beki Lukasz Piszczek naye atacheza mchezo wa mwisho wa Dortmund kabla ya kufanyiwa upasuaji wa paja, huku mshambuliaji Robert Lewandowski (24), akicheza mechi yake ya mwisho kwa klabu hiyo ya Dortmund
Mwananchi

No comments: