
Sauda Mtondoo
KWA UFUPI
Ofisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Pwani, Iroga Nashoni alisema hali ya bahari imebadilika na kuwa mbaya zaidi.
Rufiji. Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Sauda Mtondoo amepiga marufuku usafiri wa boti kutoka Mafia kwenda Nyamisati, wilayani Rufiji, kutokana na hali ya bahari kuendelea kuwa na mawimbi makubwa na upepo mkali.
Akizungumza kwa simu jana, Mtondoo alisema baada ya kutokea maafa ya wananchi wilayani Rufiji, wameona ni vyema kuzuia usafiri huo kwa muda na utaruhusiwa hali ya bahari itakapokuwa shwari.
Alisema jukumu la Serikali ni kulinda raia na mali zao, kutokana na hali ya bahari kuwa mbaya hakuna jinsi, wananchi wawe wavumilivu na hali iwe shwari.
Ofisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Pwani, Iroga Nashoni alisema hali ya bahari imebadilika na kuwa mbaya zaidi.
Nashoni alisema mawimbi yamekuwa makubwa yanakwenda juu mita tatu na upepo unavuma kwa kilomita 40 kwa saa moja, jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa usafiri wa majini.
Alisema kutokana na hali hiyo wamelazimika kuzuia vyombo kuingia baharini, kutokana na kuchafuka na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu kipindi hiki.
Katika hatua nyingine, watu tisa ambao hawajaonekana baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama wanahofiwa kufa.
No comments:
Post a Comment