ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 29, 2013

Kikwete: Afrika ibadilike

  Asisitiza sayansi na teknolojia kuboresha maisha
Rais Dk .Jakaya Kikwete amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kubadilika kwa kuwekeza kwenye  sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wake na maendeleo endelevu ya bara  hilo.

Amesema changamoto kubwa inayoikabili Afrika ni ukosefu wa teknolojia ya Sayansi  inayotoka nje ya bara hilo ambayo ni ghali kwa serikali na watu binafsi.

Dk. Kikwete alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano unaohusu Majadiliano ya Kimataifa kwa Manufaa ya Wote (ISPD)  2013, unaohudhuriwa na  marais  9, marais wastaafu watano, wakuu wa serikali na wajumbe wapatao 800 kutoka nchi mbalimbali duniani.


Alisema Afrika haitaweza kupiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii bila ya uwekezaji  wa kutosha katika Sayansi na Teknolojia.

Alisisitiza kuwa uwekezaji huo ufanyike kwa vijana ambao mustakabali wa bara la Afrika  unawategemea wao. Alisema mapinduzi ya Sayansi na Teknolojia ndiyo yatakayorahisisha huduma za kijamii katika nchi hizo.

“Tukiwekeza kwenye elimu ya Sayansi na Teknolojia  tutasonga mbele katika maendeleo  na kuinua uchumi wa nchi zetu kutokana na ubunifu watakaojifunza vijana wetu,” alisema.

Dk. Kikwete alisema nchi zinazoendelea zina changamoto kubwa ya kupambana na  matatizo yao kutokakana na kukosa elimu ya Sayansi na Teknolojia.
Alisema upatikanaji wa teknolojia na ubunifu ndio njia pekee itakayozikomboa nchi hizo.

“Bidhaa nyingi za teknolojia zikipatikana, hazishikiki kutokana na gharama kubwa, lakini tukiwa na uwezo wa kuzitengeneza wenyewe, tutasonga mbele,” alisema na kuongeza kwa kuwataka viongozi hao kulijadili suala hilo katika mkutano huo.

 Hata hivyo, Dk. Kikwete alisema nchi zote za Afrika zinapaswa kuanza elimu ya sayansi na teknolojia kwa watoto wao kuanzia shule za msingi.
Aidha, alizishauri nchi za Afrika kuanzisha vyuo vikuu na taasisi za utafiti wa Sayansi na Teknolojia kinyume chake mustakabali wa Afrika utakuwa shakani.

Marais wengine waliotarajiwa kuwasili kwenye mkutano huo ni pamoja na Uhuru Kenyatta wa Kenya  ambaye hakuweza kufika baada ya kutoa udhuru.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: