ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 28, 2013

KUGUNDUA NA KUANZISHA UHUSIANO ULIO SAHIHI!

WENGI wamekuwa wakiumia mioyo yao kutokana na kukosa penzi la kweli au kuingia katika penzi la kitapeli wakiamini ni penzi la dhati. Tatizo hili limekuwa likiwasumbua wengi, inawezekana hata wewe limekukuta!

Mara nyingi jambo hilo husababishwa na kukosa umakini kabla na baada ya kuanzisha uhusiano wa mapenzi. Hapa sasa ndipo mateso na misukosuko inapoanzia.
Ukiona mtu ameanza kuchanganyikiwa kutokana na mapenzi ni wazi kwamba kila kitu kitakuwa hakiendi sawa, maisha yanabadilika, kila anachokipanga kinavurugika, ufanisi kazini unashuka na inawezekana hata bosi wake anafikiria kumuachisha kazi kutokana na matatizo ya aina hiyo.
Kimsingi haya ni matatizo sugu katika maisha ya kiuhusiano na ni vyema kama utajifunza mapema jinsi ya kuepuka kufanya uchaguzi usio sahihi na mwisho wake maisha yakuharibikie.
Kubwa zaidi katika eneo hili ni kwamba mhusika akiwa kwenye matatizo haya, mwisho wake ni kukosa furaha na kuwa na simanzi. Muda mwingi atautumia kuwaza na kunyong’onyea akijilaumu kwa kufanya makosa makubwa katika maisha yake.
Inawezekana tayari umeshaingia kwenye ndoa lakini kila siku maneno hayaishi, amani hakuna na umekata tamaa kabisa. Rafiki yangu, bado lipo tumaini na ninakuhakikishia mara baada ya kumaliza kusoma mada hii kuna kitu kitaingia kichwani mwako.
Mada hii nimeigawa katika sehemu mbili, kabla ya kuingia kwenye uhusiano na ndani ya uhusiano ambapo kuna wengine tayari wanakuwa na ndoa zao kabisa.

KABLA YA UHUSIANO
Hapa nazungumza na wale ambao bado hawajaingia kwenye uhusiano. Nitafafanua mambo ya msingi ambayo unatakiwa kuzingatia kabla ya kuingia katika uhusiano utakaokusababishia matatizo.
Ukigundua vitu vya kuepuka kabla ya kuingia katika uhusiano itakusaidia kufanya maamuzi sahihi na kuingia katika uhusiano mzuri, wenye mwanga mbele yako.
Hebu tuone...

(i) Fikiria zaidi
Simanzi huletwa na mateso ambayo mhusika huyapata akiwa katika uhusiano ambao hakuutarajia. Hii inamaanisha kwamba ama mpenzi aliyenaye hampendi au yeye mwenyewe amekuja kugundua kwamba hampendi!
Hisia hizi zinatosha kumuingiza katika simanzi ya moyo. Kugundua kwamba mpenzi aliyenaye hampendi kwa dhati ni tatizo kubwa sana, maana hapa lazima ataanza kumfanyia vitimbi na kumkosesha raha.

Wiki ijayo tutaona zaidi, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: