Wednesday, June 5, 2013

MAISHA NDIVYO YALIVYO:Mke wangu akiwa hana kazi mstaarabu, akiwa kazini hunidharau, nifanyeje?

Na Flora Wingia
Mpenzi msomaji, wiki iliyopita tulikuwa na mada kuhusu dharau. Nikauliza ni kwanini neema au mafanikio yanapoanza kuonekana dharau huanza kuchipuka. Wapo baadhi ya wasomaji wetu wamechangia maoni kuhusu jambo hilo.

Wasomaji waliochangia wanasema hivi;
….Cha kufanya ni kwamba familia imeshaneemeka, wazazi wawe wazi kwamba kipato cha kila mmoja kijulikane, kiwekwe mezani, kipangiwe taratibu za maendeleo ya familia.

Na kama kuna mjeuri inabidi mmoja afanye mambo mazuri na kipato chake ili mwenzake aone ni yapi na mangapi ya maana anafanya nafsi yake itamsuta. Au unasemaje ndugu Mhariri?(Mr. Ewald J. Kiria wa Kibosho, Moshi). Nakubaliana na wewe kabisa msomaji wangu.
“….Aunt Flora, nimeanza kusoma makala zako tangu nikiwa sekondari miaka ya 1990 na sasa ni mama wa watoto.
Kuhusu kwanini dharau huanza baada ya familia kuneemeka ni kweli kabisa pepo hili lipo hasa kwa wanaume pale mwanamke utakapoanza kuonyesha mafanikio inferiority complex inamjaa. Kila utakachofanya hata jema linakuwa baya kisa umekuwa meneja, umeteuliwa mkurugenzi.

Hata kama unajenga na unamtaarifu na site hakanyagi, taabu kweli kweli mpaka unatamani ukatengue kile kiapo cha ndoa cha kanisani kuwa yale maneno ‘Mpaka Kifo Kitakapotutenganisha’ hayakuwa yangu nilipewa niyasome tu kama nilivyosoma makala nyingine. Ogopa cheti unachopewa bure bila kukifanyia mitihani utaikuta ndani,” ndivyo anavyomaliza ujumbe wake.

…Hii tabia kwa ujumla huchangiwa na wanaume wanapopanda vyeo na kuhamishwa kikazi kwa visingizio vya nyumba huku akiwa gesti na nyumba ndogo.

Kwa mfano mimi mwenyewe mume wangu yuko Kusini ana cheo cha ngazi ya mkoa lakini nilienda mpaka kwa RC(Mkuu wa Mkoa), lakini vitisho nilivyopewa inasikitisha. Yeye hajui tunakula nini. Kwa hili serikali inachangia inapomhamisha mtu anaacha mke nyumba.(msomaji Dodoma).

…Mkono mtupu haulambwi. Marafiki wa yule apataye neema huchangia kuwapo dharau. Ukichomoza, marafiki wanakumwagia sifa. Ukilewa hizo sifa tu dharau!(Meleck, China).

…Anti Flora, mimi naitwa Peter kutoka Arusha naomba ushauri. Mke wangu akiwa hana kazi ananiheshimu kupita maelezo. Akianza kazi tu ananidharau. Kwa sasa ametoka likizo ya uzazi na ana mwezi tangu aanze kazi.

Nikimuuliza kitu anajibu mkato na iko siku niliahidiana naye niende kazini kwake lakini akiwa bado hajaniona nikamkuta kijana mmoja kasimama naye huku akimwambia yule mwanaume ‘nitoe basi’.

Yule jamaa akamwambia nitakutoa baadaye. Sasa mimi nikashindwa kuelewa kuna biashara gani wanayofanya na mke wangu. Kazi yake ni usafi tu kwenye ofisi. Siku nyingine nikamkuta jamaa anamshika shika. Mimi kazi yangu dereva. Nifanyeje?

Mpenzi msomaji, nimejaribu kupitia maoni ya wenzetu hapo juu nimegundua yafuatayo. Lipo suala la wivu mbaya kwamba kama mama kaonyesha mafanikio fulani, basi baba badala ya kufurahia huonyesha kuchukizwa . Huu ni wivu mbaya.

Kwa mfano msomaji aliyetoa maoni hapo juu kwamba amejitahidi akaanza kujenga. Lakini kila akimtaarifu baba angalau aende kutizama au achangia mawazo yeye hakanyangi. Hii maana yake ni nini? Kama huyu baba ana wivu na kijidharau cha moyoni ni kitu gani? Wapo baadhi ya kina baba wenye gubu la aina hii. Hafurahii mafanikio ya mwenzake.

Lingine nimeona kuhusu vyeo. Wapo kinamama ambao wanapopata vyeo, huonyesha vijidharau kwa waume zao hasa kama cheo hicho kinamzidi mumewe. Lakini hii ni mara chache kwani wengi huboresha maisha ya familia.

Lakini cheo akipata baba hapo ndipo ngoma huanza. Hata nyumba ndoa ambayo hakuwa nayo huichipua haraka. Na wabaya zaidi ni wale wanaopandishwa cheo, kisha kuhamishwa kituo cha kazi.

Ametoa mfano msomaji wetu hapo juu kuwa mumewe alipandishwa cheo na kupelekwa mkoani. Lakini mama alipomfuatilia akapata vitisho. Hili ni tatizo kubwa ambalo serikali nayo kwa upande wake inapaswa kulitizama kwa macho mawili kwani linaboa familia badala ya kujenga.

Mwingine amezungumzia ulevi wa sifa. Kwamba marafiki wanakumwagia sifa na pale zinapokulewesha dharau zinaanza unasahau hata familia yako. Na wakati mwingine hizo sifa siyo za kutoka moyoni bali wanakubeza, au kukudharau kwa namna fulani. Unatapaswa kutafakari mara mbili mbili unaposifiwa kuona ni za kweli?

Naam. Mpenzi msomaji, hayo ndiyo niliyoweza kukumegea kwa leo. Wiki ijayo tutajadili wale kinamama wanaoaga waume zao kwamba wanasafiri kwenda kwao kusalimia kumbe wamejichimbia mahali fulani na wachuchu/washikaji. Upo hapo? Usilikose

No comments: