ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 5, 2013

Serikali tatu: Mzigo mzito

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maua Daftari
Mapendekezo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuhusu muundo wa serikali tatu, umeibua kauli za kukinzana miongoni mwa wabunge.

Kundi moja linatoa kauli zinazobainisha kuwa sasa kila upande ubaubeba mzigo wake.
Hata hivyo, wananchi na makundi mengine ya jamii yameunga mkono mapendekezo mengi yaliyomo katika rasimu hiyo na kukosoa machache.

Miongoni mwa wabunge wanaotoka Zanzibar, wameelezea wasiwasi kuhusu hatima ya kiuchumi na kiusalama kwa eneo hilo la Muungano, ikiwa litaachwa kuwa katika mamlaka yake kamili. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maua Daftari, alisema Zanzibar haijaimarika kiasi cha kuwa na uwezo wa kuhudumiwa serikali yake na kuchangia katika serikali ya Muungano. “Ni lazima tuwe wakweli, Zanzibar inasaidiwa kwa kiasi kikubwa na Muungano kwa kutegemea rasilimali za Bara, sasa tukisema tujitenge, si rahisi (Wazanzibari) tukamudu kuiendesha serikali yetu na kuichangia ile ya Muungano,” alisema jana wakati wa kutoa maoni yake kuhusiana na tume kupendekeza kuwapo kwa serikali ya Zanzibar, Tanzania Bara na Shirikisho.
“Ingefaa zaidi kabla ya kuwasilisha mapendekezo hayo, Tume ingezitafakari faida na hasara za serikali tatu, na mimi binafsi naona hasara zake ni nyingi kuliko faida,” alisema Daftari ambaye kwa asili anatokea Zanzibar.

Daftari aliyewahi kushika nyadhifa tofauti serikalini ukiwamo naibu waziri, alisema ni vizuri kwa Zanzibar kujitafakari upya kuhusu kuingia katika mfumo wa serikali tatu, huku akikielekezea kidole Chama Cha Wananchi (CUF) kuwa watetezi wa mfumo huo.

“CUF walihamasishwa sana kuhusu kuwapo kwa serikali tatu, kwa maana tangu awali Muungano unaonekana si sehemu ya hitaji lao,” alisema.

Daftari alisema miongoni mwa hofu inayomkabili ni kuhusu hatima ya wafanyabiashara Wazanzibar waliowekeza na kuweka makazi ya kudumu upande wa Bara, ikiwa zitaundwa serikali za Zanzibar na Tanganyika (Bara).

“Wazanzibar wanafanya biashara sana Bara, wamejazana kila sehemu ya nchi, sasa tukifikia kila upande kuwa na serikali yake, maana yake itabidi warudi Zanzibar ili serikali ya Bara iwatambue na kuwahudumiwa raia wake,” alisema.

Alisema hali ilivyo sasa, wafanyabiashara hao wanaendesha shughuli zao pasipo kubughudhiwa, hali ambayo bila shaka itawaathiri ikiwa Bara itaunda serikali yake.
Daftari alisema jambo la msingi lililopaswa kufanyika ni kushughulikia kero za Muungano pasipo kuathiri muundo wa Muungano.

SANYA: WAZANZIBARI KUNUFAIKA
Hata hivyo, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya (CUF), alisema pendekezo la kufikia serikali tatu ni muhimu na litafanikisha azma ya kuwa na Zanzibar yenye kuwanufaisha zaidi Wazanzibari.

Alisema hofu zinaelekezwa katika masuala kama uchumi, uwekezaji na ulinzi, hazina msingi kwa sababu yatashughulikiwa kwa uadilifu na kujali misingi ya utaifa pasipo kuwaathiri watu wa upande mmoja wa Muungano.

“Mbona watu wanaangalia mambo mabaya tu kwa kuwapo serikali tatu, hawasemi mambo kama Mfuko wa Muungano uko wapi hadi sasa,” alisema.

Sanya alisema zipo sheria na maazimio ya mahusiano na ujirani yatakayoongoza mchakato wa kuzishughulikia haki za Wazanzibari waliopo Bara kama itakavyokuwa kwa Wabara waliopo Zanzibar.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), alisema suala la serikali tatu linahitajika uangalifu, kwa kuwa linaweza kusababisha udhaifu katika Muungano.

MKULO ZANZIBAR ITACHANGIA
Mbunge wa Kilosa, Mustafa Mkulo, (CCM), ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne ya uongozi, aliunga mkono serikali tatu, na kusema alipokuwa Waziri, alipata malalamiko makubwa kutoka Zanzibar kuhusiana na masuala ya fedha.

“Kwa mpango huu, wataanza kuchangia katika shirikisho la Muungano, watachangia kulipia mabalozi mambo ambayo walikuwa hawafanyi kwa sababu waliokuwa wakiumia kulipa gharama zote hizo ni Tanzania Bara,” alisema.

SERUKAMBA MUUNGANO HATARINI
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisema mfumo unaoifaa Tanzania ni serikali mbili na kwamba itakapoundwa ya tatu ni sawa na kuuvunja Muungano.

“Kwa kukubali serikali tatu kunausogezea muda kidogo Muungano huu ufe,” alisema.

Pia alisema gharama za utawala zitakuwa kubwa kwa kuwa na serikali tatu na kuhoji kwanini fedha hizo zisipelekwe katika maeneo ambayo yana matatizo kama maji na kilimo.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alihofu muundo wa serikali tatu kuwa huenda ukasababisha kuvunjika kwa Muungano.
“Kama hiyo ndiyo njia ya kutatua matatizo mbalimbali ni sawa, lakini utaratibu huo unaweza ukauvunja Muungano,” aliasa.

MBATIA: NI MAJIBU YA MIAKA MINGI
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema pendekezo la kuwepo serikali tatu linakidhi matakwa ya harakati zilizoanzishwa Juni 12, 1991 jijini Dar es Salaam, kupitia Kamati ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba ambayo alishiriki.

Alisema harakati hizo ziliwaathiri watu wengi akiwamo yeye mwenyewe kwa kufukuzwa Chuo Kikuu, huku wengine wakiwekwa ndani.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikosoa pendekezo la kutaka Naibu Spika asitokane na chama cha siasa.

Ndugai alisema, pasipo kuhusishwa na kuwa katika wadhifa huo, Naibu Spika anapaswa kutofautishwa na Spika, hivyo kupewa haki ya kikatiba, atokane na chama cha siasa akiwa miongoni mwa wabunge.

“Kwa Spika asitokane na chama cha siasa, hilo si tatizo, lakini Naibu Spika atokane na chama cha siasa miongoni mwa wabunge, kwa sababu mfumo huo ndio unaotumiwa na mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo Tanzania ni mwanachama wake.

Ndugai alisema pia ni vigumu kujadili muundo wa serikali ya Tanganyika (Bara) kama itaundwa, kwa vile mpaka sasa haipo kama ilivyo kwa upande wa Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ).

LIPUMBA AHOJI GHARAMA
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema licha ya tume kujitahidi kuandaa rasimu ya Katiba yenye maoni yaliyotolewa na wadau, kuna mambo bado hayajaeleweka.

Alisema hadi jana alikuwa bado hajaiona rasimu hiyo, lakini kwa kuangalia muhtasari wake jambo la kwanza, ambalo hajalielewa linahusu namna uendeshaji wa Serikali ya Shirikisho na utakavyogharimiwa.

“Warioba hakueleza hilo. Alizungumzia suala la kodi, lakini yale mambo ya Muungano aliyoyataja hayana chanzo cha kupata mapato. Labda litakuwamo kwenye hiyo rasimu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema anahoji hilo kwa kuwa ni wazi kuwa kwa vyovyote vile, namna ya uendeshaji na kuigharimia serikali hiyo litakuwa zito.

Alisema pendekezo la kuanzishwa kwa serikali ya Tanzania Bara maana yake ni kwamba, kutakuwapo na mchakato mpya wa kupata Katiba ya serikali hiyo.

“Kama kutakuwa na mchakato huo, je, mchakato wetu wa kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hatima yake ikoje?” alihoji Profesa Lipumba.

DK. KITIMA: WABUNGE WAWILI HAPANA
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk. Charles Kitima, alipinga pendekezo la kila jimbo la uchaguzi kuwa na wagombea wawili mwanamke na mwanaume.

Badala yake alipendekeza kila mgombea achaguliwe kwa sifa na uwezo wake wa kufanya kazi na siyo kwa sababu ya jinsia yake au hali yake ya ulemavu.

Dk. Kitima alisema dhana kwamba wanawake wanahitaji kupewa nafasi za uongozi sawa na wanaume imetokana na mfumo mbovu wa kiutawala.

Hata hivyo, alisema nchi ikiwa na utawala wa sheria unaozingatia maslahi ya wananchi walio wengi hakuna mtu hata mmoja atajiona amenyimwa haki kushiriki ujenzi wa taifa au kufaidi matunda ya uhuru.

DK. MKUMBO: RAIS BADO MADARAKA MENGI
Mhadjiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, alisema rasimu bado inampa madaraka makubwa Rais yakiwamo ya kuwateua viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Alisema a kitendo cha bunge kwenda kuwathibitisha watendaji hao ni kama “danganya toto”.
Alisema Rais ni miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais na kwamba ikiwa anahusika kuwateua watendaji wa tume hawatakuwa na uhuru wa kufanya maamuzi sahihi.

‘ARDHI IINGIZWE KATIKA KATIBA’
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wasomo Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema taifa lolote ni lazima liwe na ardhi iliyowekewa utaratibu mzuri wa kuimiliki ili wananchi wake wanufaike.
Alisema kuwa katika nchi nchingi umiliki wa ardhi huwa ni chanzo cha migogoro na vita, hivyo kutoliweka suala la ardhi kwenye katiba ni upungufu mkubwa.

“Nchi huwa zinakwenda vutani kutokana na kugombea ardhi, hata wazee wetu akina Mkwawa, Mtemi Mirambo na Kinjektile Ngwale walipigana na Wazungu wakitetea ardhi ya himaya zao, ni lazima watanzania tutambue kuwa suala la ardhi sio la kupuuza ni lazima liingizwe kwenye katiba kwa kuliwekea utaratibu mzuri wa kuimiliki,” alisema Mwaihojo.

WATETEZI HAKI ZA BINADAMU WAMEACHWA

Mwanasheria ambaye ni mtafiti wa utetezi wa haki za binadamu, Onesmo Olenguruma, alisema kuwa rasimu hiyo ni nzuri, lakini haijatambua na kuyapa nafasi mashirika ya utetezi.

Olenguruma ambaye pia ni mkurugenzi wa mtandao wa haki za binadamu hapa nchini alifafanua kuwa rasimu hiyo ya katiba imetambua haki za binadamu, lakini wanaopigania haki za binadamu ambayo ni mashirika hayajapewa kipaumbele kuweza kufanya kazi hiyo.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Joel Mmasa, alisifia rasimu ya katiba hiyo kwa kuwa imeweka vipaumbele vingi vilivyotolewa na wananchi wakati wa kukusanya maoni.

TEC: TUME IMEFANYA KAZI KUBWA
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Antony Makunde, alisema kazi iliyofanywa na Tume ya Mabadiriko ya Katiba ni kubwa na kwamba kama mapendekezo hayo yatapita kama yalivyo, yataleta mabadiliko makubwa hususani katika nyanja ya utawala na uongozi.

Pia alisema ni mwanzo mzuri kwa pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar kutulia na kuijadili kwa kina rasimu hiyo.

“Ni kazi kubwa sana ambayo imefanywa na Tume, ila ni mwanzo mzuri pia kwa wananchi kutulia kuijadili kwa kina rasimu hii kwa sababu ni mapendekezo yanayohitaji uelewa zaidi,” alisema na kuongeza:

“Pia Tume ina kazi nyingine ya kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi ili washiriki ipasavyo katika kuijadili kwa sababu baadhi ya mapendekezo yanahitaji uelewa zaidi na kama yote yaliyopendekezwa yatapita, yataleta mageuzi makubwa sana.”

WASOMI IRINGA: MWANZO MZURI
Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Tumaini, Profesa Seth Nyagava, alisema kuwa kupunguzwa kwa madaraka ya Rais na matokeo ya uchaguzi mkuu kuhojiwa mahakamani ni mwanzo mzuri.

Mhadhiri na Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Tumaini, Renatus Mgongo, alisema rasimu hiyo, imefungua njia kwa kupanua wigo katika masula ya msingi yanayohusu haki za binadamu ikiwamo haki za binadamu,wajibu wa raia na mamlaka ya nchi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha, Rwezaura Kaijage, alisema tume imefungua njia na kurejesha yale yote yaliyokuwa yakikataliwa na baadhi ya viongozi yasiingie kwenye katiba.

ATAKA SERIKALI YA TANGANYIKA
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mount Meru, Dk Simon Kadigumira, alisema naunga mkono mapendekezo ya rasimu hiyo, lakini akasema hakubaliani na jina la Serikali ya Tanzania Bara.

Alisema Tanzania inatokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivyo vema serikali ya Tanganyika ikawekwa kwenye Katiba Mpya.

Dk. Kadigumira alisema kwa muda mrefu Watanzania Bara walikuwa wakipunjwa katika mfumo wa serikali mbili.

Kuhusu hoja ya mgombea binafsi, alisema anaunga mkono kwa kuwa itaondoa urasimu wa vyama vinavyodai kuwa na dhamana ya kuongoza nchi.

WAZANZIBARI WAFURAHIA
Wanasiasa, wanasheria na wanaharakati Zanzibar wamesema rasimu mpya ya katiba inaonesha mwanga wa kupata katiba nzuri na kutoa ushauri kwa wanasiasa kutowaingilia wananchi wakati wa kujadili rasimu hiyo katika ngazi ya mabaraza ya katiba.

Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamid Mwezeleni, alisema suala la katiba linahusu wananchi na siyo vyama vya siasa, asasi za kiraia na taasisi nyingine mbalimbali.

“Asitokee mtu akawasemea Wazanzibari kuhusu rasimu hiyo wala kuweka mbele maslahi ya vyama vyao kwa sababu wasomi wako wachache na hata idadi ya wafuasi wa vyama vya siasa ni ndogo kuliko Watanzania wasiokuwa na chama chochote cha siasa,” alisema Mbwezeleni.

CUF: NI MAPEMA KUSEMA KITU
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani, alisema ni mapema kwa chama chake kutoa msimamo kuhusu rasimu hiyo hadi watakapojifungia na kuipitia kifungu kwa kifungu hasa kwa kuzingatia maoni ya Wazanzibari wengi yalikuwa yanafungamana kwa kutaka Muungano wa mkataba.

“Kwa upande mmoja nampongeza Jaji Joseph Warioba kwa kueleza ukweli kuwa maoni ya Wazanzibari wengi walikuwa wakitaka Muungano wa Mkataba ingakuwa hakusema ni asilimia ngapi, hivyo kuna mambo ambayo yanahitaji kujadiliwa na viako vyetu na baadaye kutoa msimamo wetu baada ya kuichambua rasimu hiyo,” alisema Bimani.

CCM ZANZIBAR: DAWA YA KERO ZA MUUNGANO
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema rasimu hiyo itasaidia kumaliza kero za Muungano na kuimarisha misingi ya amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Vuai alisema kwamba tume imezingatia maoni ya wananchi waliokuwa wengi na jambo la msingi kwa wanaharakati, vyama vya siasa na wananchi wenyewe kuheshimu maamuzi ya waliokuwa wengi katika suala zima la upatikanaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye mwanaharakati wa Zanzibar, Rashid Salum Adi, alisema rasimu hiyo siyo mwarubaini wa matatizo ya Muungano kwa vile tatizo kubwa ni mfumo wa siasa uliopo pamoja na ukosefu wa mamlaka kamili.

Wakati huo huo, maskani maarufu CCM iliyopo Kisonge imetoa ujumbe kupitia ubao wake wa matangazo kuhusu rasimu mpya ya katiba ukisema ‘Rasimu hii safari itafika, iwe kwa jahazi, gari au ndege’ na kusababisha watu wengi kusimama na vyombo vya moto kwa muda wakisoma maandishi hayo na wengine kurushiana kupitia ujumbe wa simu.


KIKWETE ATOA SALAMU
Rais Kikwete ametoa pongezi kwa Jaji Warioba na wajumbe wengine wa tume hiyo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwezesha kupatikana kwa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa ameamua kutoa pongezi hizo kwa sababu anatambua kazi iliyofanywa na tume hiyo, kwani kuzunguka pande zote za nchi kusikiliza maelfu ya wananchi ni kazi kubwa na pevu.

Alisema kuwa kazi nyingine iliyokuwa ngumu zaidi kwa wajumbe wa tume ni ya kuchambua maoni na mapendekezo yote lukuki yaliyotolewa na kuamua yale ya kupendekeza yaliyojumuishwa katika rasimu waliyoitangaza juzi; kwamba kwa umahiri wao matokeo ya kazi yao ni ya kiwango cha hali ya juu.

Rais Kikwete alisema tume imemaliza kazi yake ya msingi ya kutayarisha rasimu hiyo na kwamba kinachofuatia ni kwa wajumbe wa mabaraza ya katiba na wananchi kuijadili rasimu hiyo na kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu namna ya kuiboresha.

Rais aliwataka Watanzania kuitumia vizuri mabaraza ya katiba kutoa maoni yao yatakayoboresha rasimu hiyo ili katiba kupata nzuri yenye kutetea maslahi ya taifa kwa miaka mingi ijayo kwa umoja, amani, upendo, mshikamano.

Alivipongeza vyombo vya habari katika mchakato wa kupatikana rasimu hiyo kwa kuelimisha jamii.

Imeandikwa na Mashaka Mgeta na Sharon Sauwa, Dodoma; Muhibu Said, Richard Makore, Isaya Kisimbilu, Elizabeth Zaya, Dar; George Ramadhan, Mwanza; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Ashton Balaigwa, Morogoro; Godfrey Mushi, Iringa; John Ngunge, Cynthia Mwilolezi, Arusha na Mwinyi Sadalah, Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments: