ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 27, 2013

Mandela kama Nyerere

Ule usemi kuwa “duniani wawili wawili” huenda ukawa na ukweli kama tutaangalia mazingira ya ugonjwa na kifo cha  Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na mazingira ya kuugua na hali aliyo nayo hivi sasa, Baba wa Taifa la Afrika Kusini isiyo na ubaguzi, mzee Nelson Mandela maarufu kama Madiba.

Mpaka sasa mazingira yanaonyesha kufanana kwa kiwango kikubwa katika maeneo mengi, mbali na ukweli kwamba wawili hawa ni viongozi mashuhuri waliolijengea jina bara la Afrika na kulifanya liheshimike katika anga za kimataifa, kwa namna kila mmoja wao alivyotoa uongozi wa mfano kabla na baada ya kustaafu kwao kwa hiari, japokuwa wangeweza kuendelea kuziongoza nchi zao.

Mwalimu Nyerere alilazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London nchini Uingereza  kwa ugonjwa wa saratani ya damu tangu Septemba 24 mwaka 1999 na kufariki dunia Oktoba 14 mwaka huo, siku 22 baada ya kulazwa.
Kwa upande wake, Mandela ambaye anapigania uhai wake, alilazwa tangu Juni 8, mwaka huu katika Hospitali ya Medi-Clinic, iliyo katika Jiji la Pretoria ikiwa ni siku ya 20 kufikia leo.


Kadri matibabu ya  Mwalimu yalivyokuwa yakiendelea na hali yake ilivyokuwa ikibadilika na kuwa mbaya kiasi cha kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua, Ikulu ya Tanzania  kupitia kwa aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa na mwandishi wake wa habari, Geoffrey Nkurlu, walikuwa wakitoa taarifa kwa umma kuujulisha maendeleo ya ugonjwa kwa ujumla.

Hivyo ndivyo inavyofanyika hivi sasa kueleza maendeleo yote ya ugonjwa wa mzee Mandela na hali ya kuwekewa mashine za kumsaidia kupumua kupitia kwa Rais Jacob Zumma au kwa msemaji wake.

Kwa muda wote wa ugonjwa wa Mwalimu Nyerere hadi kifo chake, umma wa Watanzania ulishiriki kumwombea kupitia kwenye makanisa, misikiti na sehemu zingine ili apone, na umma ulifuatilia kwa shauku kujua habari za maendeleo yake.

Hali hiyo inafanana na hali ilivyo nchini Afrika Kusini ambako wananchi wa nchi hiyo wamefanya ibada mbalimbali za kumuombea Mzee Mandela ili apone, huku wakipeleka kadi na maua ya kumtakia afya njema hospitalini na salamu za kumtakia afya njema kupitia kwenye vyombo vya habari.

Siyo kwamba habari za kuugua kwa Mwalimu Nyerere zilifuatiliwa na Watanzania pekee, bali ulimwengu wote kwa ujumla wakiwamo marais wa mataifa makubwa ambao baadhi kama Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, walijitolea kusaidia matibabu yake katika hospitali bora za Marekani.

Hali hiyo pia inatokea hivi sasa kutokana na dunia nzima wakiwamo viongozi wa nchi na serikali wakiwamo wastaafu kufuatilia kwa karibu hali ya Mzee Mandela tangu alipoanza kuugua.

Wakati bara zima likiendelea kumuombea Mandela aliyeko hospitalini wakati huu, liko pia kwenye ugeni mzito wa rais Barack Obama wa Marekani ambaye ataitembelea vile vile nchi hiyo katika ziara ya kikazi iliyoanzia nchini Senegal jana usiku na kutarajiwa kuwasili Afrika Kusini kesho na baadaye Tanzania Jumatatu ijayo.

Kama gazeti la Independence lilivyoeleza katika tolea lake la hivi karibuni kuwa, huenda ziara ya Obama katika nchi hiyo, pengine na bara la Afrika kwa ujumla, ikamezwa na hali mbaya ya kiafya aliyonayo Mzee Mandela.

HALI ILIVYO AFRIKA KUSINI
Wakati Mandela akiwa mahututi, wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, wameanza kuandika jumbe mbalimbali za kukata tamaa juu ya uhai wake kwenye kuta za hospitali ambako amelazwa.

Baadhi ya jumbe hizo ni pamoja na ile uliotundikwa kwenye shingo ya kikatuni ambacho kimelazwa kwenye kitanda huku kitanda kilicholala kikatuni kikiwa kimezungukwa kwa mashada ya maua kuashiria hakuna uhai tena kwa kiongozi huyo.

Ujumbe huo unasomeka hivi: “Asante kwa yote uliyotutendea kwa ajili ya nchi yetu.”

Ujumbe wote unaashiria kutokuwa na uhakika wa kuwa naye tena kiongozi huyo huku nyingi zinazodaiwa kuandikwa na watoto zinaeleza kuwa “siku zote utakuwa hadithi ya kweli kwetu na babu kwetu sisi sote. Tata Mandela umegusa maisha yetu, tunakupenda pia njia hiyo uliyoendea ni yetu sisi sote.”

Nyumbani kwa Mandela jijini Johannesburg, vyombo vya habari kutoka kila kona ya dunia vimepiga kambi vikisubiri habari yoyote kuhusu jabali hilo lililopigana na siasa za ubaguzi wa rangu na kutumikia jela kwa miaka 27 chini ya utawala wa makaburu.

Maua yametanda nje ya nyumba yake, huku ujumbe mbalimbali ukiwa umeandikwa kwenye mawe, mwingi ukimtakia kila la kheri.

Hata hivyo, wananchi wengi katika viunga vya Johannesburg wanaamini kuwa serikali inawaficha kuhusu ukweli hasa wa afya ya Mandela. Wengi waliohojiwa na waandishi wa habari wanaamini kuwa Mandela amekwisha kufa.

Wanaamini kuwa ama serikali inataka Mandela afikishe umri wa miaka 95 mwezi ujao, au wanataka kupisha kwanza ziara ya Obama.

Kwingineko duniani, watu mbalimbali wamekuwa wakimuombea uzima kiongozi huyo humo huku macho yote ya wananchi yakiwa kwa kiongozi wa taifa hilo, Rais Jocob Zuma, kuweka wazi juu ya hali yake.

Tangu Jumapili iliyopita, afya yake ilipozidi kudhoofu vyombo vya habari duniani vimekuwa vikizunguka katika Hospitali ya Medi-Clinic mjini Pretoria ili kujua ukweli wa hali yake.

ASKOFU MKUU AMWOMBEA MANDELA 
Askofu Mkuu, Thabo Makgoba, nchini humo, alimuombea Mandela sala ya mwisho ya amani baada ya kumtembelea hospitalini hapo na kuona hali yake hairidhishi.

Katika maombi hayo, Askofu Makgoba aliomba pamoja na mke wake kiongozi huyo, Graca Machel.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: