Saturday, June 15, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-10

Kuendelea na mada yetu, nilitoa mfano wa Romeo na Shantale. Romeo hakumjali Shantale, badala yake akajiingiza kwenye uhusiano na mwanamke mwingine ambaye ni Jannine. Huyo alijitahidi kumpa kila kitu lakini hakupata mapenzi anayostahili, zaidi akawa ananyanyasika.

Shantale anampenda sana Romeo ambaye yeye moyo wake upo kwa Jannine. Shantale akawa anamjali Romeo kwa kila hali lakini hakuambulia mrejesho wowote wa mapenzi yake. Romeo naye akawa hasikii, haambiwi kwa Jannine ambaye naye hakurejesha upendo kwa Romeo.
Romeo anaendelea kusimulia: “Kwa maana hiyo, nilikuwa na Shantale kama mwanamke wa kwenye kapu, sikumjali kabisa, marafiki na wafanyakazi wenzangu walimjua Jannine peke yake. Ndugu zangu, hususan dada zangu waliwajua wote na siku zote waliniambia mwanamke mzuri ni Shantale na kwamba Jannine hanifai, kwani si mjenzi wa familia, bali ni mwanamke mwenye dharau, maringo na kauli chafu.
“Nilipomuwaza sana Shantale nikakumbuka ukarimu na wema wake kwangu. Hata siku moja hajawahi kuninyanyasa. Alinisaidia nikiwa na shida, tena hakunisimanga. Nilipomwambia tuachane, hakusema vitu alivyoninunulia nimrudishie, alinibembeleza tu nisimuache kwa sababu ananipenda sana.
“Nilichanganua kwa marefu na mapana, mwisho nikagundua kwamba Shantale ni mwanamke mwenye thamani kubwa lakini namnyanyasa. Nilimuona ni almasi iliyochanganywa na chupa, kwa hiyo si rahisi kuitambua na kujua thamani yake. Kikubwa kilichonivutia kwake ni kauli, Shantale ana kauli nzuri sana.
“Kikubwa kilichonikimbiza kwa Jannine ni kauli, maana mdomo wake ni mchafu mno. Asubuhi palipopambazuka, nilimtumia SMS Jannine, nikamwomba tuonane, kwanza alichelewa kunijibu, baadaye akaniambia ataangalia ratiba zake kama itawezekana.
“Alizidi kunifanya nimuone hanifai baada ya mimi kumuuliza kama ana ratiba gani tofauti na za kawaida akitoka kazini, akasema alikuwa amepanga kukutana na marafiki zake waende ufukweni. Akanisisitizia ni mtoko wa yeye na wanawake wenzake na ni muhimu kwake.
“Nikamtumia SMS Shantale kuomba kuonana naye, baada ya muda mfupi ilijibiwa kwamba yupo tayari, akaniuliza saa. Kwa mara ya kwanza nilimtoa ‘out’ Shantale, tukaenda kwenye hoteli yenye mandhari tulivu, nikamuomba msamaha kwa kujifanya kipofu siku zote hata nikaacha kuuona upendo wake.
“Nilipomuomba msamaha Shantale alilia, bila shaka hakuamini maneno yangu. Nikatoa pete ya uchumba nikamvalisha na nikamuomba anikubalie nianze taratibu za kumchumbia kihalali nyumbani kwao ili nimuoe kabisa. Ilikuwa siku nzuri sana kwetu, Shantale alikuwa mwenye furaha sana.
“Baada ya siku mbili, sikuona sababu ya kutaka kuonana na Jannine wakati mtu mwenyewe alikuwa haonekani kujali, nilimtumia SMS kumfahamisha kuhusu uamuzi wangu wa kusitisha uhusiano wetu, akanijibu maneno makali. Kwa kifupi alinitukana sana.
“Mimi na Shantale ukurasa ukafunguliwa upya, kuanzia hapo nikaanza kuuona ule uchangamfu wake wa siku za nyuma umerudi, maana kuna kipindi alikuwa mpole sana, tena mnyonge. Taratibu zote nilifuata, tukafunga ndoa, Mungu akatujalia kupata watoto wawili wazuri na maisha yetu ni mazuri sana, kwa maana tunaelewana, hatuna migogoro, tunasikilizana.
“Shantale ni mwanamke bora sana lakini kidogo nimpoteze. Angekuwa mapepe, asingekuwa na mimi leo. Ila uvumilivu wake umekuwa nafuu kwangu. Vilevile kwake, kwa maana sasa hivi nampa mapenzi ya kipekee sana, nikifidia nyakati ambazo nilimsaliti. Nasema asante Mungu kwa kunifanya mimi Romeo kuwa mume wa Shantale.”
Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake