Maandamano nchini Misri
Jeshi la Misri limeonya kuwa litatumia nguvu dhidi ya makundi yatakayosababisha ghasia na machafuko wakati wa maandamano ya leo.
Mkuu wa majeshi Jenerali Abdel Fattah al-Sisi ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kuandamana katika b arabara za mji kuunga mkono juhudi zao za kukabiliana na vitendo vya kigaidi.
Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi vile vile wanatarajiwa kushiriki katika maandamano hayo.
Bwana Morsi amekuwa akizuiliwa na jeshi tangu tarehe tatu mwezi huu.
Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali amesema, Bwana Morsi anazuiliwa kuhusiana na uhusiano na wapiganaji wa Kiislamu wa Hamas nchini Palestina.
Shirika la habari la serikali, Mena, limesema Bwana Morsi anachunguzwa kufuatia madai kuwa anashirikiana na kundi hilo la Hamas kushambulia vituo kadhaa vya polisi na magereza wakati wa mageuzi ya mwaka wa 2011.
Lakini chama chake cha Muslim Brotherhood, kimesema kuwa kilipata msaada kutoka kwa raia wa nchi hiyo kushambulia magereza na wala sio raia wa kigeni kama inavyodaiwa.
Maandamano nchini Misri
Kiongozi huyo kwa kwanza kuwahi kuchaguliwa kwa njia ya Kidemokrasia kuongoza Misri, aliondolewa madarakani baada ya raia wa nchi hiyo kuandamana wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja tangu alipochukua madaraka.
Tangu wakati huo, Bwana Morsi amekuwa akizuiliwa na jeshi la nchi hiyo katika eneo lisilojulikana.
Shirika hilo la Mena limesema agizo lilitolewa kwa rais huyo kuzuiliwa kwa muda wa siku kumi na tano.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo anasema kuwa tangazo hilo sasa limeondoa wasi wasi kuhusiana na hatma yake, hasa kufuatia shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa ya kutaka rais huyo wa zamani kauchiliwa huru an kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi Kanali Ahmed Mohammed Ali amesema jeshi la nchi hiyo litaruhusu maandamano ya amani lakini ameonya kuwa watakabiliana vikali na kundi lolote ambalo litajaribu kusababisha machafuko.
No comments:
Post a Comment