
Askari wa kikosi cha Zimamoto wa mjini Pretoria nchini Afika Kusini wakiimba nyimbo za kumtakia afya nje Rais Mstaafu wa nchi hiyo, Nelson Mandela walipofika nje ya Hospitali ya MediClinic alipolazwa kiongozi huyo. Picha na AFP.
Johannesburg. Madaktari wanaomtibu Nelson Mandela wameishauri familia yake iondoe mashine zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’.
Taarifa hizo zimo kwenye viapo vya wanafamilia hao ambavyo viliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Eastern Cape, Mthatha ambako familia hiyo ilikuwa ikipambana kurejesha mabaki ya miili ya watoto wa Mandela kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Wanafamilia 16 walifungua kesi mahakamani akiwemo mkewe Graca Simbine Machel Mandela na mtalaka wake Winnie Madikele Mandela dhidi ya walalamikiwa watatu akiwemo Zwelivelile Mandle Sizwe Dalibhenga, maarufu Mandla, ambaye ni mjukuu wa Mandela.
Mandela ambaye aliongoza vita ya ubaguzi wa rangi enzi za utawala wa mabavu wa Makaburu, alilazwa tangu Juni 8 mwaka huu katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliyopo Pretoria ambako hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya sana.
Juzi na jana afya ya kiongozi huyo ilizua utata na mvutano mkubwa kutokana na kutolewa kwa taarifa kwamba madaktari wanaomtibu walishauri familia yake iondoe mashine zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’.
Hati za viapo hivyo zinathibitisha kwamba Mandela anapumua kwa mashine na madaktari wanaomtibu waliishauri familia kuondoa mashine hizo suala ambalo limebaki katika mikono ya familia.
Viapo hivyo viliandikwa Juni 26 mwaka huu na kuwasilishwa mahakamani Juni 28, lakini havikuwahi kutolewa hadharani hadi Julai 3, wakati uamuzi wa kesi ulipotolewa na kumwamuru mjukuu wa Mandela, Mandla arejeshe mabaki ya miili ya watoto wa babu yake Qunu.
Mabaki hayo yaliyohamishiwa Mvezo 2011 ni ya watoto wa Mandela ambao ni Madiba Thembekile aliyefariki kwa ajali ya gari 1969, Makgatho aliyefariki 2005 na binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) aliyefariki dunia 1948 akiwa mtoto mchanga.
Mabaki hayo yalizikwa juzi Alhamisi katika makaburi ya familia, Qunu ikiwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama.
Kati ya juzi na jana, Ikulu ya Pretoria ililazimika kutoa taarifa mbili; moja muda wa jioni na nyingine usiku wa kuamkia jana ikiwa ni hatua ya kuondoa hofu iliyokuwa imeanza kusambaa baada ya vyombo vya habari kuweka bayana kilichoandikwa katika viapo vya mahakama.
Hoja kubwa ambayo imekuwa ikijadiliwa ni kwa jinsi gani viapo vya mahakama vionyeshe kwamba uwezekano wa Mandela kuendelea kuishi ni mdogo huku Serikali ikitoa taarifa kwamba hali ya Mandela ni imara licha ya kwamba yu mahututi.
Katika taarifa zote mbili Rais Jacob Zuma kupitia kwa msemaji wake, Mac Maharaj aliweka wazi kwamba Mandela ‘siyo mtu wa kufa wakati wowote’ kama ilivyoripotiwa ikasisitiza kwamba hali yake imeendelea kuwa imara licha ya kwamba ni mgonjwa sana.
Jana asubuhi, mmoja wa wanaharakati waliopinga ubaguzi wa rangi, Denis Goldberg naye aliungana na Serikali akisema kwamba hali ya rafiki yake Mandela siyo mbaya kama ambavyo iliripotiwa na vyombo vya habari.
“Kweli ni wazi kwamba ni mgonjwa sana, lakini alikuwa bado ana hisi na alijaribu kuchezesha midomo yake na macho yake pia wakati nilipomsemesha hospitalini,” alisema Goldberg ambaye aliwahi kufungwa wakati wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
“Si kwamba hatambui kabisa kwa sababu alijua mimi ni nani wakati nikiwa hospitali,” aliongeza.
Juzi mchana kwa mara ya kwanza Machel alizungumzia afya ya mumewe kwa kusema kuwa licha ya kulazwa kwa siku zaidi ya 25, lakini si mara zote amekuwa katika maumivu makali.
“Ni kama siku 25 tuko hospitalini kwa ajili ya matibabu, pamoja na kwamba wakati mwingine hali yake inakuwa siyo nzuri ni mara chache anapatwa na maumivu,” alisema Graca.
Hati za viapo
Nyaraka hizo za mahakama katika kesi ambayo matokeo yake yanaelekeza ni wapi atakakozikwa Mandela akifariki dunia, ziliweka wazi kwamba mzee huyo mwenye miaka 94 ‘matumaini yake ya kuishi ni finyu’.
Nyaraka hizo ni viapo ambavyo familia ya Mandela iliviwasilisha mahakamani chini ya hati ya dharura ambavyo vinawahusisha wanafamilia 15 wakiwamo mtoto wake wa kwanza wa kike, Makaziwe, mke wake Graca Machel na mtalaka wake Winnie.
Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba Mandela anayepumulia mashine muda wote hali yake ni mbaya na kwamba madaktari walishauri mashine zizimwe kwani zisingeweza kusaidia chochote.
“Familia imeshauriwa na madaktari mashine za kumsaidia kupumua zizimwe kutokana na hali yake,” zinasema nyaraka hizo na kuongeza: ‘Badala ya kuendeleza/kurefusha maumivu yake, familia inaangalia uwezekano wa kuzingatia ushauri huo’.
Wakili wa familia hiyo Wesley Hayes, alisema nyaraka hizo zilikuwa sehemu ya jitihada za kuhakikisha kwamba mahakama inaona udharura wa kusikiliza kesi dhidi ya Mandla ili kumaliza mgogoro ambao ulikuwa ukiendelea wakati Mandela akiwa hospitalini.
Hata hivyo taarifa ya Ikulu ilisema:
‘Tunarejea taarifa yetu ya awali kwamba Rais Zuma alimtembelea Madiba hospitalini na hali yake bado ni mbaya lakini imara’.
Iliongeza: ‘Madaktari wamekanusha taarifa kwamba eti Mandela yuko katika hali ambayo hawezi kupona’.
Itakumbukwa kuwa Juni 26 mwaka huu tarehe inayoonekana kwenye nyaraka za mahakama ndiyo siku ambayo Rais Zuma aliahirisha safari yake ya kwenda Msumbiji kuhudhuria kikao cha wakuu wa SADC kwa maelezo kwamba hali ya Mandela ilikuwa hairuhusu.
Hata hivyo tangu Juni 27, taarifa za Serikali zimekuwa zikitolewa kwamba hali ya mzee huyo ilibadilika na kuonekana kupata nafuu, na Rais Zuma amekuwa akiwahamasisha wananchi wa Afrika Kusini kujiandaa kwa maadhimisho ya miaka 95 ya Mandela ifikapo Julai 18 mwaka huu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment